Na Mwandishi Wetu


SHIRIKA la WaterAid Tanzania liliungana pamoja na wanafunzi na walimu katika shule ya Misima iliyoko halmashauri ya mji wa Handeni katika hafla ya kukabidhi mradi wa ukarabati wa miundombinu ya maji na mafunzo tabia siha uliofadhiliwa na shirika la Hilton Global Foundation pamoja na WaterAid.

Lengo likiwa ni kupunguza makali ya ukosefu wa maji katika shule hiyo hasa kwa watoto wa kike wanapokua katika kipindi cha hedhi sambamba na ukarabati wa huduma za maji na tabia siha.

Akizungumza kwenye Maadhimisho ya Siku ya Hedhi ambayo huadhimishwa kila Mei 8 ya kila mwaka, Mkurugenzi wa shirika la WaterAid Tanzania Anna Mzinga amesema pia wamemkabidhi mkuu wa shule cherehani moja kwa ajili ya wanafunzi kujishonea pedi za kitambaa.

Pia wamekabidhi vifaa 40 vya kushonea pedi, katoni 55 za pedi (kutumika katika kipindi cha mvua pale pedi za kufua zitashindwa kukauka), vifaa vya michezo seti 3, mabango 20 kwa ajili ya kujifunza masuala ya usafi na televisheni kwa ajili ya kujifunza tabia siha na usafi kwa ujumla.

Anna Mzinga amesema wamefanikisha ukarabati wa miundombinu kadhaa ya mfumo wa maji, matenki la kuhifadhia maji, vyoo ikiwemo kuweka muundombinu wa choo rafiki kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu na zaidi ya yote wametoa elimu kuhusu usafi kwa wasichana na wavulana katika hatua za makuzi yao binafsi.

Ameongeza hiyo ilijumuisha pia mafunzo maalumu ya namna ya kujitengezea taulo za kike za kujisitiri wakati wa hedhi ili kujilinda na adha mbalimbali wanapokua katika kipindi cha hedhi.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Handeni Upendo Magashi akizungumza kwenye hafla hiyo iliyofanyika shule ya Misima wilayani Handeni amesema miundombinu iliyopo inahitaji kutunzwa ili iweze kutoa huduma husika kwa kipindi kirefu kwa sasa na kwa wanafunzi watakaokuja.

Hata hivyo imeelezwa licha ya kwamba jitihada za dhati zimefanyika na serikali pamoja na wadau ila bado inaripotiwa kwamba asilimia 34 ya wasichana hukosa vipindi shule kutokana na upungufu wa vyumba maalumu vya kujisitiri wakati wa hedhi huku asilimia 26 kutokana na ukosefu wa maji na vyoo safi katika shule.

Mwito wa shirika la WaterAid wadau wote kupitia kauli mbiu ya kitaifa ya siku ya hedhi “ “Hedhi ni tunu na Msingi wa Afya kwa wasichana na Wanawake, Tuiwezeshe” ni kuendelea kuweka mkazo katika masuala ya hedhi iliyo salama kwa wasichana na wakina mama kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Kuhusu WaterAid ni shirika la kimataifa lenye dira ya kuhakikisha kuwa watu wote ulimwenguni wanapata maji ya uhakika, vyoo bora na huduma za usafi zilizoboreshwa ifikapo mwaka 2030.

Inafanya kazi katika nchi 28, ambapo nchi 18 zipo barani Afrika. Nchini Tanzania, shirika la Wateraid lilianza kazi 1983 na kufanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya Maji, Vyoo na Usafi binafsi katika zaidi ya mikoa 11.

Aidha shirika limeshirikiana na serikali pamoja na wadau wengine wa maendeleo na kuwafikia wananchi zaidi ya milioni nane wanaoishi maeneo ya pembezoni mwa miji pamoja na vijijini. 




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...