Mabibi na Mabwana,
NAWASALIMU KWA JINA LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA……

Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema
ambaye ametuwezesha kuifikia siku hii ya leo tukiwa wazima wenye afya njema.
Aidha, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,
Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philipo Isdor Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim
Majaliwa Majaliwa, Waziri wa Afya Mhe. Ummy Ally Mwalimu, Naibu Waziri wa
Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe,
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe na Mganga Mkuu wa
Serikali Prof. Tumaini Nagu kwa kuiwezesha Taasisi yetu kutekeleza majukumu
yake kwa ufanisi zaidi. Nawashukuru Wafanyakazi wote wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete kwa kujitoa kwao kuwahudumia wananchi wenye matatizo ya
moyo. Pia nipende kuwashukuru Waandishi wa Habari kwa kufanya kazi na Taasisi
yetu bega kwa bega ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi za magonjwa
ya moyo pamoja na huduma tunazozitoa.

Ndugu Waandishi wa Habari, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ni hospitali
maalumu inayotoa tiba ya magonjwa ya moyo, mafunzo na utafiti. Katika
kutekeleza majukumu yake Taasisi imeendelea kuzingatia sera, mipango na
mikakati yenye lengo la kuimarisha utoaji wa huduma za kibingwa za matibabu ya
magonjwa ya moyo hapa nchini.

Taasisi yetu inafanya yafuatayo:
a) Wagonjwa wanaotibiwa kwa siku ni 500.
b) Wagonjwa wanaolazwa kwa wiki ni 130
c) Wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wa kufungua kifua,
upasuaji wa mishipa ya damu na mapafu kwa siku ni sita.
d) Kupitia mitambo ya Cathlab (Catheterization Laboratory) wagonjwa
wanaochunguzwa, kuzibuliwa mishipa ya damu ya moyo na kuwekewa
vifaa visaidizi vya moyo kwa siku ni 14.

