- Amechaguliwa kwenye Mkutano Mkuu wa 73 wa FIFA
- Kwa mara ya kwanza Mkutano huo umefaninyika barani Afrika
Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
Rais wa Shirikisho la Soka dunia (FIFA), Gianni Infantino ataendelea kuwa Rais wa Shirikisho hilo baada ya kuchaguliwa tena kwenye kipindi kingine cha miaka minne (2023-2027) kwenye Mkutano Mkuu wa 73 uliofanyika mjini Kigali nchini Rwanda.
Akizungumza baada ya kuchaguliwa, Rais Infantino amesema kuwa nafasi ya Rais wa FIFA ni uwajibikaji, huku akisisitiza ushirikiano baina ya Wanachama wote 211 wa Shirikisho hilo. “Nifuraha kwangu kuchaguliwa tena kuwa Rais wa Shirikisho hili la soka duniani kwa kipindi kingine cha miaka minne.”
Aidha, katika hotuba yake Rais Infantino ameahidi kusimamia mashindano mbalimbali ya soka ulimwenguni na kuhakikisha mchezo wa mpira wa miguu unaendelea na kukua, ikiwa sanjari na kuongeza zawadi katika mashindano mbalimbali yanayoendelea ulimwenguni.
“Tuweke wazi, mashindano ya Kombe la Dunia kwa Wanawake yanayoshindanisha timu 32 duniani kote, yatakayofanyika nchini Australia na New Zealand mwaka huu, tutaongeza zawadi kwa washindi kufikia hadi kiasi cha fedha cha ‘USD 150 Millions’, thamani hii ni zaidi ya mara tatu ya mashindano haya ya mwaka 2019 na zaidi ya mara 10 katika mashindano ya 2015,” amesema Rais Infantino.
Rais Infantino amesema wataboresha mashindano ya Kombe la Dunia kwa vijana (Wavulana na Wasichana) ili kuchezwa kila mwaka sanjari na kueleza kuwa wataendelea kuboresha mashindano ya Kombe la Duna kwa ngazi ya vilabu ili kuzipa fursa Klabu mbalimbali duniani kushiriki kwenye mashindano ya Kimataifa.
Katika masuala ya kifedha, Rais Infantino amesema katika miaka minne ijayo Shirikisho hilo linatajwa kuingiza kiasi cha fedha, Dola za Kimarekani Bilioni 11 ambayo ni ongezeko kubwa la lengo, tofauti na miaka minne iliyopita ambayo ilikuwa Dola Bilioni 6.4 na ongezeko la Dola Bilioni 7.5 za mapato ambayo iliripotiwa.
Hata hivyo, ni mara ya kwanza kwa Uchaguzi wa Shirikisho hilo kufanyika barani Afrika, Mkutano huo ulifunguliwa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame. Jumla ya Wanachama 208 walihudhuria Mkutano huo, licha ya mataifa mawili ya Zimbabwe na Sri Lanka kuripotiwa kusimamishwa uanachama.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...