Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Mhandisi Profesa Zacharia Mganilwa, akimkabidhi zawadi Katibu Tawala wa Wilaya ya Singida, Goodluck Mwangomango kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa kozi ya Maafisa Usafirishaji na Madereva Wakuu wa Taasisi za Umma na Halmashauri zote hapa nchini uliofanyika Julai 26, 2023 katika Ukumbi wa RC Misheni mjini hapa. Kulia ni Mkuu wa Kituo cha Mafunzo Endelevu cha NIT, Bahati Mabina.
Na Dotto Mwaibale, Singida
MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba ametoa wito kwa Uongozi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kuendelea kuwa wabunifu na kufanya kazi kwa weledi mkubwa ili kukifanya chuo hicho kuwa mahali sahihi pa kupatia mafunzo stahiki.
Wito huo umetolewa na Serukamba kwa niaba yake na Katibu Tawala Wilaya ya Singida, Goodluck Mwangomango wakati akizindua kozi ya Maafisa Usafirishaji na Madereva Wakuu wa Taasisi za Umma na Halmashauri zote hapa nchini uliofanyika Julai 26, 2023 katika Ukumbi wa RC Misheni mjini hapa.
“Nimeisikia hotuba ya Mkuu wa Chuo, Profesa Zacharia Mganilwa kuhusu umuhimu wa mafunzo haya kwenu binafsi na serikali yetu inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan naamini baada ya mafunzo haya mtakuwa mabalozi wazuri wa chuo chetu hiki kwenye utoaji wa mafunzo mbalimbali ya operesheni za usafirishaji pamoja na Taasisi zenu mnazofanyia kazi,”alisema Mwangomango.
Alisema kuwepo kwa mafunzo hayo ni matokeo ya juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia waliowezesha kuwepo kwa Mradi huo wa East Africa Skills for Transformation and Regional Integration Project unaofadhiliwa na Benki ya Dunia ambao ni mkopo wa Serikali.
‘Chuo cha Taifa cha Usafirishaji kimepewa jukumu kubwa la kuwaandaa wataalamu waliobobea katika nyanja tano za Usafirishaji. Lakini leo nimejikita kwenye usafiri wa barabarani ambapo mmekuwa mkituzalishia maafisa usafirishaji na madereva wenye weledi mkubwa. Ombi langu kwa chuo ni kuhakikisha kinatoa mafunzo haya mara kwa mara ili wataalamu hawa waendane na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia," alisema Mwangomango.
Alisema ubunifu si jambo la kufumbia macho hata kidogo hasa katika ukuaji huu mkubwa wa teknolojia ambapo aliwaomba washiriki wa mafunzo hayo kuwa wabunifu na kusoma kwa bidii ili watakapomaliza waweze kuongeza tija katika vituo vyao vya kazi.
Mwangomango alitumia nafasi hiyo kuupongeza uongozi wa chuo, wanataaluma na wafanyakazi wote kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuhakikisha kuwa mafunzo hayo yanafanyika katika Mkoa wa Singida kwa kanda ya kati na kueleza kuwa wangeweza kuamua yakafanyike mikoa mingine.
Awali akizungumza wakati akimkaribisha mgeni rasmi kuzindua mafunzo hayo, Mkuu wa chuo hicho, Mhandisi Profesa Zacharia Mganilwa alianza kwa kutoa historia fupi ya chuo hicho kuwa kilianzishwa mwaka 1975 ili kuwaandaa wataalamu watakaoziba pengo lilosababishwa na kuondoka kwa Wataalamu na kisha kuunda Makampuni ya Usafiri Dar es Salaam (UDA), Kamata,Usafiri wa mabasi ya mikoani, Uchukuzi wa Mizingo , Usafiri wa Maji mwambao wa Pwani (TACOSHILI ) na kuwa makampuni hayo yalianzishwa na Shirika la Taifa la Uchukuzi (NTC) kwa niaba ya Serikali ili kuziba pengo la Wataalam wa Usafirishaji nchini.
Alisema chuo hicho kwa sasa kipo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na kinaendesha Mradi wa Kikanda wa East AfricaSkills for Transformation and Regional Integration Project (EASTRIP) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia na kueleza kuwa mradi huo unatekelezwa katika nchi tatu yaani Tanzania, Kenya na Ethiopia ili kuwezesha muingiliano wa kijamii katika nchi za ukanda wa Afrika.
Alisema ndani ya nchi hizo kuna vituo vya umahiri 16 ambapo kwa hapa nchini kinaitwa Kituo cha Umahiri cha Usafiri wa Anga na Operesheni za Usafirishaji.
