Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila hadi sasa imetoa huduma ya kupunguza uzito kwa watu 128 wenye uzito uliopitiliza kwa kutumia puto maalum (intragastic balloon) , ambapo huduma hiyo pamoja na kupunguza uzito imekuwa na mafanikio makubwa ikiwemo kuwawezesha wateja hao kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi tofauti na ilivyokuwa awali. 

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkuu wa Idara ya Upasuaji MNH-Mloganzila Dkt. Erick Muhumba na kubainisha kuwa kati ya watu hao 128 waliofanyiwa huduma hiyo wanawake wanne (4) wamefanikiwa kupata ujauzito ambapo mmoja wao alikaa zaidi ya miaka sita bila kupata ujauzito kutokana na tatizo la uzito uliopitiliza.

Dkt. Muhumba ameongeza kuwa zaidi ya watu 12 wameondolewa puto hilo kutokana na uzito wao kupungua na wachache wameondolewa kutokana na maudhi madogo madogo waliyoyapata kutokana na kuwekewa puto hilo hivyo kupelekea kuliondoa.

“Wapo baadhi ya wateja wetu takribani wanne tuliwawekea puto lakini tumelazimika kuliondoa kutokana na maudhi madogo madogo ikiwemo kutapika, lakini wengi wao huduma hii imekuwa rafiki na yenye mafanikio makubwa na wapo ambao wametoa baada ya uzito kupungua” amesema Dkt. Muhumba

Dkt. Muhumba amefafanua kuwa wapo ambao wameongeza maji au kupunguza maji kwenye puto kulingana na mahitaji ya wateja, ametoa mfano kuwa miongoni mwa  waliongezewa maji kwenye puto kwa lengo la kuendelea kupunguza uzito ni msanii na balozi wa puto Mloganzila Bw. Peter Msechu.

Kwa upande wake msanii na balozi wa puto Bw. Peter Msechu amesema kwa kipindi cha miezi sita amepunguza takribani kilo 17 kutoka 144 alizokuwa nazo awali na ameona umuhimu wa kuongeza maji kwenye puto kutokana na kuwa na kasi ndogo ya uzito kupungua.

Msechu ameongeza kuwa tangu awekewe puto ameweza kufanya majukumu yake kwa muda mrefu bila kuchoka, pia amebainisha kuwa uzito wake haujapungua kwa kasi kama alivyotarajia kutokana na kutofanya mazoezi kama alivyoshauriwa na wataalamu hali iliyotokana na ratiba yake kusongwa na majukumu mengi ya kitaifa.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...