Na Mwandishi Wetu
WAKALA wa Elimu Nje ya Nchi, Global Education Link (GEL), umesema idadi ya wanafunzi wanaokwenda kusoma nje ya nchi inazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka na kwamba kwa mwaka huu pekee wanatarajia kusafirisha wanafunzi 700.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa GEL, Abdumalik Mollel, wakati akizungumza na wanafunzi wanaotarajiwa kwenda kwenye nchi mbalimbali duniani kwa mwaka huu wa masomo.

Alitaja moja ya sababu kamba ni uhakika kwa mwanafunzi kupata nafasi kwenye aina ya kozi anayotaka kuisomea kwani kwenye vyuo vikuu vya ndani ushindani umekuwa mkubwa na nafasi zimekuwa za kushindania.

Alitoa mfano kuwa ushindani umekuwa mkubwa kwenye masomo ya sayansi kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi wanaofaulu kwenda vyuo vikuu hali ambayo inasababisha wengi kukosa na kuamua kutatafuta vyuo nje ya nchi.

Alisema wanafunzi wengi wa udaktari, ufamasia, uhandisi, udaktari wa meno wamekuwa wakiamua kwenda vyuo vya nje ya nchi kutokana na uhaba wa nafasi kwenye vyuo vya ndani.

“Kikubwa kinachowavutia wanafunzi ni uhakika wa nafasi kwasababu vyuo vikuu vya nje vinafungua udahili mapema sana na ingawa matokeo yao hayajatoka lakini wanaweza kumwekea nafasi kwasababu kule ushindani siyo mkubwa sana,” alisema

Mollel alisema kingine kinachowavutia wazazi kuwapeleka watoto wao kwenye vyuo vya nje ni gharama nafuu wanayopewa katika nchi kama Cyprus, India uturuki na Malaysia ambako wanakuwa na uhakika wa kulipa ada.

“Kwenye nchi nyingi hata za Ulaya ada mara nyingi inakuwa kati ya Dola 2,500 ambayo ni wastani wa kama shilingi milioni tano za hapa kwetu na ukiangalia vyuo vingi vya nje hawana shida ya vifaa vya kufundishia na hata uwiano wa darasa kwa mwalimu ni mzuri sana,” alisema Mollel.

Kadhalika, Mollel aliwataka wanafunzi wanaokwenda kusoma nje ya nchi kujiepusha na vitendo vya anasa na starehe kwani wanaweza kurejeshwa nchini kutokana na kukosa nidhamu.

Alisema baadhi ya wanafunzi wanapofika nje ya nchi wamekuwa wakiendekeza starehe na anasa na kusahau kazi iliyowapeleka nchini humo na wengine kushindwa kumaliza masomo yao na kutimiza ndoto zao.

“Baadhi wamekuwa hata hawahudhurii masomo na kuendekeza starehe na vyuo vina vigezo vyao ambavyo mwanafunzi asipovitimiza wanamkatalia kufanya mtihani, ukirudia mitihani ukafeli wanakufuta na kisha kuiarifu Idara ya Uhamiaji wakurejeshe nchini kwako,” alisema Mollel

Alitoa mfano kuwa kuna baadhi ya nchi ambazo haziruhusu mwanafunzi kufanyakazi lakini baadhi yao wamekuwa wakifanyakazi kwa ujanja ujanja na wanapobainika hurejeshwa nchini na hivyo kuwatia hasara wazazi wao waliowalipia ada.

Alisema wanafunzi wanapaswa kuzingatia masomo badala na kuhangaika na kazi za kujiingizia kipato kwani walikwenda kwenye mataifa hayo kwaajili ya kusoma na siyo kufanyakazi.

Mollel alisema zipo nchi ambazo zinaruhusu wanafunzi kufanyakazi lakini uzoefu unaonyesha kwamba wanapopata fursa ya kufanya kazi hutumia muda mwingi zaidi na wakati mwingine kutelekeza masomo yao na kushindwa kufikia ndoto zao.

“Siyo kila mwanafunzi anayekwenda kusoma nje ya nchi anatimiza ndoto zake kuna wengine wanaishia katikati kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutohudhuria masomo kwa hiyo mnapokwenda kwaajili ya masomo mnapaswa kuzingatia masomo na si vinginevyo,” alisema Mollel

Aidha, Mollel alitoa mfano wa mwanafunzi mmoja wa udaktari ambaye alifukuzwa mwaka wanne nchini China kutokana na kujihusisha na shughuli za ujasiriamali nchini humo wakati kibali chake hakikuwa kinamruhusu kufanya kazi.

Alisema mwanafunzi huyo alikuwa akifanya kazi hizo kwa kificho wakati wa mlipuko wa COVID lakini watu wa uhamiaji walipombaini walimfukuza na kumpiga marufuku kurejea nchini humo hivyo kupoteza fursa yake ya masomo na kuwatia hasara wazazi wake.

“Sasa ukaingalia fedha alizokuwa amekusanya kwa kufanyakazi na ukiangalia hasara ambayo wazazi wake wameingia kumsomesha miaka yote minne haviendani. Wanafunzi wengine wanakwenda kule na kuanza kujihusisha na maisha ya anasa kwa kwenda klabu za usiku,”

“Unakuta mwanafunzi kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa yuko klabu anatumia fedha zote halafu anaanza kusumbua wazazi kwamba fedha zimeisha kwa hiyo wazazi pia wanapaswa kufuatilia nyenendo za watoto hata kwenye matumizi kwasababu wakati mwingine wanawadanganya,” alisema


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...