Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi( CCM) Daniel Chongolo amempa siku 10 Waziri wa Maji Jumaa Aweso awe amefika kwenye Kijiji cha Uhambingeto kilichopo jimbo la Kilolo ambako mradi wa maji umekwama na hivyo kusababisha changomoto ya uhaba wa maji.
Akizungumza leo baada ya kupokea kilio cha wananchi kuhusu kukwama kwa mradi huo, Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo amesema haiwezekani fedha itolewe na mradi huo ushindwe kukamilika wakati wananchi wanahitaji maji.
Wakati anaendelea kuzungumzia changamoto hiyo, Chongolo amesisitiza lazima Waziri wa Maji afike Uhambingeto ndani ya muda huo wa siku 10 ambao ameutoa ili ashughulikie kilio hicho huku akitaka hadi ifikapo Septemba 30, wananchi hao wawe wamepata maji.
Chongolo ambaye alionesha kutofurahishwa na kukwama kwa mradi huo amesema haridhishwi na kukwama kwa mradi huku akisisitiza hawawezi kwenda kwa stahili hiyo.
Hata hivyo amesema katika kuanza kutafuta suluhu ya changamoto hiyo anatoa matanki mawili ya kuhifadhia maji huku akisisitiza lazima wananchi hao wapatiwe maji haraka.
Awali akizungumza kwa niaba ya wananchi mbele ya Chongolo Diwani wa Kata ya Uhambingeto, Tulinumtwa Mlangwa amesema mradi wa maji Uhambingeto unaotekelezwa na Mkandarasi Mshamind Co LTD na gharama yake ni Sh.bilioni 2.1 na tayari Sh.bilioni 1.3 zimeshatolewa.
Hata hivyo diwani huyo alijikuta anashindwa kuvumilia hivyo akaanza kuangua kilio mbele ya Chongolo huku akieleza kutokamilika kwa mradi huo wananchi wanalazima kufuata maji kwenye bwawa ambayo sio safi na salama.
"Mkandarasi amekuwa mwiba mkubwa kwa wananchi wa kata hii na hivyo kusababisha chuki kwa Chama na Serikali kutokana na ucheleweshwaji wa mradi huo.Kuna miradi ya maji ambayo iliukuta mradi huu unatekelezwa na imeshakamilika,tunahitaji nguvu ya ziada ili kuokoa afya ya wananchi."
Ameongeza Mkandarasi alifika kwenye kijiji hicho kujitambulisha na akaahidi kuwa mpaka Februari utakuwa umekamilika.Baadae akarudi Aprili akaeleza watakamilisha mradi huo.
Kwa upande wake mbunge wa Jimbo la KiloloJustine Nyamoga amesema ameshahangaika kufuatilia mradi huo lakini hakuna majibu na sasa wananchi wananunua ndoo ya maji kuna wakati inafika kwa Sh.5000.
Baadhii ya Wananchi wakimsikiliza katibu Mkuu wa CCM Ndugu Daniel Chongolo alipokuwa akitoa malekezo kufuatia kukwama kwa mradi wa maji zaidi ya miaka kumi katika Kijiji cha Uhambingeto kilichopo jimbo la Kilolo,mkoani Iringa
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...