Na Immaculate Makilika - MAELEZO
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Wilaya nchini kuhakikisha huduma za jamii zinawafikia wananchi katika maeneo yao.
Hayo ameyasema Machi 18, 2023 jijini Dodoma wakati akifunga Mafunzo ya Uongozi kwa Wakuu wa Wilaya Tanzania Bara.
"Simamieni utoaji wa huduma za jamii katika maeneo yenu hakikisheni suala la elimu limetengamaa wanafunzi wanaenda shuleni na madarasa yapo ya kutosha" amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Aidha, amesitiza "miundombinu iimarishwe kupitia mapato ya ndani, huduma za afya zitolewe pamoja na kutatua migogoro ya watumishi wa umma na wanachi"
Katika hatua nyingine, Mhe. Waziri Mkuu Majaliwa amewataka Wakuu hao wa Wilaya kusimamia shughuli zinazoleta uchumi utakaonufaisha wananchi.
Sambamba na kuvutia wawekezaji na kuwaratibu vizuri wafanyabiasha wadogo wadogo katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Angela Kairuki amesema kuwa baada ya mafunzo hayo kwa Wakuu wa Wilaya 138 ya namna ya kuongoza na kusimamia rasilimali watu na fedha na kuwajengea uwezo katika masuala muhimu yanahohusu utekelezaji wa majukumu yao yatawaongeza ufanisi katika shughuli zao.
"Tunaamini mkirudi katika maeneo yenu ya kazi mtatekeleza yale yote mliyoelekezwa kwa kushirikiana na viongozi wenzenu, watumishi wa umma na wadau na kuepuka migogoro ya kiutendaji katika maeneo yenu ya kazi" ameeleza Waziri Kairuki.
Mafunzo hayo ya Uongozi kwa Wakuu wa Wilaya Tanzani Bara yameandaliwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Taasisi ya Uongozi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...