Benki ya Exim Tanzania imesherehekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa kuitambulisha rasmi huduma yake mpya ya akaunti maalum kwa ajili ya wanawake ijulikanayo kwa jina la ‘Supa Woman’ ambayo pamoja na faida nyingine inalenga kusogeza karibu na kuhamasisha huduma za kibenki kwa kundi hilo muhimu.

Hafla ya utambulisho wa huduma hiyo yenye kauli mbiu ‘Unaweza Yote’ imefanyika katikati ya wiki jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wafanyakazi wanawake wa benki hiyo ikiwa ni muendelezo wa utambulisho wa huduma hiyo iliyozinduliwa mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Arusha na Mkuu wa Mkoa huo Bw John Mongella alipokuwa akifungua Maonesho na Mkutano wa pili wa wanawake na vijana wafanyabiashara barani Afrika uliofanyika jijini humo.

Akizungumza kwenye hafla hiyo Mkuu wa Matawi ya Benki ya Exim Bi. Agnes Kaganda alisema katika kuadhimisha Siku ya wanawake Duniani benki hiyo iliona umuhimu wa kutambulisha huduma hiyo mpya ili kuthibitisha dhamira yake katika kuwakomboa kiuchumi wanawake nchini kwa kutoa upendeleo maalum kwenye huduma zake.

“Kama ilivyo kauli mbiu ya Siku hii mwaka huu ni ‘‘Ubunifu na mabadiliko ya Teknolojia, chachu katika kuleta usawa wa kijinsia’ huduma hii ‘Supa Woman’ inahusisha mapinduzi makubwa ya kidijitali na teknolojia kwenye utoaji huduma za kibenki lengo likiwa ni kuondoa vikwazo na usumbufu ambao kwa kiasi flani umekuwa ni moja sababu ya wanawake wengi kukwepa kutumia huduma rasmi za kibenki,’’ alisema.

Zaidi, akizungumzia huduma hiyo Bi Kaganda alisema inalenga kurahisisha uendeshwaji wa biashara miongoni mwa wafanyabiashara wanawake nchini wenye umri kuanzia miaka 18 kwa kuwawezesha kupata mikopo ya dharura ya hadi asilimia 90 ya kiasi kilichopo kwenye akaunti au hati fungani, mikopo ya nyumba na mikopo ya kawaida ya biashara.

“Zaidi pia kupitia akaunti hii wateja wetu ambao ni wanawake wataweza kupata huduma ya bima ya maisha bure, riba yake inahesabiwa na kuliwa kwa muda atakaochagua mteja mwenyewe, inawawezesha kufanya manunuzi mtandaoni au sehemu yoyote kwa kuwa inawawezesha kufanua miamala kwa urahisi kupitia njia ya simu, mtandaoni au kupitia wakala wa benki yetu,’’

“Pamoja na dhamira yetu ya dhati ya kuwa karibu zaidi na wanawake, huduma hii mpya ni muitikio wa maoni ambayo tumekuwa tukiyapokea kutoka kwa wadau wetu mbalimbali wakiwemo wateja wetu wanawake ambao kiukweli wana ndoto kubwa za mafanikio kwenye shughuli zao hivyo na sisi tukaona tuna jukumu la kwenda nao sambamba katika kufanikisha malengo yao,’’ alisema.

Akizungumzia utambulisho wa huduma hiyo kipindi hiki Mkuu wa Bidhaa za Rejareja na Uhakika wa Mapato wa Benki ya Exim, Bi. Mtenya Cheya alisema imekuja wakati muafaka kutokana na mwamko mkubwa wa wanawake katika kuchangamkia fursa mbalimbali za biashara kutokana ongezeko la muingiliano wa kibiashara baina ya wananchi wanaounda Jumuiya ya Afrika Mashariki na mataifa mengine jirani.

“Kwasasa ni kitu cha kawaida kukuta wanawake wa Kitanzania wapo nchi jirani wakifanya biashara zao. Na kwa kuwa benki ya Exim ni moja ya benki ambazo zina matawi mengi zaidi nje ya mipaka ya Tanzania tunaamini ujio wa akaunti hii utakuwa msaada mkubwa kwao,’’ alisema.

Mkuu wa Matawi ya Benki ya Exim Bi. Agnes Kaganda (wa pili kushoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitambulisha huduma mpya ya akaunti maalum kwa ajili ya wanawake ijulikanayo kwa jina la ‘Supa Woman’ ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani wakati wa hafla ya kusherekea siku hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam katikati ya wiki. Wengine ni pamoja na Mkuu wa Matawi wa Kanda Benki ya Exim, Bi Elizabeth Mayengo (Kulia), Mkuu wa Bidhaa za Rejareja na Uhakika wa Mapato wa Benki ya Exim, Bi. Mtenya Cheya (wa pili kushoto) na Meneja Msaidizi Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo Bi Mariam Mwapinga (kushoto).

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim Bw Jaffari Matundu (katikati) akiwaongoza wafanyakazi wengine wa benki hiyo kuonyesha ishara maalum inayotumika katika maadhimisho ya Siku ya wanawake Duniani.





Wafanyakazi wa benki ya Exim wakiwa kwenye matukio tofauti ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya wanawake Duniani.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...