Ndugu Waandishi wa Habari, kwa mwaka wa fedha uliopita wa 2022/23
Taasisi yetu ilitengewa kiasi cha shilingi bilioni 44.5 fedha ambazo zilitumika
kufanya shughuli mbalimbali za utoaji wa huduma ya matibabu ya moyo
pamoja na shughuli za maendeleo. 
Katika mwaka huo wa fedha Taasisi
ilifanikiwa kufanya yafuatayo:
a) Tuliona wagonjwa 122,362 kati ya hawa watu wazima walikuwa 111,542
na watoto 10,820 wagonjwa waliolazwa walikuwa 4407 watu wazima
3286 na watoto 1121.
b) Wagonjwa waliofanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wa kufungua kifua
na kubadilishwa Valvu za moyo moja hadi tatu, upasuaji wa kupandikiza
mishipa ya damu ya moyo (Coronary Artery Bypass Graft Surgery
–CABG), upasuaji wa mishipa ya damu na mapafu walikuwa 714 kati ya
hao watu wazima walikuwa 412 na watoto 305. Watoto tuliowafanyia
upasuaji walikuwa na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni
matundu na mishipa ya damu ya moyo kutokukaa katika mpangilio wake
na matatizo ya Valvu.
c) Kupitia mitambo ya Cathlab (Catheterization Laboratory) ambayo ni
maabara ya uchunguzi wa matatizo na tiba ya magonjwa ya moyo
inayotumia mionzi maalumu wagonjwa 2046 kati yao watu wazima
1762 na watoto 284 walipata huduma za matibabu. Wagonjwa hawa
walipata huduma za uchunguzi, matibabu ya mfumo wa umeme wa
moyo, matibabu ya mishipa ya damu ya moyo iliyokuwa imeziba na
kuwekewa vifaa visaidizi vya moyo.Uchunguzi huu pamoja na tiba
unafanyika kwa njia ya upasuaji wa bila kufungua kifua kupitia tundu
dogo linalotobolewa kwenye paja.
d) Gharama ya matibabu ya wagonjwa hawa 2,760 tuliowafanyia upasuaji
mkubwa na mdogo wa moyo kama wangetibiwa nje ya nchi ni shilingi
62,340,000,000 lakini kwa kutibiwa kwao katika Taasisi yetu matibabu
yao yamegharimu kiasi cha shilingi 31,170,000,000 fedha ambazo
zimelipwa na bima za afya, ndugu wa wagonjwa, wafadhili na wengine
kupata msamaha wa matibabu. Kwa wagonjwa hawa kutibiwa hapa
nchini Serikali imeweza kuokoa kiasi cha shilingi 31,170,000,000 fedha
ambazo zingelipwa kama wagonjwa hawa wangetibiwa nje ya nchi.
e) Kwa kipindi cha mwaka mmoja wagonjwa waliotibiwa katika Taasisi yetu
kutoka nje ya nchi walikuwa 301. Wagonjwa hawa walitoka katika nchi
za Somalia, Malawi, Kenya, Rwanda, Uganda,Zambia,Visiwa vya Comoro,
Ethiopia, Burundi na wengine kutoka nje ya Afrika zikiwemo nchi za
Armenia, China, India, Norway, Marekani na Uingereza.
f) Taasisi ilitumia shilingi bilioni 1,249,521,800 kwaajili ya kununua
mashine mbalimbali zikiwemo za utasishaji wa  vifaa vya Hospitali,
Digital X-Ray na mashine tatu za kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi
(Echocardiography).
g) Tarehe 20/4/2023 Taasisi yetu ilisaini makubaliano ya miaka miwili na
Hospitali za Taifa za nchini Rwanda na Zambia ya kutibu wagonjwa wa
moyo pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa hospitali
hizo. Pia tumesaini makubaliano ya kushirikiana katika utoaji wa
huduma za matibabu kwa wagonjwa, kubadilishana ujuzi wa kazi,
kufanya tafiti mbalimbali na kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wetu na
chuo Kikuu cha Jagiellonian cha nchini Poland, chuo cha madaktari wa
upasuaji Afrika Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (COSESCA) nchi ya
Malawi, Visiwa vya Comoro, Taasisi ya Afya  Ifakara (IHI), Taasisi ya Taifa
ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) na Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam.
h) Kupitia kozi ya miezi sita ya mafunzo ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa
mahututi na wa dharura inayotolewa kwa wauguzi kati ya wanafunzi 50
waliomaliza sita walitoka katika nchi za Rwanda na Zambia.
i) Katika kutoa huduma za tiba mkoba zijulikanazo kwa jina la Mhe.
Dkt.Samia Suluhu Hassan Outreach Services tulifanya upimaji na
matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi kwa kuwafuata mahali
walipo. Huduma hii imetolewa katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma,
Pwani, Arusha, Geita, Iringa, Mtwara, Lindi, Unguja, Manyara na Pemba.
Wananchi 6309 walifikiwa na huduma hii kati ya hao 3239 walikutwa na
matatizo ya moyo na waliopewa rufaa ya kuja kutibiwa JKCI walikuwa
724.
j) Mwezi Mei mwaka huu wataalamu wetu walikwenda nchini Malawi
katika Hospitali ya Queen Elizabeth kutoa huduma za upimaji na
matibabu ya magonjwa ya moyo, huduma hii ilitolewa kwa watu 724.
Waliokutwa na matatizo ya moyo walikuwa 537 kati yao 201 walipewa
rufaa ya kuja kutibiwa katika Taasisi yetu.
k) Serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma iliajiri
wafanyakazi wapya 64 wa kada mbalimbali na wafanyakazi 98
walipandishwa vyeo katika madaraja tofauti. Wafanyakazi 50 walilipiwa
ada za masomo katika kozi mbalimbali walizozifanya.

l) Tarehe 14 Novemba mwaka jana Serikali ilitupatia Hospitali ya Dar
Group iliyopo wilayani Temeke kuwa sehemu ya JKCI. Kwa kutupatia
hospitali hii kumetatua changamoto ya nafasi ambayo tulikuwa
tunakabiliana nayo kwa muda mrefu na kutatusaidia kuboresha huduma
za matibabu tunazozitoa kwa wananchi.
m) Tumechapisha matokeo ya tafiti za kisayansi (Publication) 12 katika
majarida ya kimataifa (International scientific journals).

