Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa taasisi za fedha nchini kutumia vema Maonesho ya Kilimo ya NaneNane yanayoendelea jijini Mbeya kwa kutoa elimu kuhusu masuala ya fedha kwa wakulima huku akiipongeza Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa kuandaaa banda maalum kwa ajili ya kutoa elimu hiyo.

Dkt. Mpango alitoa wito huo jana wakati alipotembelea banda la maonesho la Benki ya NBC lililopo kwenye viunga vya Uwanja wa John Mwakangale jijini humo akiwa ameambatana na viongozi wengine waandamizi akiwemo Spika Bunge la Jamhuri wa Muungano ambae pia ni Mbunge wa jimbo la Mbeya Mjini Dkt Tulia Ackson, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bw Juma Homera na viongozi wengine waandamizi kutoka Chama tawala pamoja na serikali.

Kwa mujibu wa Dkt Mpango hatua hiyo itawasaidia wakulima kwa kuwajengea uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya kifedha ikiwemo aina ya mikopo inayotolewa na taasisi hizo, viwango vya riba na makato mengine ili waweze kufanya uamuzi sahihi pindi wanapofanya uamuzi mbalimbali yanayohusisha fedha.

‘’Nimevutiwa zaidi kuona kwamba benki ya NBC kwenye suala hili la elimu ya fedha mmeliwekea msisitizo mkubwa kiasi kwamba mmetenga eneo maalum kwa ajili ya utoaji wa elimu kuhusu huduma zenu za kifedha hususani riba na uwekezaji kwa wakulima…hongereni sana kwa hatua hiyo ambayo ningependa taasisi nyingine zifanye hivyo pia. Natamani kuona taasisi za fedha zinatumia vema maonesho haya kwa faida ya wakulima si tu kutoa huduma zao kwa washiriki bali elimu ndio iwe kipaumbele,’’ alisisitiza.

Awali akifafanua kuhusu baadhi ya huduma za benki hiyo mahususi kwa wakulima, Mkuu wa kitengo cha wateja wadogo wadogo, Lariba na wakulima kutoka Benki ya NBC, Bw Raymond Urassa alisema benki hiyo imeendelea kubunio huduma zaidi mahususi kwa wakulima ikiwemo mikopo ya zana za kilimo ikiwemo matrekta, mashine za kuvuna (Combine harvester), huduma za bima ya kilimo, program maalum ya utoaji wa elimu ya fedha kwa wakulima sambamba na kuwaunganisha wakulima na mitandao ya kibenki ili kuwarahishia huduma za kibenki.

‘’Kwa mwaka huu pekee tayari tumetoa mikopo ya matrekta 69 kwa wakulima sambamba na mikopo ya ‘combine harvester’ ili tu kuongeza matumizi ya vifaa vya kisasa kwenye sekta kilimo. Kupitia huduma ya bima, kwa kushirikiana na kampuni ya Bima ya Jubelee tunatarajia kuwalipa fidia wakulima wa tumbaku walioathirika na mvua za mawe kwenye msimu wa kilimo mwaka jana,’’ alisema Urassa.

Akizumzungumzia zaidi kuhusu elimu ya fedha kwa wakulima, Bw Urassa alimuhakikisha Dkt Mpango kuwa benki hiyo inayatumia vema maonesho hayo kwa kuhakikisha kuwa mbali na kutoa huduma za kifedha kwa washiriki, pia msisitizo unawekwa kwenye utoaji wa elimu kwa wakulima wakubwa na wadogo ili waweze kuelewa vizuri huduma za benki hiyo, aina ya mikopo inayotolewa na riba zake pamoja na elimu ya uwekezaji kwenye fursa mbalimbali kwenye sekta ya kilimo.

‘’ Tulibaini kuwa wakulima wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu riba na viwango vyake kwa hiyo walikuwa wanakopa bila kujua tafsiri ya viwango vya riba jambo ambalo ni muhimu sana na hiyo ndio sababu kupitia maonesho haya elimu ya mambo kama hayo tumeipa kipamumbele. Zaidi pia kwenye maonesho haya tunajivunia huduma yetu ya akaunti ya wakulima inayozingatia misimu ya kilimo na hivyo haifungwi ndani ya miezi 24 inapokuwa haitumiki na hata baada ya kipindi hicho mkulima bado atakuta akaunti ikiwa hai tena ikiwa na ongezeko la faida,’’ alisema.

Bw Urassa alitoa wito kwa wakulima na wadau wengine wa kilimo pamoja na washiriki mbalimbali wa maonesho hayo kutembelea banda la benki hiyo ili kunufaika na elimu inayotolewa bure kuhusu huduma mbalimbali za kifedha zinazohusiana na sekta ya kilimo huku akiahidi kwa niaba ya benki hiyo kuendelea kubuni na kutoa huduma zinazoendana na mahitaji wa wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo wakiwemo wakulima wakubwa na wadogo, wasambazaji wa pembejeo za kilimo pamoja na wauza mazao ya kilimo.

Mkuu wa kitengo cha wateja wadogo wadogo, Lariba na wakulima kutoka Benki ya NBC,  Raymond Urassa (kulia)  akielezea mbele ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango (wa tatu kushoto) kuhusu huduma mbalimbali mahususi kwa wakulima zinazotolewa na benki hiyo wakati Makamu wa Rais alipotembelea banda  la benki hiyo kwenye Maonyesho ya Kilimo Nanenane yanayofanyika katika Uwanja wa John Mwakangale mkoani Mbeya karibuni. Wengine ni pamoja na Spika Bunge la Jamhuri wa Muungano ambae pia ni Mbunge wa jimbo la Mbeya Mjini Dkt Tulia Ackson (katikati) na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe (kushoto)






Maofisa wa Benki ya NBC wakiwahudumia wadau mbalimbali wa kilimo waliotembelea banda la benki hiyo lililopo kwenye maonyesho  hayo.


NBC Shambani…Vuna  Zaidi na NBC!



 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...