Na Mbaraka Kambona, Lindi

Kamati ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imesema pamoja na hatua nzuri ya ujenzi wa bandari ya uvuvi iliyofikiwa, ni muhimu Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha kasi ya ujenzi huo inaongezeka ili kutimiza adhma ya Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwa na bandari ya kwanza ya kisasa ya Uvuvi hapa nchini.

Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara Kilimo na Mifugo, Mhe. David Kihenzile wakati wa ziara yao ya kutembelea Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi waliyoifanya Wilayani Kilwa, Mkoani Lindi Machi 16, 2023.

Mhe. Kihenzile alisema kuwa Serikali imetenga pesa za ujenzi wa bandari hiyo kwa lengo la kuongeza kasi ya uvunaji wa rasilimali za uvuvi ili ziweze kusaidia kuinua uchumi na kuongeza fedha za kigeni ndani ya nchi.

Aliongeza kwa kusema kuwa Serikali inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kutengeneza ajira Milioni 8 kwa ajili ya vijana kupitia Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi, hivyo ujenzi wa bandari hiyo utakuwa ni sehemu ya majawabu ya upatikanaji wa ajira kwa vijana.

"Tumesisitiza kuwa kasi ya ujenzi iongezeke ili wananchi wanaosubiri waanze kunufaika na mradi huu", alisema Mhe. Kihenzile

Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega alisema kuwa wamepokea maelekezo, ushauri na maoni ya kamati hiyo huku akisistiza kuwa kasi ya ujenzi wa bandari hiyo itaendelea kuwa kubwa zaidi ili waweze kutimiza adhma ya Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwa na bandari ya uvuvi ya kwanza na ya kihistoria hapa nchini.

Sambamba na hilo, Waziri Ulega ameitaka kampuni inayosimamia ujenzi wa Mradi huo ya China Harbour Engineering Company (CHEC) kuhakikisha inatoa fursa za ajira kwa vijana waliokaribu na mradi huo ili na wao waweze kunufaika.

Aliongeza kwa kusema kuwa dhamira yao kama Serikali ni kuuendesha mradi huo kibiashara ili fursa nyingi za uwekezaji ziweze kupatikana na kwamba hapo mbeleni watatangaza fursa mbalimbali za uwekezaji hususani Viwanda ili kuchechemua uchumi wa Mkoa wa Lindi na nchi kwa ujumla wake.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa jumla ya Tsh. Bilioni 266.7 kwa ajili ya Ujenzi wa mradi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko Mkoani Lindi ambao unatarajiwa kukamilika mwaka 2024.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...