Na Said Mwishehe, Michuzi TV

MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) imesema kampuni 1188 nchini pamoja na 112 kutoka mataifa mbalimbali yanatarajiwa kushiriki katika Maonesho ya 47 ya Kibiashara Kimataifa yanayotarajia kuanza Juni 28 huu hadi Julai 13 mwaka huu.

Kwa mujibu wa Tantrade hadi sasa mataifa 14 yamethibitisha kushiriki katika maonesho hayo na lengo la mwaka huu ni kuwa na mataifa 30 na kwamba kwa muda uliobakia wanaamini idadi hiyo itafikiwa kutokana na mvuto wa maonesho hayo.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji biashara kutoka TanTrade, Fortunatus Mhambe ameyasema hayo leo Mei 19, 2023 jijini Dar es Salaam alipokuwa akielezea maandalizi ambayo yameanza kuelekea msimu wa maonesho hayo.

"Maonesho yataanza Juni 28 mwaka huu mpaka Julai 13,  na mpaka hivi sasa tunavyoongea nchi  takribani 14 ikiwemo China,  Umoja wa Falme za Kiarabu, India na nchi nyingine za Afrika Mashariki tayari zimethibitisha,  kwa mwaka huu matarajio yetu ni kuwa na mataifa 30,  kwa muda huu uliobakia tunaamini malengo ya kuwa na mataifa hayo yatayatimia, " amesema.

Amesema kauli mbiu inasema Tanzania, mahali sahihi pa biashara na uwekezaji huku akifafanua malengo makuu ya maonesho hayo ni kuwakutanisha wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi na kuwapa fursa ya kutangaza bidhaa na huduma zao pamoja na kutafuta masoko.

"Maonesho ya 47 ya biashara ya Kimataifa Dar es Salaam yatakuwa na maeneo mbalimbali yaliyoboreshwa na programu za kuvutia ikiwemo ya Sabasaba Expo Village ambalo ni eneo ambalo litatumika kutangaza fursa zilizopo kwenye  sekta ya madini, Tehama, gesi na mafuta, mazingira, sanaa, vijana pamoja na wanawake," amesema

Ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wafanyabiashara kushiriki  maonesho hayo ya 47 pamoja na kutembelea banda maalum la Sabasaba Expo Village ili kuchangamkia fursa zilizopo na kuongeza kuwa hiyo ni nafasi nzuri kwa wajasiriamali kukuza na kujenga mtandao wa kuinua biashara zao.

"Hata hivyo Sabasaba Expo Village inatoa jukwaa la kujenga mtandao wa kibiashara kwa wafanyabiashara na kuwapa fursa ya kuanzisha mawasiliano na wenzao, kubadilishana uzoefu na kujenga ushirikiano mpya, eneo hili litawavutia wageni kutoka ndani na nje ya nchi wakiwemo wawekezaji,  wafanyabiashara na wadau wengine wa biashara," amesema

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), Mwajuma Hamza ameeleza katika kipindi hiki cha kuelekea maonesho hayo wataendelea kuwahamasisha na kuwawezesha wanawake wajasiriamali kushiriki maonesho hayo.

"Maonesho haya yamesaidia wajasiriamali wetu kupata masoko ya uhakika,  hivyo ushiriki ni mkubwa na tunawaahidi TanTrade kuwa tutaendelea kuyatangaza maonesho haya ambayo yanatoa fursa ya watu kujitangaza na kuuza biashara zao kwa viwango wa hali ya juu," amesema

Wakati huo huo Kaimu Mkurugenzi Taasisi ya  Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA), Mwanakhamis Hussein   amesema wataendelea kuwaelimisha wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kushiriki maonesho hayo na fursa zilizopo ambazo zikitumika vizuri zitaendelea kuinua sekta  biashara nchini

 Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Biashara kutoka Tan Trade Fortunatus Mhembe akizungunza na waandishi wa habari leo Mei 19, 2023 jijini Dar es Salaam alipokuwa akielezea maandalizi ya Maonesho ya 47 ya Biashara Kimataifa yanayotarajia kuanza Juni 28 hadi Julai 13 mwaka huu


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...