Na Mwandishi wetu, Mirerani
MKURUGENZI wa kampuni ya Franone Mining and Company LTD, inayomiliki kitalu C kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite Mji Mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Onesmo Mbise (Onee) amepongezwa kwa namna anavyowasaidia mchanga wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.
Wanawake wachekechaji kutokana na hali hiyo ya kuwapatia udongo kwa ajili ya kuchekecha na kujipatia mabaki ya madini ya Tanzanite, wamempongeza Onee kwa kumpatia zawadi ya fimbo yenye maana ya kiongozi wa kimila, mbuzi na blanketi ya kujikinga na baridi.
Pia, wanawake hao wamewapatia zawadi ya mbuzi na blanketi Afisa madini mkazi (RMO) wa Mirerani mhandisi Menard Msengi na mjiolojia Ezra Gregory Ntaluka, kwa kufanikisha utaratibu mzuri wa kupata mchanga kutoka kampuni ya Franone Mining LTD.
Mkurugenzi wa kampuni ya Franone Mining LTD, Onesmo Mbise, akizungumza baada ya kukabidhiwa zawadi hizo za mbuzi, blanket na rungu ya kiongozi wa kimila, amewashukuru kwa kumpatia zawadi hizo kwa kutambua mchango wake.
"Hivi sasa udongo umeongezeka hivyo tumuombe Mungu tupate riziki ili tuweze kufaidika kwa pamoja pia tunampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyowajali Wataanzania," amesema Onee.
Hata hivyo, amewataka vijana wanaowaghasi wanawake, wazee na watu wenye ulemavu kuachana na tabia hiyo kwani wao bado wana nguvu hivyo wakafanye kazi kwenye migodi.
Diwani wa viti maalum Tarafa ya Moipo, Pauline Makeseni amesema wanawake hao wametoa zawadi hizo ili kuishukuru kampuni ya Franone Mining LTD kupitia Mkurugenzi wake Onesmo Mbise kwa namna ilivyosaidia jamii.
"Tunaomba kampuni nyingine ziige mfano wa Franone katika kusaidia jamii inayozunguka hasa kwa wanawake, wazee na watu wenye ulemavu ili kuondokana na umasikini," amesema Makeseni.
Diwani wa Kata ya Naisinyai, Taiko Kurian Laizer amepongeza Mkurugenzi wa kampuni ya Franone Mining LTD Onesmo Mbise kwa kusaidia kundi hilo maalum lenye uhitaji la wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.
"Hivi sasa wanawake wanafaidika kupitia kampuni ya Franone Mining LTD, kutokana na kupata riziki ndiyo sababu mimi nimeshiriki pamoja nanyi kwenye tukio hili la kumpongeza Mkurugenzi wa kampuni ya Franone Mining LTD na maofisa wa madini," amesema.
Amemkabidhi Onee rungu kwa ajili ya heshima ya kiongozi wa kimila (Mshili) kwa sababu ya kuwasaidia wanawake hao waliomvika blanket na kumkabidhi mbuzi.
Afisa madini mkazi RMO wa Mirerani, mhandisi Menard Msengi amewashukuru wanawake hao kwa kutambua mchango wao hadi kuwapa zawadi hizo.
"Hivi sasa kuna utaratibu mzuri wa kupata mchanga tofauti na pale awali kulipokuwa na vurugu na kugombania ila sasa hivi ni tofauti, endeleeni hivyo hivyo ili muweze kufanya kazi zenu vizuri," amesema mhandisi Msengi.
Mwenyekiti wa UWT Kata ya Endiamtu, Claudia Dengesi amesema kitendo cha kampuni ya Franone Mining LTD kutoa mchanga kwa wahitaji hao kinapaswa kupongezwa kwani ni msaada mkubwa kwa jamii.
Mwenyekiti wa UWT Kata ya Mirerani Mama Mwaselela ameishukuru kampuni ya Franone kwa kuwajali wapiga kura wao wanawake kwa kuwapatia mchanga kwani unawanufaisha kiuchumi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...