Na Rahma Khamis Maelezo
Waziri wa Habari Vijana Utadumu na Michezo Zanzibar Mhe, Tabia Maulid Mwita amewataka wananchi kutumia kiswahili sanifu ili kuitunza na kuikuza lugha hiyo.
Ameyasema hayo huko Ofisini kwake Migombani wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani.
Amesema Kiswahili ni lugha mama inayotumika katika sehemu tofauti ndani na nje ya nchi ingawa bado kuna baadhi ya watu wanakichafua kutokana na kukitumia bila ya kuzingatia usahihi wake.
“Licha ya lugha hiyo kuendelea kutumika duniani kote lakini bado kuna mapungufu kwa baadhi ya watumiaji ,wanakiharibu na kukichafua kutokana na kukua kwa utandawazi nchini,”alisema Waziri Tabia.
Aidha amefahamisha kuwa mambo ya utandawazi yamepelekea kuharibu kiswahili hivyo wamejipanga kuhakikisha kiswahili kinatumika na kuwataka wanahabari kuhamasisha matumizi bora ya kiswahili kwani viongozi wote wakuu ni wadau wa kiswahili.
Akizungumzia kuhusu mikakati ya Serikali katika kulinda Utamaduni wa Mswahili Waziri Tabia ameeleza kuwa wamejipanga vizuri kuhakikisha wanapokuja wageni wanatumia lugha rafiki ili wageni hao waweze kufuata utamaduni wa Zanzibar bila kuharibu Utalii.
Aidha amefahamisha kuwa katika kuelekea siku ya Kiswahili Duniani , Julai 4 wanatarajia kufanya mkutano maalum na wahariri wakuu wa Vyombo vya Habari katika Ukumbi wa Idriss-Abdul Wakili Kikwajuni ambapo katika mkutano huo watajadili Nafasi ya wahariri Wakuu katika matumizi ya Kiswahili sanifu kwenye vyombo vya habari.
Katika hatua nyengine Waziri amefafanua kwamba Julai 5 kutafanyika mjadala mpana katika Ukumbi huohuo ambapo mada kuu itakuwa ni Kiswahili ni nyenzo ya ukombozi wa fikra kwa maendeleleo ya kiuchumi Barani Afrika.
Waziri Tabia ameongeza kwa kusema kuwa Julai 6 kutafanyika matembezi yatakayoanzia Skuli ya Sekondari Dkt Shein hadi Ukumbi wa Ziwani Polisi ambako kutafanyika ufunguzi rasmi wa maadhimisho hayo.
Hata hivyo Waziri huyo amewaomba wananchi kujitokeza na kushiriki kwa wingi katika maadhimisho ya Siku ya kiswahili ili kukitangaza na kukitumia zaidi duniani kote.
Nae Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Said Yakubu amesema ushirikiano kati yao na Zanzibar upo karibu sana hasa katika shughuli za kiutamaduni kwani wanafanya kazi kwa pamoja na wamekuwa wakipanga mipango ili kuhakikisha maadhimisho hayo yanakwenda sawa.
Siku ya Kiswahili duniani huadhimishwa kila ifikapo Julai 7 ambapo maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika katika Ukumbi wa Ziwani Polisi na kuhudhuriwa na wageni kutoka ndani na nje ya nchi ikikwemo Urusi,Ghana ,Ujerumani ,Comoro na Mombasa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...