Raisa Said,Kilindi
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Tanga Husna Sekiboko amewataka Wazazi na Walezi kuhakikisha wanawekeza katika elimu ya awali na msingi ili kuwajengea uwezo watoto wao ambao ni taifa la kesho.
Wito huo ameutoa wakati akizungumza na Wazazi na Walezi katika ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo aliyoifanya Wilayani Kilindi.
Sekiboko ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge elimu ,Utamaduni Sanaa na michezo alisema kuwa kila mzazi anajukumu la kumuandikisha mtoto wake ili aweze kupata haki yake ya elimu ambayo kwasasa Serikali ya awamu ya sita imekuwa ikitoa bure katika shule zote.
" Jukumu letu sisi Wazazi ni kuhakikisha tunawekeza katika elimu ya watoto wetu kuanzia ngazi ya elimu ya awali na msingi ili tuweze kujenga msingi bora ya kielimu Kwa watoto wetu " Alieleza Sekiboko.
Sekiboko alieleza elimu ya awali au chekechea ni msingi wa elimu kwa watoto ambapo Kila hatua ya elimu inayofuata inategemea mafanikio ya msingi huo,lakini bado watoto wengi duniani kote wananyimwa fursa hii.
Sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) 2012- 2016, vimebainisha kuwa Elimu ya Awali ni moja kati ya vipaumbele vya serikali. Aidha, kila shule ya msingi inatakiwa kuwa na darasa la elimu ya awali.
Mwaka 2016, Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) iliboresha mtaala wa elimu ya awali,Mtaala huo ulianza kutumika rasmi mwaka 2017,Baada ya uboreshaji, baadhi ya walimu wa elimu ya awali walipata mafunzo ya namna ya kutekeleza mtaala huo.
Hata hivyo, imeonekana kuwa kuna haja ya kuwajengea uwezo walimu wote wa elimu ya awali katika ufundishaji na ujifunzaji wa mtoto. Hivyo, TET kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la Aga Khan Foundation (AKF) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto “UNICEF “ waliandaa moduli za mafunzo kazini kwa walimu wa elimu ya awali kwa kuzingatia mtaala wa elimu ya awali wa mwaka 2016.
Kwa upande wao Wazazi na Walezi walioshiriki kikao hicho na Mbunge huyo wa Viti Maalum wamesema kuwa watahakikisha wanawekeza katika elimu ya awali ili kuwajengea uwezo wa kitaaluma watoto wao.
Amina Omari Mkazi wa Kwediboma alisisiza kuwa suala la elimu ni msingi imara wa maisha ya badae Kwa watoto wao hivyo atahakikisha anashauriana na mwenza wake kuhakikisha wanawekeza kipaumbele katika kuwekeza katika elimu kwanzia ngazi ya elimu na msingi .
Kwa upande wake Kaimu Ofisa Elimu Wilaya ya Kilindi ambaye ni ofisa Elimu kata ya Negero Wilayani humo Linus Shechambo alisema kuwa awali walikuwa wanafanya uhamasishaji wa uwekezaji wa elimu katika mikutano mbalimbali ya Wazazi na Walezi wanapokutana.
Shechambo alieleza kuwa kulingana na uhamasishaji wa uwekezaji wa elimu wanaofanya umesaidia kuvuka lengo la uwandikishaji wa elimu ya awali namsingi katika mwaka huu wa 2023
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...