Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya miundombinu Mhe Seleman Kakoso ameitaka TRC Kuwekeza kwenye Karakana ili iweze kuzalisha wataalamu na vifaa ambavyo kwa sasa vinaletwa kutoka nchi za nje kwa ajili ya ujenzi,ukarabati na utekelezaji wa miradi ya Reli Nchini

Ameyasema hayo leo wakati kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ilipotembelea na kukagua karakana ya ukarabati wa vichwa vya Treni ya kawaida-MGR iliyopo Mkoani Morogoro

“Wekeni bajeti nzuri ambayo itasaidia karakana kutengeneza vifaa ambavyo vinawezekana kutengenezwa hapa Nchini, ukizingatia tunaelekea kipindi cha bajeti kuu ya Serikali hivyo shirikianeni na Wizara na sisi kama kamati tupo tayari kuwaunga mkono” amesisitiza Mhe Kakoso

Kwa upande wake Naibu Waziri Sekta ya Uchukuzi, Mhe Atupele Mwakibete amesema Serikali ya Awamu ya sita inaeendelea kutenga Fedha kwa ajili ya kukarabati vichwa na mabehewa ya treni ili kuboresha huduma ya Reli ya kati Nchini ambapo tarehe 30 juni, 2021 Serikali ya awamu ya sita iliiingia mkataba wa Dola za Kimarekani Mil 10.5 na kampuni ya SMH RAIL kutokea nchini Malaysia kwa kutumia karakana ya Morogoro kufanya ukarabati mkubwa wa vichwa vya treni ya kawaida-MGR

‘‘Ukarabati huu ni wa kufufua vichwa vya treni ya kawaida tisa vya Reli ya kati ambapo viwili ni vya njia kuu na saba ni vya sogeza na unaohusisha ufungaji wa vipuri vipya, Engine Mpya, Bogi mpya na unatarajiwa kukamilika ifikapo julai,2023.” amesisitiza Mhe Mwakibete

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la reli Tanzania bi Amina Lumuli amesema Karakana ya Vichwa vya Treni Morogoro inakumbana na changamoto mbalimbali kama vile ugumu wa upatikanaji vipuri kwa wakati, pamoja na upungufu wa rasilimali fedha.

Shirika la Reli Tanzania lina jumla ya vichwa vya Treni ya kawaida-MGR 59,vichwa 43 vikiwa vya njia kuu na 16 vikiwa vya Sogeza na kati yake vichwa vinavyofanya kazi ni 44 ambapo vichwa 30 ni njia kuu na vichwa 14 sogeza na limeendelea kukuza wataalamu wa ndani kwa kuwapatia ujuzi wa kimasomo ndani na nje ya nchi ili kuendana na teknolojia ya kisasa na mabadiliko ya mara kwa mara ya vipuri kwa minajili ya kuboresha usafiri wa reli ya kawaida Nchini kwa maslahi ya Taifa.

Kichwa cha Treni ya kawaida-MGR cha kuvutia mabehewa ya abiria na mizigo kwa njia kuu aina ya 88 class kikifanyiwa ukarabati ndani ya Karakana ya Ukarabati wa Vichwa vya Treni ya kawaida-MGR Mkoani Morogoro

Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi anayeshughulikia Sekta ya Uchukuzi Mhe Atupele Mwakibete akifafanua jambo kwa Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe Selemani Kakoso na Wajumbe wa kamati hiyo wakati wakitembelea na kukagua Karakana ya Ukarabati wa Vichwa vya Treni ya kawaida-MGR Mkoani Morogoro.

Fundi Sanifu na Msimamizi wa sehemu ya bogi Ndugu James Mlosa akifafanua jambo kwa Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakati   kamati hiyo ilipotembelea na kukagua Karakana ya Ukarabati wa Vichwa vya Treni ya kawaida-MGR Mkoani Morogoro.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...