NDANI ya miaka miwili ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumekuwa na uimarikaji kwa mtandao wa barabara za vijijini na mijini kwa Mkoa wa Iringa hatua iliyorahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii.

Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Iringa, Mhandisi Makori Kisare anasema kabla ya Serikali ya Awamu ya Sita kuingia madarakani, TARURA Mkoa wa Iringa ilikuwa ikitengewa bajeti ya Sh bilioni 6.35 kwa ajili ya matengenezo ya barabara.

“Kiasi kilichotengwa kilikidhi kufanya matengenezo ya kilometa 780 sawa na asilimia 15 ya mtandao wote wa barabara. Hali hii ilipelekea barabara nyingi ambazo zilikuwa hazipati matengenezo kwa wakati kuzidi kuharibika.”

(TARURA) Mkoa wa Iringa unahudumia mtandao wa barabara wenye kilometa 5,162.01, kati ya hizo kilometa 2,173.433 ni za mjazio, kilometa 1,787.27 ni za mkusanyo na kilometa 1,201.31 ni za Jamii.

Mtandao huo wa barabara pia umegawanyika katika makundi matatu ambayo ni barabara za lami kilomita 167.06 sawa na asilimia 3.2, barabara za changarawe kilometa 1,372.51 sawa na asilimia 26.6 na barabara za udongo ni kilomita 3,622.44 sawa na asilimia 70.2 ya mtandao mzima.

Hali ya barabara za TARURA kwa ujumla katika Mkoa wa Iringa ni ya kuridhisha ambapo barabara za lami, changarawe na zege hupitika kirahisi majira yote ya mwaka wakati baadhi ya barabara za udongo hupitika kwa shida wakati wa mvua.

Barabara zilizo katika hali nzuri ni kilomita 2,014.45 sawa na asilimia 39, barabara zilizo katika hali ya wastani ni kilomita 1,545.91 sawa na asilimia 30 na barabara zilizo katika hali mbaya ni kilomita 1,601.65 sawa na asilimia 31.
Mhandisi Kisare anasema baada ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia kuingia madarakani, bajeti ya barabara imeongezwa hadi kufikia Sh bilioni 16.3 sawa na ongezeko la asilimia 259 ya bajeti ya awali.

“Ongezeko hili limeweza kukidhi kufanya ujenzi na matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilometa 1533 sawa na asilimia 30 ya mtandao wote wa barabara za TARURA katika Mkoa.”

Kutokana na ongezeko la bajeti, kwa miaka miwili ya Rais Samia madarakani (2021/22-2022/23), Mhandisi Kisare anasema TARURA Mkoa wa Iringa imejenga na kufanya matengenezo kwenye mtandao wa barabara za lami zenye urefu wa kilomita 61.8.

Pia barabara za changarawe kilomita 386.82, barabara za udongo kilomita 863.07, madaraja 19, mirefeji ya maji ya mvua yaliyojengwa kwa mawe mita 9,180 na makavati 182.

“Ujenzi huo umeimarisha sana mtandao wa barabara za vijijini na mijini na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii katika maeneo yote yaliyofikiwa.”

Kuhusu miradi ya kimkakati itakayotekelezwa katika mwaka mpya wa fedha wa 2023/24, Mhandisi Kisare anasema TARURA Mkoa wa Iringa inatarajia kuanza utekelezaji wa mradi wa RISE.

“Mradi huu unaofadhiliwa na Benki ya Dunia na utatuwezesha kujenga jumla ya kilometa 33 za barabara kwa kiwango cha lami.”

Aidha, Mhandisi Kisare anasema pia kupitia mradi wa kuongeza mnyororo wa thamani ya mazao (AGRI-CONNECT) awamu ya pili, TARURA Mkoa wa Iringa inatarajia kujenga barabara yenye urefu wa kilometa 1.1 kwa kiwango cha lami.

“Miradi yote hii itaimarisha mtandao wa barabara za Mkoa wa Iringa.”

Anapozungumzia mipango endelevu, Mhandisi Kisare anasema kwa kutumia fedha zilizoongezwa, TARURA Mkoa wa Iringa imepanga kuendelea kuboresha mtandao wa barabara kwa kufungua barabara kuelekea maeneo ambayo hayana huduma ya barabara.

“Pia kuendelea kupandisha hadhi ya barabara za udongo kwenda kiwango cha changarawe na za changarawe au udongo kwenda kiwango cha lami kwa kadri bajeti itakavyoruhusu.”

Aidha, Mhandisi Kisare anasema TARURA Mkoa wa Iringa imeweka mikakati ya kuendelea kuzipandisha hadhi barabara za udongo kwenda kiwango cha lami na changarawe.

Pia kuendelea kutumia teknolojia mbadala yenye gharama nafuu kwa kutumia vifaa vya ujenzi vinavyopatikana katika mkoa wetu katika ujenzi wa barabara na madaraja.

“Pia kuimarisha matunzo ya barabara na madaraja yaliyotengenezwa ili viweze kudumu kwa muda mrefu.

Aidha, Mhandisi Kisare anatumia fursa hiyo kutoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoonozwa na Mheshimiwa Rais Samia kwa uamuzi dhabiti wa kuongozea takribani Sh bilioni 16.3 kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara zinazosimamiwa na TARURA Mkoa wa Iringa.

“Hakika tunampongeza Rais wetu shupavu, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa ongezeko fedha ambazo zimewezesha TARURA Mkoa wa Iringa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa na kuwahudumia wananchi wa Tanzania kwa kuzingatia maono, mwelekeo na mwongozo mwema wa Rais wetu Mpendwa.”

“Tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu ampe afya njema, heri na Baraka tele ili aweze kutuongoza kwa amani na upendo.”





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...