NA. ZAINABU ALLY -  DODOMA.

Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania - TANAPA limejipanga kukusanya mapato kupitia vyanzo vyake vya ndani kiasi cha Shilingi Bilioni  343.8 katika  mwaka wa fedha 2023/2024 tofauti na mwaka jana ambapo ilikusanya shilingi bilioni 337.

Akitoa taarifa hiyo leo Julai 24, 2023 katika mkutano na wanahabari ulifanyika katika Ukumbi wa Idara ya Habari - Maelezo jijini Dodoma juu ya mwelekeo  wa Shirika hilo katika kukuza shughuli za Utalii  kwa mwaka wa fedha 2023/2024, Kamishna Mwakilema amesema "TANAPA  imeweka mikakati thabiti ya kuongeza idadi ya watalii kufikia 1,802,460 kwa mwaka 2023/2024".

Kamishna Mwakilema alisema, "shirika lina dhamana ya kusimamia na kuendeleza maeneo yaliyoteuliwa kuwa hifadhi za taifa hivyo TANAPA imeweka vipaumbele katika maeneo ya uhifadhi, ulinzi, utalii, ushirikishaji jamii na uboreshaji wa miundombinu pamoja na ukamilishaji wa miradi ya kimaendeleo ya shirika ili kufikia malengo tuliojiwekea".

Aidha, shirika limejipanga kuboresha miradi ya maendeleo kwa ukarabati wa viwanja vya ndege katika Hifadhi za Taifa za Ruaha, Mikumi na Nyerere, ikiwa ni pamoja na ununuzi wa ndege na Helikopta ili kuimarisha utalii pamoja na shughuli za ulinzi mkakati.

Hata hivyo, Kamishna Mwakilema alisema, "shirika limeendelea kujipanga katika kuboresha miradi ya maendeleo kwa kutenga bilioni 60.6 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ili kuwezesha utekelezaji wa maendeleo katika miradi mbalimbali inayosimamiwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania(TANAPA)".

Sanjari na utekelezaji wa mipango hiyo itakayoweza kuimarisha uchumi kwa shirika na taifa kwa ujumla TANAPA pia, imejipanga kumaliza changamoto za uhifadhi kwa kushirikiana na taasisi nyingine za uhifadhi na serikali kwa kufanya kazi kwa weledi ili kumaliza migogoro ya wanyamapori wakali na waharibifu.

Naye, Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa alitoa shukrani  kwa shirika kutoa ufafanuzi juu ya muelekeo wa TANAPA mbele ya wanahabari hao ambao utawaongezea uelewa kutoa taarifa sahihi zinazohusiana na ulinzi wa hifadhi za taifa na kuwa mabalozi wazuri  wa kuvitangaza vivutio vya utalii kwa wananchi na namna shirika hilo linavyofanya kazi zake kwa weledi na maarifa.

‘’Nikushukuru sana Kamishna wa Uhifadhi -  TANAPA kwa taarifa yako  yenye malengo chanya ya kukuza utalii na iliyotilia mkazo suala zima la uhifadhi wa maliasili. Hivyo ni matumaini yangu kuwa wanahabari hawa wameelewa dhana nzima ya uhifadhi wa vyanzo vya maji hivyo kupitia kalamu zenu watanzania wataelewa shughuli nzima ya uhifadhi’,’ alisema Msigwa.

Aidha, shirika linaendelea  kutekeleza sera ya ujirani mwema ambapo pamoja na kutoa elimu ya uhifadhi shirika litaendelea kutekeleza miradi ya ujirani mwema  iliyoanzishwa na jamii kwa kuchangia kiasi cha shilingi bilioni 2.3 kwenye miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2023/2024, katika wilaya 20 za kipaombele.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...