Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameitaka Afrika kwa pamoja kuanza safari ya kutekeleza mikakati iliyojadiliwa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Rasilimali Watu na kuwa na mtazamo wa pamoja katika kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa bara hilo na kuongeza tija ya vijana kupitia elimu bora na stadi za kazi.

Ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akihitimisha Mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere kuanzia Julai 25 na 26, 2023.

"Ni jukumu letu Waafrika kupitia kizazi hiki kupanga mstakabali wetu kwa kuhakikisha kwamba uwepo wa idadi kubwa ya vijana katika nchi zetu unakuwa na faida kwetu badala ya kuwa mzigo, kwa hakika mkutano huu umekuwa wa mafanikio kwa kuwa umetoa fursa muhimu ya kubadilishana mawazo na kupeana uzoefu juu ya namna ya kutatua changamoto na kufikia malengo yaliyokusudiwa.", amesema Rais Dkt. Mwinyi.

Ameongeza kuwa, majadiliano hayo yametoa mwanga juu ya sera na uwekezaji unaotakiwa ili kutumia ipasavyo uwezo na idadi kubwa ya vijana ambao bara la Afrika inao. Aidha, imekuwa kipimo tosha juu ya utayari wa Afrika kuwekeza katika elimu na mafunzo ya stadi za kazi ambavyo vinaweza kuongeza ajira na kuboresha tija kwa Afrika.

Aidha, amewashukuru Wakuu wa Nchi, Makamu wa Rais, Mawaziri Wakuu, Mawaziri na wajumbe wengine kwa kushiriki katika mkutano huo pamoja na michango yao yenye tija waliyoitoa ambayo imefanikisha mkutano huo na kusema kuwa mafanikio ya mkutano huo ni deni ambalo Tanzania inaweza kulilipa kwa kutimiza ahadi zilizotolewa wakati wa mkutano.

"Tunaahidi kuendeleza Azimio la Dar es Salaam kuhusu mtaji wa rasilimali watu katika bara la Afrika na nje ya bara hili, tunaishukuru Benki ya Dunia kwa ushirikiano wao, ni imani yetu kwamba Benki hii itaendeleza dhamira yake katika utekelezaji wa ahadi zilizotolewa kupitia Azimio hilo juu ya mtaji wa rasilimali watu", amesema Rais Dkt. Mwinyi.

Katika mkutano huo, nchi zimebadilishana uzoefu wa njia na mbinu mbalimbali za kuharakisha kufikiwa kwa ufumbuzi wa kukabiliana na changamoto ya rasilimali watu katika nchi za Afrika. Pia wamepata fursa ya kujadiliana kwa kina juu ya mikakati muhimu ya kufikiwa kwa elimu bora na afya kama nguzo muhimu kwa ukuaji wa uchumi na maendeleo ya jamii.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...