Na. Damian Kunambi, Njombe
Kufuatia uwepowa wa changamoto ya miundombinu ya barabara nne zilizopo katika maeneo mbalimbali ya kata ya Lubonde Wilayani Ludewa mkoani Njombe serikali imesema tayari imeziweka katika mpango wa ujenzi kwa mwaka ujao barabara tatu kati ya hizo ambapo kiasi cha sh. Ml. 600 kitakwenda kutatua changamoto hiyo huku barabara moja iliyosalia kwa sasa inaendelea na hatua za mikataba.
Hayo ameyasema Meneja wa Wakala wa barabara mijini na vijijini (TARURA) wilaya ya Ludewa Eng. Butene Jilala mbele ya mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga walipokuwa katika mikutano ya hadhara katika vijiji vya Masimbwe, Mkiu pamoja na Kiyombo ikiwa ni muendelezo wa ziara ya mbunge huyo ya kutembelea kijiji kwa kijiji kwa lengo la kutoa mrejesho wa aliyoagizwa na kupokea changamoto.
Baada ya wananchi wa vijiji hivyo kuwasilisha changamoto hiyo kwa nyakati tofauti mbunge Kamonga aliwaambia tayari zimesha patiwa ufumbuzi huku akimtaka Eng. Jilala kutoa mchanganuo wa fedha hizo za ujenzi wa barabara.
Eng. Jilala amesema barabara zilizoingizwa katika mpango wa mwaka kesho ni barabara ya Lutemaluche kwa kiasi cha sh. Mil 200, Mapogolo Kiyombo sh. Mil 200, Mlangali Kiyombo sh. Mil. 200 na kwa upande wa barabara ya Masimbwe Lusala aliwaomba wananchi kuwapa muda wa kushughulikana mikataba ya barabara hiyo.
Hata
hivyo mbunge Kamonga amesema serikali ya awamu ya sita iliyo chini ya
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imelenga kuleta maendeleo mbalimbali kwa
wananchi na hasa katika miundombinu ya barabara za vijijini ili
kuwezesha wananchi kukua kiuchumi kwa kusafirisha mazao yao kwa urahisi.
Mbunge
huyo ameanza ziara hiyo Julai 7 mwaka huu na bado anaendelea nayo ili
kuvifikia vijiji vyote 77 vya jimbo hilo ambapo mpaka sasa tayari
amekwisha tembelea vijiji 12 ambavyo ni Madilu, Ilawa, Ilininda, Manga,
Mfalasi, Iwela, Madope, Mangalanyene, Luvuyo, Masimbwe, Mkiu na Kiyombo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...