Na Said Mwishehe

KUNA mambo yanakera tena yana kera sana, ninaposema yanakera unielewe ujue, sio unatoa macho tu.

Kuna hili la wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama Machinga hasa waliopo katikati ya jiji la Dar es Salaam, najaribu kuangalia changamoto wanazokumbana nazo, hakika utawaonea huruma, wanateseka, wananyanyasika.

Ukweli hawana raha na utafutaji wao, hawana raha na maisha yao na hapa niseme kabisa naelewa Serikali ilitoa tamko kuhusu Machinga, Wilaya na mikoa walitakiwa kutenga maeneo kwa ajili ya wafanyabiashara ndogo ndogo.

Hatukatai Machinga kuwapangwa lakini swali msingi unawapanga wapi? Kwa utaratibu upi?Wanakopangwa kuna wateja? Ni muhimu tukajiuliza na kupata majibu na majibu bora sio bora majibu.

Katika siku kadhaa nimekuwa nikishuhudia namna ambavyo Machinga wa katikati ya Jiji la Dar es Salaam hasa maeneo ya Posta mpya mpaka kule Mnazi Mmoja, kwa kifupi kumekuwa na utumiaji mkubwa wa nguvu, mgambo wanatumia marungu kudhibiti wafanyabiashara.Inakera, inasikitisha.

Mgambo wa Jiji au askari wa Jiji wanawatesa sana Machinga , naposema wanawatesa naomba unielewe, maisha ya Machinga kukutana na purukushani za mgambo wa Jiji imekuwa ni jambo la kawaida.

Mgambo wanapora mali za Machinga, wanabeba nguo, wanabeba maji yaliyoko kwenye matorori.Swali wanayapeleka wapi?/Tufanye wanapeleka Jiji , sawa, wakishapeleka utaratibu wa Machinga kuchukua bidhaa zake ukoje?

Ngoja niseme kitu nimezungumza na baadhi ya Machinga wa maeneo ya Posta Mpya mpaka kule maeneo ya Kitega Uchumi, wanasema wanaishi maisha ya mateso sana, wanajua kuishi kwao kunategemea biashara hiyo hivyo wanalazimika kukaa maeneo ambayo wanajua angalau wanaweza kuuza chochote maisha yaende.

Wakati Machinga wameamua kutafuta fedha za kujikimu kimaisha kwa utaratibu unaoeleweka mgambo wa Jiji nao wanatumia nafasi hiyo kuangalia watapataje hela za Machinga.

Inasemekana Mgambo wakishachukua bidhaa za wafanyabiashara kinachofuata ni mazungumzo kati ya mporwaji(Machinga) pamoja mporaji(mgambo) na inadaiwa kwa sehemu kubwa hapo inayozungumziwa ni faini ambayo sio ya kwenda serikalini bali kuingia mifukoni mwa watu.

Machinga wanasema hela ambayo inachukulia na hao Mgambo wa Jiji la Dar es Salaam ni bora ingekuwa inaingia katika mfuko wa Serikali ili itumike kuleta maendeleo ya Watanzania.

Lakini fedha inakwenda kwenye mifuko ya watu.Hili ni tatizo na lazima Serikali ifuatilie na kuangalia namna ya kudhibiti haswa namna ya kushughulika na Machinga lakini fedha za faini zinapotakiwa kwenda.

Machinga wamekuwa na malalamiko sana kwa yanayoendelea kati yao na Mgambo, hakika Serikali yangu sikivu iko haja ya kutupia jicho kwenye hili, kwa ngazi ya Wilaya na Mkoa ni kama wameshindwa kutafuta ufumbuzi.

Ndio maana haiwezekani kila uchwao Machinga na Mgambo ni mwendo wa mapambano tu.Kuna wakati unaangalia yanayofanywa na Mgambo halafu najiuliza kweli hii ni nchi yetu nzuri ya Tanzania inayoongozwa na Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan.

Mama msikivu, mama mnyenyekevu, mama mwenye huruma na kujali, Mama mwenye anayetambua namna ya kutuongoza kwa amani, upendo na mshikamano.Na kwenye hili naomba nitoe msimamo wangu mimi na Mama Samia tu, ndio Rais wangu, ndio chaguo langu.

