*Taarifa za mapato na matumizi bado haziwekwi wazi, wazazi hawajitokezi katika miradi ya uboreshaji elimu
KATIKA Kuboresha upatikanaji wa elimu nchini jamii imetakiwa kuchangia chakula ili wanafunzi waweze kushiriki vyema katika masomo na kukidhi mahitaji ya elimu nchini.
Hayo yameeelezwa leo jijini Dar es Salaam na Meneja miradi wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET,) Martha Makala wakati wa utoaji wa matokeo ya mradi ulioangazia 'Ukosefu wa uwazi na Uwajibikaji katika Kuendesha Shughuli za Elimu katika shule za Umma,ngazi ya Kijiji na kueleza kuwa ni wajibu wa jamii kushiriki katika uboreshaji na upatikanaji bora wa elimu Tanzania.
"Serikali ina nafasi na jamii lazima iangalie namna inavyoweza kuchangia katika kuboresha upatikanaji wa elimu bora nchini ikiwemo kuchangia chakula ili wanafunzi washiriki vyema katika masomo na kuongeza ufaulu...Hii pia itasaidia kupunguza vishawishi vinavyopelekea mimba za utotoni kwa baadhi ya wanafunzi kupokea fedha kwa ajili ya chakula." Amesema.
Amesema, Jamii pia inatakiwa kushirikiana na Serikali za mitaa na asasi za kiraia katika kuhakikisha elimu inakidhi mahitaji ya Taifa kwa kuhakikisha rasilimali zinatumika kwa usahihi.
Bi. Martha amesema, mradi huo uliofadhiliwa na asasi ya Foundation for Civil Society (FCS,) umetekelezwa katika Halmashauri 10 Tanzania bara uliwalenga wadau katika ngazi ya jamii, Halmashauri za Wilaya, asasi zinazofanya kazi katika eneo husika, watunga sera na wabunge huku dhumuni kubwa likiwa ni kujenga uwezo kwa jamii kwa kuwafundisha mbinu za ufuatiliaji rasilimali zinazotolewa na Mamlaka za Serikali kwa ajili ya kuboresha elimu na utekelezaji wake pamoja na kujenga uelewa kwa kamati za shule katika kuhakikisha zinawajibika na kutekeleza majukumu yake kikamilifu.
Akizungumza juu ya matokeo ya mradi huo Mshauri wa Masuala ya Elimu na Maendeleo Japhet Makongo amesema, taarifa za makadirio ya mapato ya fedha za shule na matumizi zimekuwa hazifahamiki vyema kwa jamii na wazazi.
"Ruzuku zimekuwa zikitolewa kwa shule za msingi, lakini zinatolewa zikiwa chini ya kiwango kinachostahili cha shilingi 6,000 kwa mwanafunzi...Asasi ya TARUDECO iliyopo wilayani Kibiti, Pwani katika ripoti imeonesha kwamba katika mwaka wa fedha 2020/2021 na 2021/2022 ruzuku iliyofika shuleni ni kati ya shilingi 5,400 na 5,600 na hiyo ni pamoja na taarifa za ruzuku kutobandikwa katika mbao za matangazo za shule na kusambazwa kwa wajumbe wa kamati za shule... amesema.
Amesema, Wazazi pia hawana taarifa sahihi na hawashirikishwi katika vipaumbele vya shule ikiwa ni pamoja na mpango na mchakato mzima wa mapato na matumizi pamoja na baadhi vijiji na viongozi wa vijiji kutofuata kalenda yakuitisha mikutano ya kila mwezi ambapo taarifa kuhusu sekta ya elimu zingewakilishwa.
"Kwa mujibu wa matokeo yaliyotolewa na TARUDECO wilayani Kibiti yameonesha kuwa wazazi wanne kati ya kumi waliohojiwa walieleza kushiriki katika kuandaa bajeti ya shule, wanafunzi wawili kati ya kumi waliohojiwa walisema walishiriki katika kuandaa bajeti ya shule huku wajumbe wote kumi waliohojiwa walieleza kushiriki katika kuandaa bajeti za shule lakini hawakuwa na taarifa ya bajeti iliyopitishwa." Amesema.
Pia ameeleza kuwa imebainika kuwepo kwa mwitiko mdogo wa wazazi katika kushiriki kwenye miradi ya kuboresha elimu kama ukarabati wa miundombinu ikiwemo ujenzi wa vyoo, upatikanaji wa vyakula shuleni na posho zinazotolewa kwa walimu wanaojitolea katika mpango wa kuboresha elimu na hiyo ni sambamba na uwajibikaji hafifu wa Mamlaka za Serikali za mitaa katika shule, vijiji, Kata na Halmashauri kwa kushindwa kuchukua hatua madhubuti dhidi ya watendaji wanaohusika na matumizi mabaya ya rasilimali za Umma na walimu kutohudhuria vipindi vyao.