Ndugu Waandishi wa Habari, Kwa mwaka wa fedha 2023/24 Taasisi imetenga
bajeti ya kiasi cha Shilingi Bilioni 66.3 fedha hizi zitatumika kwaajili ya utekelezaji
wa kazi mbalimbali zilizoainishwa kwenye Mpango Kazi na Bajeti ya Mwaka
2023/24.
Taasisi itatumia fedha hizi kulipa mishahara ya wafanyakazi, uendeshaji wa
gharama za Taasisi, manunuzi ya vifaa tiba na dawa, kusomesha wataalamu wetu
kozi za muda mrefu na muda mfupi pia zitatumika kwenye miradi ya maendeleo
ikiwemo ujenzi wa jengo la vipimo vya uchunguzi wa magonjwa pamoja na ofisi za
utawala, ujenzi wa jengo la kutolea huduma za matibabu kwa watoto katika
Hospitali yetu ya Dar Group na ununuzi wa vifaa kazi.
Mchanganuo wa maeneo ambayo yamepewa kipaumbele katika bajeti kwa
mwaka wa fedha wa 2023/24 ni pamoja na yafuatayo:-
a) Kuimarisha tiba za moyo kwa kudhamini masomo ya muda mfupi na mrefu
kwa wafanyakazi, kununua vifaa tiba vya kisasa zaidi, kuendeleza ujenzi
mbalimbali, kutoa huduma za tiba mkoba kwa kuwafuata wananchi walipo.
b) Kuendelea kutoa elimu ya magonjwa ya moyo pamoja na lishe bora kwa
wananchi kupitia luninga, magazeti na mitandao ya kijamii.
Ndugu Waandishi wa Habari, manufaa ambayo wananchi watayapata kupitia
vipaumbele vya Taasisi kwa mwaka wa fedha 2023/24 ni pamoja na:
a) Kuzidi kuimarika kwa huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo kwani
wataalamu wanazidi kuongeza ujuzi walionao kupitia kozi za muda mrefu
na mfupi wanazosoma pia kununuliwa kwa vifaa tiba vya kisasa kutasaidia
kutolewa kwa huduma bora kwa wananchi.
b) Kukamilika kwa jengo la utawala na vipimo ambalo limegharimu kiasi cha
shilingi bilioni 3.6 kutasaidia wagonjwa wengi zaidi kupata huduma za
vipimo vya moyo kwa wakati pia wafanyakazi watakuwa na ofisi za kutosha
na hivyo kupunguza msongamano katika ofisi walizopo.
c) Taasisi itaendelea kusogeza huduma za matibabu ya kibingwa ya moyo kwa
wananchi kwa kuwafuata mahali walipo (Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan
Outreach Services) kwa kufanya hivyo wenye matatizo ya moyo watapata
huduma za matibabu mapema tofauti na ambavyo wangezifuata huduma
hizo Dar es Salaam. Tunafanya hivi kwa kuwa asilimia kubwa ya wagonjwa
tunaowatibu mioyo yao huwa imechoka hii ni kutokana na kuchelewa
kufika JKCI kwaajili ya kupata matibabu ya kibingwa ya magonjwa haya.
d) Kupitia vyombo vya habari Taasisi itaendelea kutoa elimu ya jinsi ya
kuyaepuka magonjwa ya moyo kwa wananchi kwani magonjwa haya ni
moja ya magonjwa yasiyoambukiza na mtu anaweza kuyaepuka akifuata
mtindo bora wa maisha. Pia tutaendelea kutoa elimu ya matumizi sahihi ya
dawa za moyo pamoja na umuhimu wa kufuata ushauri wa wataalamu wa
afya kwa wagonjwa wa moyo.
Ndugu Waandishi wa Habari, ninaomba nimalizie taarifa yangu kwa
kuwakumbusha wananchi mambo yafuatayo:
a) Unaweza kuepuka kupata magonjwa ya moyo kwa kufanya mazoezi.
b) Kuzingatia lishe bora kwa kula matunda, mboga mboga, vyakula vyenye
madini ya potassium vile vile kupunguza kula vyakula vyenye kiasi kikubwa
cha mafuta na chumvi.
c) Kuepuka uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe uliokithiri, kutambua
kiwango cha sukari katika mwili wako, kutambua msukumo wako wa damu
na kiwango cha mafuta mwilini.
d) Kupima afya ya moyo japo mara moja kwa mwaka kunaweza kukakusaidia
kujua kama una tatizo hili au la na kama unatatizo utaweza kupata
matibabu mapema.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.

“Afya ya Moyo Wako ni Jukumu Letu”.

 Imetolewa na :
Dkt. Peter Kisenge
Mkurugenzi Mtendaji
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
18/07/2023

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...