Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Geita
UWEPO wa kambi ya kudumu ya watumishi wa Wakala wa Huduma za Misitu TFS) kwenye hifadhi ya msitu wa Rwamgasa katika eneo la Nyarugusu mkoani Geita umesaidia kupunguza uharibifu wa hifadhi hiyo kutokana na kuimarishwa kwa ulinzi muda wote.
Akizungumza na waandishi wa habari Msimamizi wa Hifadhi ya Msitu wa Rwamgasa mkoani Geita Almas Khamis Mggalu amesema tangu Serikali kupitia TFS kujenga kambi hiyo kwa ajili ya watumishi hata uoto wa asili uliokuwa umeharibiwa umeanza kurejea na hiyo inatokana na kuimarishwa kwa ulinzi.
“Kambi hii ambayo imejengwa ndani ya msitu wa Rwamgasa umesaidia kupungua umbali wa zaidi ya kilometa 70 kutoka Geita Mjini hadi hapa katika kambi yetu, umbali huo ulikuwa kikwazo kwani hata ukipata taarifa za uwepo wa halifu wa rasilimali za misitu hadi ufike unakuta wameshaondoka,”amesema.
Amesisitiza baada ya kuwepo kwa kambi ya kudumu wanakaa sehemu moja, hivyo ulinzi umeimarika tofauti na hapo awali kabla ya kujengwa kwa kambi hiyo huku akieleza katika Mkoa wa Geita uharibifu wa mazingiara ni mkubwa kutokana na shughuli za kibinadamu.
“Hali ya uhifadhi Geita ina changamoto kubwa kwasababu karibia asilimia 50 ya maeneo ya uhifadhi yamevamiwa na shughuli za kibanadamu , sehemu nyingine hata miti imeisha kabisa, kwa hiyo kwa ujumla uharibifu ni mkubwa ndio maana TFS tunapambana kuurejesha,”amesema
Kuhusu jitihada zinazofanywa na Serikali kupitia TFS katika kuhakikisha Geita inakuwa ya kijani, amesema kumekuwepo na jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanyika na miongoni mwa jitihada hizo ni kuwa na kitalu cha miti Usindakwe ambapo kuna miti mingine inatumika kwenda kurejesha uoto wa asili na mingine inapandwa maeneo ya wazi ili kupunguza presha kwenye maeneo ya uhifadhi.
“Jitihada nyingine ambazo TFS tunaendelea nazo ni kufanya doria kila siku lakini tumekuwa tukitoa elimu kwa umma kutambua umuhimu wa kutunza mazingira na rasilimali zitokanazo na misitu.
“Pia tunawaelemisha wananchi vitu vinavyoweza kuwekezwa ndani ya misitu ya hifadhi kama vile kuweka kampu a utalii na mtu akiwekeza hawezi kufikiria tena kempu ambazo wananchi wanaweza kwenda kupumzika.
“Kwa hiyo tunajitahidi kutoa elimu kupitia majukwaa mbalimbali yakiwemo ya makongamano na maonesho yanayofanyika ndani ya mkoa huu.Tumekuwa tukitoa elimu kuhusiana na fursa mbalimbali ambazo ziko ndani ya hifadhi pamoja na utunzaji wa mazingira anaofaa kwa maslahi ya walio wengi,”amesema Mggalu.
Jengo lililojengwa na Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania( TFS) kwa ajili ya kambi ya kudumu ya watumishi wa Wakala huo kwa ajili ya kulinda hifadhi ya Msitu ya Rwamgasa mkoani Geita
Msimamizi wa Hifadhi ya Msitu Rwamgasa Almas Khamis Mggalu akifafanua jambo kuhusu uwepo wa kambi hiyo na faida zake
Sehemu ya miti iliyopo ndani ya hifadhi ya Msitu Rwamgasa kama inavyooonekana baada ya kuimarishwa kwa ulinzi ndani ya hifadhi hiyo
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...