Njombe
Mkuu wa wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa ameagiza maafisa wa mamlaka ya uhifadhi wanyamapori Tanzania (TAWA) kanda ya Iringa pamoja na Taasisi nyingine zinazohusika na wanyamapori wanaowatafuta Simba waliovamia katika mji wa Makambako na kujeruhi pamoja na kuua mifugo kuhakikisha wanawatafuta na kuwapata wakiwa hai au wamekufa.
DC Kissa amebainisha hayo wakati akitoa salamu za serikali kwenye kikao cha baraza la madiwani robo ya nne na kufunga mwaka 2022-2023 cha halmashauri hiyo ambapo pia ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari huku pia akiwaomba wananchi kuwasha moto karibu na mabanda ya mifugo kwa kuwa Simba wamekuwa wakiogopa moto.
"Nimepata taarifa kuwa nguvu kutoka TAWA imeongezwa na wanafanya kila jitihada kuhakikisha hao wanyama (Simba) wanakamatwa,ombi langu kwa wananchi ni kuchukua tahadhari na niawatoe hofu kwamba serikali jambo hili tunalishughulikia na nimeshatoa maagizo kwamba Simba apatikane akiwa hai au akiwa amekufa"amesema DC Kissa
Awali madiwani wa halmashauri hiyo akiwemo Navy Sanga,Salum Mlumbe pamoja Hanana Mfikwa wamesema kuwa wananchi wamekuwa na taharuki kubwa na kupelekea kushindwa kwenda kwenye shughuli zao huku pia madiwani wengine wakiomba wananchi jamii ya Mang'ati watumiwe kwa kuwa wana utaalamu wa kuua Simba.
Afisa Maliasili na uhifadhi mazingira halmashauri ya mji wa Makambako Gift Kiwia amesema kuwa Simba wawili ndio wanaosadikika kuwepo katika halmashauri ya mji wa Makambako kutoka siku ya tarhe 29 wakitokea hifadhi ya taifa ya Ruaha ambapo waliingia kupitia kijiji cha Malombwe na kuua Ng'ombe wawili na Nguruwe mmoja na siku ya kuamkia leo katika kijiji cha Mkolangu wakiua tena Ng'ombe mmoja na Nguruwe wawili.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...