NA Mwandishi Wetu
KATIKA kutimiza dhamira ya kuimarisha sekta ya elimu na kuwezesha mazingira ya utoaji elimu nchini kuwa ya usawa, Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imetoa msaada wa madawati 8,823 kwa shule za Geita ili kuweka mazingira mazuri ya kujifunzia kwa wanafunzi wa mkoa huo.
Katika hafla ya makabidhiano hayo iliyofanyika juzi Mjini Geita kwa ushirikiano na mamlaka za serikali za mitaa kupitia mpango wa GGML wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella, aliishukuru kampuni hiyo kwa kuwa msaada huo umekuja wakati muafaka.
Amesema kadiri shule nyingi zinavyoendelea kujengwa ndivyo hitaji la madawati linavyozidi kuonekana jambo ambalo GGML inajitahidi kutatua changamoto hiyo.
Shigella alipongeza GGML kwa kuwa na mipango ya muda mrefu ya kuinua sekta ya elimu mkoani Geita na Tanzania nzima kwa ujumla.
"Ni furaha yangu kwamba tangu GGML ianze shughuli za uchimbaji hapa mkoani Geita, imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Serikali kutekeleza miradi kadhaa ya elimu, hasa ujenzi wa madarasa na shule".
Aidha alikiri kuwepo kwa uhaba wa madawati katika shule, hivyo kuwaomba wadau wengine mkoani humo kufuata nyayo za GGML katika kuboresha mazingira ya kujisomea kwa wanafunzi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Terry Strong, amesema ni muhimu kuboresha mazingira ya utoaji elimu nchini ili kufikia lengo namba 4 la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa.
"Kutoa elimu bora kwa wote ni msingi wa kujenga dunia yenye amani na ustawi. Elimu huwapa watu maarifa na ujuzi wanaohitaji ili kuwa na afya njema, kupata ajira. GGML inafurahi kuboresha maisha ya Watanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu," amesema.
Akielezea malengo ya GGML katika kuboresha maisha ya Watanzania hususani kupitia uboreshaji wa sekta ya elimu, Strong alieleza kuwa tangu kuanzishwa kwa kampuni hiyo mwaka wa 2000, GGML imeendelea kuwekeza katika nyanja mbalimbali zinazoboresha maisha ya jamii nzima ya Geita na Tanzania kwa ujumla.
Ameongeza GGML imewekeza kwa kuzingatia masuala muhimu kama vile afya, elimu, maji, barabara na miradi ya kuzalisha kipato cha kaya na kukuza uchumi wa Taifa.
"GGML imewekeza katika utekelezaji wa miradi endelevu ambayo inainufaisha jamii inayouzunguka mgodi. Kwa hiyo mchango huu wa madawati unadhihirisha jukumu la GGML kama mwananchi anayehitaji elimu bora kubadilisha maisha yake," amefafanua.
Ameongeza juhudi za GGML kujitolea kutekeleza miradi zinaendelea kuacha alama isiyofutika na kusaidia kuboresha maisha ya jamii kupitia uwepo wa kampuni hiyo mkoani Geita.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...