Alisema kituo hicho kwa upande mmoja kimelenga kufundisha wataalam wa usafiri wa Anga Marubani, wahandisi wa Ndege, Wahudumu ndani ya Ndege ambapo kwa upande wa wataalam wa usafirishaji walengwa ni wataalam wa usafiri wa njia ya reli,maji na kwa kozi hiyo walengwa ni wataalam wa njia ya barabara.
Alisema katika kufikia malengo ya mradi, chuo kinajukumu la kuandaa mitaala inayokidhi matakwa ya soko la Ajira, kuongeza ushirikiano na Taasisi nyingine za ndani na nje ya nchi kwa kuwa na mikataba ya ushirikiano, Kuboresha Miundombinu ya kufundishia na kujifunzia, kuzifikia Taasisi zingine ambazo ziko nje ya Mradi na kutoa mafunzo.
Alisema katika kulifikia lengo namba nne la utekelezaji wa mradi huo , chuo kimeandaa mafunzo ya siku tano kwa ajili ya Maafisa Usafirishaji na Madereva Wakuu kwa lengo la kuwajengea, Ujuzi wa Usimamizi,Uendeshaji na Matengenezo ya Magari.
Aidha, Mganilwa alisema mafunzo hayo yatafanyika katika Kanda mbalimbali Tanzania Bara na Visiwani kuanzia Julai 10, 2023 hadi Januari 26,
2024.
Alizitaja Kanda saba ambazo yatafanyika mafunzo hayo kuwa ni Kanda ya Mashariki, Kanda ya Kati, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Kusini, na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Zanzibar na kuwa mshiriki kutoka serikalini alipaswa kuchangia ada ya kiasi cha Sh.500,000 hata hivyo gharama hizo za ada atalipiwa kupitia fedha za mradi ambapo washiriki wanaotoka sekta binafsi chuo kilipunguza ada kutoka Sh. 500,000 mpaka Sh.250,000 ili kuhakikisha wataalamu hao wanapata ujuzi unaotakiwa.
Profesa Mganilwa alisema kozi hiyo ya muda mfupi itawaongezea umahiri katika kutumia ipasavyo vipuli vya magari na vilainishi, kufanya ukaguzi wa magari, kuhakikisha matumizi sahihi ya mafuta, kuratibu matumizi sahihi ya matairi na kuboresha uendeshaji wa magari kwa ujumla na kuwa matumaini yake washiriki hao watakua mabalozi wazuri wa mafunzo hayo kwa kuzingatia kuwa wamebahatika kuwa kanda ya pili kati ya kanda nane za Tanzania.
Kwa upande wake Mkuu wa Kituo cha Mafunzo Endelevu cha NIT, Bahati Mabina alisema washiriki waliobahatika kupata mafunzo hayo ni 42, madereva wakiwa ni 16 na maafisa Usafirishaji 26 na kuwa ni ya siku tano.
Imani Octavian mshiriki wa mafunzo hayo kutoka makampuni binafsi akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake alisema wamejifunza mengi kupitia mafunzo hayo na kuwa wanaenda kuwa mabalozi kwa wenzao.
Alisema mafunzo hayo yamelenga kuwaepusha na uingiaji wa gharama kubwa ya uendeshaji wa kazi zao kwa kutumia magari kama vile matumizi ya mafuta, matairi na matengenezo na kuwa maeneo yote hayo matatu yameguswa na wakufunzi wa mafunzo hayo.
Katibu Tawala Wilaya ya Singida, Goodluck Mwangomango akizindua kozi hiyo.
Mkuu wa Chuo cha Taifa Cha Usafirishaji (NIT) Mhandisi Profesa Zacharia Mganilwa, akitoa historia fupi ya chuo hicho na malengo ya kozi hiyo.
Mkuu wa Kituo cha Mafunzo Endelevu cha NIT, Bahati Mabina, akizungumzia washiriki wa mafunzo hayo.
Afisa Uhusiano Mkuu wa chuo hicho, Tulizo Chusi, akizungumza kabla ya kuzinduliwa kozi hiyo.
Washiriki wakiwa kwenye uzinduzi wa kozi hiyo.
Kozi ikizinduliwa.
Washiriki wakiwa kwenye kozi hiyo.
Uzinduzi wa kozi hiyo ukiendelea.
Wakufunzi wa kozi hiyo wakiwa kwenye uzinduzi huo.
Kozi ikizinduliwa.
Taswira ya kozi hiyo.
Picha ya pamoja na amgeni rasmi.
Picha ya pamoja na mgeni rasmi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...