Nampenda sana na yanayoendelea kati ya Mgambo na Machinga hayanigombanishi na mama .Ninachojua haya yanatokea kwasababu wapo walioaminiwa wameshindwa kutimiza wajibu, wameshindwa kutafuta njia nzuri ya kuwapanga Machinga, akili imebaki kuwaza kutumia virungu kudhibiti Machinga.

Hivi tujiulize ni kweli virungu vya mgambo ndio vitaleta ufumbuzi? Hivi ni kweli rushwa ndio suluhu?Hapana jamani, wenzetu wa Jiji badilikeni, tafuteni suluhu yenye maridhiano badala ya malumbano yanayoendelea.

Rais wangu Samia Suluhu Hassan kauli mbiu ya Serikali yake inasema Kazi iendelee, kwa lugha nyepesi mama anahimiza tufanye kazi.Lakini akaenda zaidi yapo katika kuiweka nchi sawa na kuirudisha kwenye mstari akatangaza umuhimu wa kutumia Maridhiano, niwaombe Jiji la Dar es Salaam tumieni maridhiano kwenye hili la Machinga.

Hata hivyo wakati naandika maelezo yangu haya marefu niseme tu nafahamu aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Albert Chalamila amehamishiwa Dar es Salaam, sina shaka na uwezo wake wa kufanya kazi, sina shaka na uwezo wake wa kutatua changamoto zinazowakabili wananchi anawaongoza, hivyo hata hii ya Machinga iko ndani ya uwezo wake.

Mkuu wa Mkoa Chalamila karibu Dar es Salaam, karibu Jiji lenye watu milioni sita kwa mujibu wa sensa ya Watu na Makazi, Chalamila najua umekuja Dar es Salaam lakini unafahamu asilimia kubwa ya wananchi utakawaongoza ni wachakarikaji, hawana mashamba wanategemea biashara na ndio hao Machinga, angalia namna ya kuwasaidia, angalia namna ya kuwatete, .

Ni kawaida kusikia Machinga amebeba Kispika akitangaza kuuza Sumu ya Panya na hiyo ndio biashara inayomuweka mjini na watoto wanasoma na akiamua kujirusha pia utamkuta Kitambaa cheupe, wapende Machinga nao wakupende.

Hata hivyo niseme kabisa bila kupepesa macho, tumesikia mgomo wa wafanyabiashara wa Kariakoo na hatua ambazo Serikali ya Rais wangu Samia inachukua, hakika tumekuwa na serikali sikivu sana.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameamua kufanya kikao na wafanyabiashara na imani yangu kila kitu kitakwenda sawa sawa, tunakuamini sana Waziri Mkuu, tunakuamini wewe na Serikali yako chini ya mikono salama ya uongozi wa Rais Samia pamoja na Makamu wake wa Rais Dk.Philip Mpango.

Hivyo Waziri Mkuu kwa unyenyekevu mkubwa nikuombe ukimaliza ya Wafanyabiashara wa Kariakoo njoo uone yanayoendelea katikati ya Jiji la Dar es Salaam kati ya Mgambo na Machinga na kwa sehemu kubwa Machinga wamekuwa wanyonge.

Naomba nimalize kwa kueleza hivi baada ya serikali kuamua kuhamia Dodoma , Dar es Salaam sasa imebaki kuwa kitovu cha biashara, niiombe Serikali wapeni uhuru Machinga kufanya biashara .

Ingawa nikiri mimi si muumini wa Machinga wanaopanga bidhaa kando kando ya Barabara, hawa kwa kweli siko upande wao, lakini wale ambao wanatembeza mkononi ndio haswa ninaowazungumzia.Hivi kweli Mama aliyebeba beseni la ndizi ni kero kwa Jiji la Dar es Salaam, washikeni mkono wasonge mbele.

Kwa leo inatosha na nitumie nafasi kuomba msamaha kwa yoyote ambaye atakwazika kwa hiki nilichoandika, najua siwezi kuwa nimemfurahisha kila mtu lakini pia siwezi kuwa nimemuudhi kila mtu.Lakini niseme tu sio mgambo wote wanaotesa Machinga , ni baadhi na wanajijua.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...