Njombe
Baadhi ya vijana wa mtaa Kikula na Kipagamo halmashauri ya mji wa Makambako mkoani Njombe wamezua taharuki makaburini na kusababisha masikitiko kwa wazee wa mitaa hiyo baada ya kitendo cha kugoma kuushusha mwili wa marehemu Peter Kibiki (30) kaburini na kuuzika wakihoji ni kwanini vijana wanapoteza maisha huku wazee wakiendelea kuishi.
Stephano Kigodi ni mmoja wa kijana aliyekuwepo makaburini amebainisha kuwa vijana waligomea kuuzika mwili wa kijana mwenzao wakidai kuwa sababu kubwa ni hofu ya vifo ambapo ndani ya wiki moja wamezika wanne huku watatu wakiwa ni ukoo mmoja.
"Huyu naye ambae tumezika leo amegonga gari aliyosimama na tumeshazika misiba minne mfululizo kweli ushirikina upo lakini hatutuhumu mtu yeyote"alisema Kigodi.
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Kikula Batwery Makweta amesema vijana hao waligoma kuuzika mwili huo huku wakitaka wazee wafanye kazi hiyo na kueleza kuwa wamechoshwa na aina ya vifo vinavyotokea kwa vijana kwenye mitaa yao wakihusisha na Imani za ushirikina.
"Wametugomea kuingiza mwili wa Marehemu kwenye kaburi Jambo hili limeleta taharuki kwa kiasi kikubwa tumesikitika sana kwasababu kifo hakina umri na hakuna ratiba ambayo Mungu alitoa kwamba mtu afe katika mazingira gani"alisema Makweta
Diwani wa kata ya Makambako John Ngimbuchi na Mchungaji wa kanisa la KKKT mtaa wa Kipagamo Daud Santuru wametoa wito kwa vijana kuachana na mila potofu kwani kifo kinaweza kumpata mtu yeyote pasipo kujali umri ambapo mara baada ushauri kutoka kwa viongozi hao ndipo baadhi ya vijana wachache wakakubali kuuhifadhi mwili wa Peter Kibiki aliyepoteza maisha kutokana na ajali ya gari hapo Julai 9 mjini Mafinga akiwa ametoka Morogoro.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...