Mtandao wa kidijitali waunganisha Benki ya CDRB na Airtel Money kurahisisha malipo ya ada za shule


Malipo ya ada za shule sasa kuwa kiganjani

IKIWA ni moja ya juhudi zinazoendelea katika ubunifu wa masuluhisho yenye kuongeza thamani kwa wateja wao, Airtel Tanzania na Benki ya CRDB jijini Dar es Salaam leo kwa pamoja wamezindua huduma nyingine ya aina yake yenye lengo la kurahisisha malipo kwa wateja wote wa Airtel na CRDB.

Kwa kupitia ushirikiano huo na Benki ya CRDB, wateja sasa wanaweza kulipa ada za shule moja kwa moja kutoka Airtel Money kwenda kwenye shule wanazotaka kulipa ada. Huduma hii inapatikana kwa shule zote zenye akaunti katika Benki ya CRDB ambapo wazazi hupewa namba maalumu ya udhibiti (Control Number) itakayomwezesha kulipa ada za shule akiwa popote.

Airtel Money na Benki ya CRDB zimeshakamilisha kuunganisha miundombinu ya benki ya CRDB na mtandao wa Airtel Money ili kuwawezesha wazazi kulipa ada za shule kupitia namba za udhibiti zinazotolewa shuleni.

Wazazi na walezi sasa wanaweza kulipa ada za shule kwa urahisi popote walipo, wakati wowote bila kupoteza muda kwa kukaa kwenye foleni ndefu benki.

Akizungumza wakati wa uzinduzi jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa Airtel Money, Andrew Rugamba alisema, “kwa kutumia Airtel Money, wazazi na walezi sasa wanaweza kulipa ada za shule za watoto wao kwa urahisi, malipo yanaweza kuwa kamili ama sehemu yake kama mzazi atakavyoamua, leo zaidi ya shule 150 zinatumia mfumo huu wa kisasa wa malipo ya ada kuanzia shule za msingi, sekondari na taasisi za elimu ya juu, wazazi wote wanahitajika kuomba hizi namba za udhibiti (control number) za kulipia ada za watoto wao kutoka shuleni na kuzitumia wakati wanapotaka kulipia ada za shule kwa kipindi cha mwaka mzima au kwa utaratibu watakaojipangia wakiwa popote.

“Airtel na CRDB kupitia huduma hii ya malipo ya ada za shule kidijitali tunaendelea kudhihirisha dhamira yetu ya kutoa huduma za kisasa kwa wateja huku tukienda sambamba na ajenda ya kitaifa ya kufikia lengo la kidunia kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia watanzania wengi zaidi”, alisema Bwana Rugamba.

Akaongeza kuwa ili kulipia ada ya shule, mteja wa Airtel anahitajika kupiga *150*60# kisha anachagua 5, lipa pili kisha 7, lipa ada ikifuata na Benki ya CRDB kisha anaweka control number ya shule, ikifuata kiasi na kuidhinisha malipo.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya CRDB Stephen Adili alisema, “Sisi kama CRDB benki inayomsikiliza mteja, tumeona kuna haja ya kuungana na Airtel, moja ya kampuni kubwa ya simu nchini kuleta suluhisho la aina yake katika njanya ya malipo ya kidigitali kwa watanzania.

“Leo kulipa ada ya shule kwa kupitia namba maalumu ya udhibiti ya benki yetu, itawasaidia wateja wote wa Airtel na CRDB kuokoa muda na kuwa mahali salama na rahisi wakati wakilipa ada za shule.

“Ni matumaini yetu ushirikiano huu utasaidia juhudi za Serikali ya awamu ya sita katika ajenda yake ya uchumi jumuishi wa kidigitali katika kuhakikisha huduma za kifedha zinakuwa rahisi na kuwafikia watu wengi zaidi”, aliongeza Bwana Adili.
Mkurugenzi wa Airtel Money, Andrew Rugamba (wa tatu kushoto), Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya CRDB, Stephen Adili (wanne kushoto) pamoja na baadhi ya maofisa wa Airtel na CRDB wakishangilia muda mfupi baada ya kuzindua huduma ya malipo ya ada za shule kwa kupitia huduma ya Airtel Money, inayopatikana kwa ushirikiano wa Airel na CRDB. Hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam leo.
Mkurugenzi wa Airtel Money, Andrew Rugamba (katikati), akizungunza wakati wa uzinduzi wa huduma ya malipo ya ada za shule kwa kupitia huduma ya Airtel Money, inayowezeshwa kwa ushirikiano wa Airtel na CRDB. Hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam leo. Kushoto ni Meneja Mahusiano wa Airtel, Jackson Mmbando na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya CRDB, Stephen Adili. 
Meneja Mahusiano wa Kampuni ya Simu za Mkononi ya Airtel Tanzania, Jackson Mmbando (kushoto), akitoa ufafanuzi kuhusu huduma ya malipo ya ada za shule kwa kupitia huduma ya Airtel Money inayowezeshwa kwa ushirikiano kati ya Airtel na Benki ya CRDB, katika hafla ya uzinduzi wake jijini Dar es Salaam leo. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Airtel Money, Andrew Rugamba, Mkurugenzi wa Wateja Binafsi wa CRDB, Stephen Adili na Meneja Mwandamizi Huduma Mbadala wa CRDB, Mangire Kibanda.
Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya CRDB, Stephen Adili (kulia), akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma ya malipo ya ada za shule kwa kupitia huduma ya Airtel Money, inayopatikana kwa ushirikiano wa Airel na CRDB. Hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam leo. Kushoto ni Meneja Mahusiano wa Airtel, Jackson Mmbando na Mkurugenzi wa Airtel Money, Andrew Rugamba.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...