Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Zuberi Homera (Kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mbolea ya Yara Winstone Odhiambo (Kulia kwake) wakipata maelezo kutoka kwa bwana shamba Donath Fungu siku ya ufunguzi wa mkutano wa wakulima katika maonyesho ya Yara Kilimo Expo 2023 mjini Mbeya hapo jana.

MKUU wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera ametoa wito wa kuwapa kipaumbele wakulima kwa kuwapatia mahitaji yao mapema ili kuweza kufanikisha malengo ya nchi katika kuboresha ajenda ya kilimo na kuifanya Tanzania kuwa kinara wa uzalishaji chakula barani Afrika.

Amesema, serikali inatambua kuwa wakulima ni muhimu zaidi katika kutimiza mipango yake ya nchi na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza Pato la Taifa.

Homera ameyasema hayo hivi karibuni, alipokuwa akifungua mkutano wa siku tano kwa wadau wa kilimo na maonyesho ya bidhaa na huduma(Yara Kilimo Expo) mjini Mbeya ulioandaliwa na kampuni ya kutengeneza na kusambaza mbolea ya Yara Tanzania, ambapo zaidi ya wakulima 400 kutoka nyanda za juu kusini wamehudhuria.

Jukwaa la wakulima ni sehemu ya maonesho ya kilimo ya Yara yaliyoanza Jumatatu katika viwanja vya Nanenane mjini humo kwa kuwaleta pamoja wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo ili kujadili changamoto na fursa za ajenda ya mageuzi inayochagizwa na Serikali.

Maonyesho hayo ni mahususi kwa uendelezaji wa mazao ya kimkakati ya chakula na biashara katika nyanda za juu kusini.

Akizungumza katika, mkutano Homera amesema, Yara wameonyesha ushuhuda kwa kutambua umuhimu wa wakulima na hivyo amewaasa wakulima hao kuleta hoja katika majadiliano ili waweze kusikika.

"Naipongeza Yara kwa kuthamini na kulifanya suala la kuwezesha wakulima wadogo kuwa kipaumbele katika shughuli zake..,mkutano huu leo kwa wakulima kutoka mikoa ya jirani unaonesha jinsi Yara inavyotambua umuhimu wako mkulima hivyo wamekuleta katika majadiliano ili hoja yako isikike," amesema Homera.

Aidha Homera ameishukuru Yara kwa juhudi zao za kumwinua mkulima na kuahidi kuwa serikali itaendelea kuipatia kampuni hiyo

msaada unaohitajika ili kuharakisha mageuzi kupitia bidhaa zake bora za mbolea na huduma za kilimo nchini.

Pia Waziri wa Kilimo Hussein Bashe leo Julai 26,2023 anatarajiwa kuongoza kongamano la ngazi ya juu ambapo wataalam wataangazia kwa kina zaidi mustakabali, mnyororo wa thamani wa sekta ya kilimo na masuala yanayoweza kuchagiza mwelekeo wa ajenda ya mabadiliko.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Yara Tanzania, Winstone Odhiambo amesema ni imani ya Yara kwamba, ni muhimu kuwawezesha wakulima wadogo ili nchi iweze kupata chakula cha kutosha na kuinua mamilioni ya watu kutoka katika umaskini kupitia uzalishaji wa kiwango cha juu cha kilimo na kuzalisha ajira kupitia mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.

“Kama Yara, tunatekeleza jukumu letu kwa kuhakikisha tunazalisha mbolea tofauti na zenye ubora wa hali ya juu na virutubisho vingine vya mazao vilivyochanganywa ambavyo vinaongeza mavuno na kipato cha wakulima. " Amesema

Odhiambo ameongezea kuwa, maonesho ya Kilimo ya Yara ya wiki moja, yatakuwa yakifanyika kila mwaka ili kuendeleza ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi na kuunga mkono ajenda ya Serikali ya maendeleo ya kiuchumi kupitia sekta ya kilimo ambayo ina nafasi kubwa zaidi kwa mamilioni ya 2atanzania kufanikiwa.

Amesema kuwa Kituo cha Maarifa cha Yara kilichofunguliwa hivi karibuni mjini Mbeya kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia (MUST) kitakuwa muhimu sana katika kampeni ya mageuzi ya kilimo.


Baadhi ya wakulima wakiangalia na kujifunza bidhaa mbali mbali za kilimo, zikiwemo pembejeo,  Mbolea na zinginezo wakati  maonesho ya bidhaa na huduma (Yara Kilimo Expo) yanayoendelea  Mjini Mbeya.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...