Na Abby Nkungu, Singida

KUANZISHWA kwa shule shikizi tisa katika Manispaa ya Singida kumetajwa kuwa ni mwarobaini kwa watoto walio chini ya miaka minane kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 10 kila siku kufuata elimu kwenye shule mama, kuimarisha ulinzi na usalama wao na kupunguza utoro na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Afisa elimu Msingi katika Manispaa ya Singida, Omary Maje alibainisha hayo wakati akizungumzia mafanikio na changamoto za shule shikizi katika halmashauri hiyo.

“Kuanzia mwaka 2017 hadi sasa, tumefanikiwa kuwa na shule shikizi tisa ambazo kwa kweli zimesaidia watoto wadogo; hasa wa chekechea, wa darasa la kwanza na la pili kutembea umbali mrefu kutafuta elimu; hivyo kumaliza utoro, vitendo vya ukatili wa kijinsia njiani au usalama wao kuwa mashakani wanapokutana na wanyama kama fisi” alisema.

Alieleza kuwa baadhi ya shule za msingi mama zipo umbali wa kilomita 5; hivyo ilikuwa vigumu kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka minane kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 10 kila siku kufuata elimu; hivyo Manispaa kuamua kuanzisha shule shikizi jirani na makazi ya watu kuondoa changamoto hiyo.

Maje alizitaja shule hizo Shikizi kuwa ni pamoja na Mnung’una, Mughenyi, Manguampyughu, Sundu, Mwembemoja, Mwachichi, Nkuhi, Mwaghumpi na Makyunje ambazo hadi hivi sasa zina jumla ya wanafunzi 2,665 kati yao wavulana ni 1,316 na wasichana 1,349.

Alisema kuwa kuendelezwa kwa shule hizo ni sehemu ya utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa juu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ya mwaka 2021, ambayo pamoja na mambo mengine, inaweka mkazo zaidi kwenye kuimarisha ulinzi na usalama, afya, lishe bora, elimu na malezi yenye mwitikio kwa watoto wenye umri wa miaka 0 hadi 8.

Hata hivyo; anakiri kuwa bado shule hizo shikizi zinakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo kutokuwa na miundombinu ya kutosha kama madarasa, vyoo na nyumba za walimu huku zikiwa hazina fungu la uendeshaji hivyo kuendelea kutegemea fungu lililoko shule mama na hakuna walimu wa kudumu kwani walimu wake hutegemea zaidi kutoka shule mama na wale wa kujitolea.

Baadhi ya wazazi na walezi wanaipongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa kuanzisha shule shikizi ili kupunguza changamoto kwa watoto na kuomba ziboreshwe na kusajiliwa kuwa shule kamili.

“Mimi mtoto wangu aliponea pale Mwembemoja ndio ikawa nafuu; vinginevyo ilikuwa aache shule kabisa au nimtafutie hizi za kuchukuliwa na magari maana mtoto alikuwa akitembea zaidi ya kilomita saba kwenda tu bado kurudi, akija nyumbani amechoka mpaka basi” alisema Halima Ali mkazi wa Mtipa Singida na kuongeza kuwa sasa shule hiyo imepata usajili kamili.

Naye, Ibrahimu Loth mkazi wa Mwenge anapongeza kuanzishwa kwa shule hizo shikizi kwani kwa dunia ya sasa watoto wadogo kutembea umbali mrefu ni hatari kwani wanaweza kufanyiwa vitendo vya ukatili ikiwemo ulawiti, kubakwa au kujeruhiwa na wanyama.

Walimu wa shule za awali na msingi katika Manispaa ya Singida wanasema kuwa shule shikizi zinaweza kusaidia kuinua kiwango cha elimu kwani awali watoto walikuwa wanafika shule wakiwa wamechoka kwa kutembea umbali mrefu na muda wote wakipiga miayo tu darasani kwa uchovu na njaa.

“Mengine huwa hatusemi tu ingawa tunaumia maana na sisi pia ni wazazi. Ukipewa kufundisha darasa la awali na la kwanza duh! ikifika saa 4 asubuhi watoto wote wanaotoka mbali unakuta wanachapa usingizi darasani na walio macho ni miayo kwa kwenda mbele, ila sasa kwa hizi shikizi watoto hawatembei umbali mrefu hivyo hawachoki, tunaishukuru Serikali” alisema mmoja wa walimu hao.

Kulingana na taarifa za idara ya elimu Manispaa ya Singida, kati ya shule 9 shikizi zilizoanzishwa, shule 5 tayari zimesajiliwa na Wizara ya elimu kuwa shule kamili huku nyingine zikiwa kwenye mchakato wa kusajiliwa.

Afisa elimu Msingi katika Manispaa ya Singida, Omary Maje akiwa kwenye moja ya vikao vyake kuelezea umuhimu wa Shule Shikizi


Moja ya shule Shikizi katika Manispaa ya Singida.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...