Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu yaishauri Serikali kupitia Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS)  kuanza na mfumo wa barabara zenye tozo katika mradi wa  ujenzi wa barabara njia nane kutoka Kimara Jijini Dar es Salaam hadi Kibaha mkoa wa Pwani ili kuweza kuongeza mapato.

Ushauri huo umetolewa wakati Kamati hiyo ilipofanya ziara kutembelea mradi wa barabara wa njia nane ambapo waliongozana na viongozi na watumishi kutoka Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) kuona maendeleo ya mradi huo ulipofikia pamoja na kuona changamoto zilizopo.

Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa Kamati hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kuduma ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Selemani Kakoso amesema duniani kote, barabara nyingi zinajengwa kwa mfumo kama wetu ambao ulishaanza muda mrefu na sheria inatukataza huwezi kuwa na barabara ya tozo kama huna njia nyingine mbadala.

Aidha amesema katika mradi wa barabara kunatakiwa pia kuimarishwa kwa mifumo ya mifereji kwaajili ya majitaka kwani mvua zinaponyesha maji yanashindwa kwenda kwenye maeneo husika na kuleta kero kwa watumiaji wa barabara.

Pamoja na hayo Kamati hiyo imeridhishwa na miundombinu inayojengwa katika Mkoa wa Dar es Salaam na kuipongeza Wizara kwa usmamizi mzuri ambao wanaufanya kupitia TANROADS kujenga miundombinu ya barabara nchini.

"Tumeiona dhamira ya Serikali kupunguza msongamano ambao wanaamini utarahisisha shughuli nzima kwenye sekta ya uchukuzi". Amesema Mhe.Kakoso.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema kumekuwa na ongezeko la gharama kubwa kwenye ujenzi wa miundombinu kutoka kwenye gharama ya mwanzo mpaka mradi unapokaribia kuisha gharama zinaongezeka kutokana na usanifu wa ujenzi wa miundombinu mipya.

Naye Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Rogatus Mativila, amesema mradi huo uliogharimu shilingi za kitanzania bilioni 218 umejengwa na Mkandarasi mzawa kutoka kampuni ya ESTIM CONSTRUCTION umefikia asilimia 98 na unatarajia kukamilika mwezi ujao.

Mhandisi Mativila amesema watahakikisha wanayasimamia kikamilifu maelekezo na ushauri ili kufikia matarajio yanayokusudiwa hasa katika uboreshaji wa miundombinu ya barabara.

Muonekano wa sehemu ya barabara ya njia nane kutoka Kimara hadi Kibaha (km 19.2),jijini Dar es Salaam. Ujenzi wa barabara hiyo umefikia asilimia 98 na unatarajia kukamilika ifikapo mwisho wa mwezi April, 2023.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...