Na Said Mwishehe, Michuzi TV

KATIKA kuelekea Siku ya Utepe Mweupe ambayo huadhimishwa Machi 15 ya kila mwaka, Muungano wa Utepe Mweupe kwa Uzazi Salama(White Ribbon Alliance) umeomba waandishi wa habari nchini kutoa taarifa zinazokwenda sawa na kauli mbiu ya Siku hiyo.

Kauli mbiu ya mwaka huu kwenye Siku ya Utepe Mweupe inaeleza hivi “Kila mwanamke anastahili huduma bora na jumuishi za uzazi zenye staha na hesima.

Akizungumza leo Machi 13,2023 kwenye mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa ofisi za Thamini Uhai jijini Dar es Salaam , Mratibu wa Muungano wa Utepe Mweupe Tanzania Rose Mlay amesema katika kuelekea siku hiyo wameamua kukutana na waandishi wa habari wakiwaomba watoe taarifa sahihi kwa lengo la kuisaidia jamii.

“Tumewakumbusha waandishi wa habari katika kuelekea siku hiyo tunawaomba Ombi letu kwa waandishi wa habari watoe habari sawa na kauli mbiu inavyosema kuwa Kila mwanamke anastahili huduma bora na jumuishi za uzazi zenye staha na heshima.

“Katika huduma jumuishi tunaona kuna watu hatujawajumuisha kama walemavu wa viungo, akili na wale ambao wako chini ya miaka 18 na wamepata ujauzito. Kwa hiyo tunaomba waandishi waingie mtaani kuzungumza na wale akina mama yaani kwenye jamii.

“Wamama wenye hizi changamoto tunatamani tukiwasikia wakisema wangependa wafanyiwe nini ili wakienda hospitali waridhike na huduma wanazopata na wafurahi kutokana na hali ambazo zinachangamoto kidogo,”amesema Mlay.

Akielezea zaidi siku ya Utepe Mweupe amesema wanatarajia kutakuwa na wadau mbalimbali wakiwemo wananchi, wafanyakazi wa afya na viongozi wa ngazi wa Serikali ili kwa pamoja wajadiliane kuhusu kauli mbiu ya Kila mwanamke anastahili huduma bora na jumuishi za uzazi zenye staha na heshima

“Na ni nini kifanyike ili hata ambao wanachangamoto kama ulemavu yaani kwa pamoja wafanye nini , hivyo tunaomba vyombo vya habari vipeleke hizo habari mpaka ziwafike wananchi wote.”

Mlay ameeleza mbali ya kauli mbiu hiyo kuna mambo ya msingi ambayo yatajadiliwa hasa katika eneo la faragha kwa wanawake wakati wa kujifungua, kuna chumba cha kujifungulia kwa ajili ya faragha ili mjamzito hasa mlemavu au chini ya miaka 18 awe na msindikizaji.

Mengine watakayojadili katika siku hiyo ni Mazingira rafiki ya kujifungulia kwa mjamzito mlemavu kwa mfano kitanda na choo pamoja na vitendo , lugha ya upendo na staha kwa kila mjamzito.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Thamini Uhai Banzi Msumi amesema katika kuelekea siku hiyo wao kama moja ya wadau ambao wako kwenye Muungano wa Utepe Mweupe wanaunga mkono uwepo wa siku hiyo.

“Tunaungana na wadau wote katika kuadhimisha siku hiyo yenye kauli mbiu inayosema Kila mwanamke anastahili huduma bora na jumuishi za uzazi zenye staha na heshima. Kama kauli mbiu ilivyokaa, Thamini Uhai tunasisitiza zaidi Serikali kuendelea kushirikiana na wadau kutengeneza usiri kwa wanawake wakati wote wa kujifungua.

Pia kuwepo na vyumba ambavyo vitaangalia faragha pamoja na makundi mbalimbali maalumu kama walemavu na akina mama ambao wako chini ya umri wa miaka 14 lakini pia kuweka mazingira rafiki ya kujifungulia kwa wajawazito walemavu kwa mfano kitanda na choo kwa ajili ya wamama wenye ulemavu.

“Lakini vitendo pamoja na lugha za staha na upendo kwa kila mjamzito na kama kauli mbiu ilivyokaa na hivi viambatanishi vyake sisi tuko pamoja na siku hii tunayoisubiria kwa furaha sana.”

01:Mratibu wa Muungano wa Utepe Mweupe Tanzania Rose Mlay akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuelekea siku ya Utepe Mweupe inayoadhimishwa Machi 15 ya kila mwaka.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Thamini Uhai Banzi Msumi akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mkutano huo ambapo ametumia nafasi hiyo kueleza wao kama mmoja ya wadau wanaungana na waday wengine kuelekea siku hiyo.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...