"Baadhi ya walimu katika shule ya msingi Nyamalela Kata ya Mlowa, wilayani Chamwino walilalamikiwa na Wanafunzi kufanya shughuli zao za biashara na kushindwa kuingia darasani kufundisha na kamati ya shule haikuchukua hatua yoyote awali na walichukua hatua baada ya kamati ya PETS kutoa taarifa na walimu wakaanza kufundisha." Amesema.
Vilevile ameeleza kuwa kamati za SAM/PETS zimebaini mazingira duni na yasiyo rafiki kwa ya kujifunzia na yanayochochea kukosekana na uwajibikaji, ikiwemo madarasa, vyoo, nyumba za walimu, viwanja na vifaa vya michezo.
"Katika shule zote kumi zilizofikiwa na mradi wa SAM/PETS kulikuwa na msongamano katika vyumba vya madarasa hususani madarasa ya awali katika vijiji vilivyopo pembezoni katika Wilaya za Kalambo, Nsimbo, Mvuha/Morogoro, Pangani, Kibiti na Nachingwea.... katika sekta ya michezo miundombinu iliyopo ni viwanja vya mpira wa miguu bila mbadala wa michezo mingine kwa wanafunzi wa kike ambao huathirika katika suala zima la michezo.....Hapa masuala mtambuka pia yameibuka ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia na mimba za utotoni kwa maeneo ya Chamwino, Kalambo, Nsimbo, Pangani na Nachingwea." Ameeleza.
Katika kuhakikisha jamii inakuwa sehemu ya kukuza sekta ya Elimu makundi mbalimbali ikiwemo walimu, wazazi na viongozi wa dini wameonesha ushiriki wao katika shughuli za kijamii.
" Viongozi wa dini katika Kata ya Chalinze, wilayani Chamwino wameitikia wito wa kupiga vita ndoa za utotoni kwa kulazimisha kuwasilisha vyeti vya kuzaliwa kabla ya kuruhusu mchakato wa kufunga ndoa pamoja na wazazi na Wanafunzi katika shule ya msingi Mizengo Pinda wamekubali kuchangia programu ya chakula shuleni." Amesema.
Mradi huo umekuja na mapendekezo kadhaa ikiwemo elimu kwa jamii juu ya ushiriki katika shughuli za SAM/PETS, Mamlaka za Serikali za mitaa kuhakikisha zinaboresha usimamizi wa fedha, kuwepo kwa mgawanyo sawa wa walimu kwa kuangazia maeneo ya pembezoni hususani vijijini, Wizara husika (TAMISEMI,) kuhakikisha kuna ongezeko sahihi la ruzuku kwa kila mwanafunzi pamoja na kusimamia ugawaji sawa wa walimu katika shule za msingi kwa uwiano unaozingatia usawa wa kijinsia, mahitaji maalumu na mpangilio wa kijiografia.
Aidha Bunge limeshauriwa kufuatilia kwa ukaribu ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG,) kuboresha ruzuku kwa kuangazia hali halisi pamoja na kupitisha bajeti sahihi na stahiki inayolenga vipaumbele vya jamii na Serikali za mitaa huku asasi za kiraia zikitakiwa kuendelea kuunga mkono kuendelezwa kamati hizo na kuimarisha ushirikiano na wadau wengine katika utekelezaji mikakati ya SAM/PETS huku vyombo vya habari vikitakiwa kuendesha majadiliano, vipindi vya mijadala na mazungumzo.
Mshauri wa masuala ya Elimu na Maendeleo Japhet Makongo (kushoto,) akizungumza wakati wa utoaji wa matokeo ya mradi huo na kueleza kuwa katika kukuza na kuendeleza sekta ya elimu ushirikiano baina ya Serikali, jamii na asasi ni muhimu katika kuleta tija katika sekta ya elimu, kulia ni Meneja Ugemaji Rasilimali Wilson Chacha.Leo jijini Dar es Salaam.
Meneja miradi wa TEN-MET, Martha Makala akizungumza wakati wa utoaji wa matokeo ya mradi ulioangazia 'Ukosefu wa Uwazi na Uwajibikaji katika Kuendesha Shughuli za Elimu katika Shule za Umma, ngazi ya Kijiji na kuhimiza jamii kushiriki katika mchakato wa uboreshaji elimu kwa kuchangia chakula shuleni. Leo jijini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...