Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imesema ipo tayari kushirikiana kikamilifu na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kwa kutumia umeme gridi ya Taifa baada ya ujenzi wa kituo cha kupoza umeme na mradi wa kupeleka umeme katika migodi ya kampuni hiyo kukamilika.
Pia imeipongeza Tanesco na Wizara ya Nishati kwa kuja na mpango mkakati wa miaka 10 utakaoliwezesha shirika hilo kuanzisha vyanzo vipya vya nishati endelevu kwani ni jambo litakalolisaidia Taifa kutimiza lengo namba saba la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) linalozungumzia matumizi ya nishati inayofikika, ya gharama nafuu, endelevu na ya kisasa kwa wananchi wake.
Hayo yameelezwa jana na Makamu Rais wa AngloGold Ashanti- GGML anayeshughulikia miradi endelevu kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo wakati akichangia mjadala wa nishati kupitia Jukwaa la fikra la Mwananchi.
Shayo amesema mpango huo mkakati wa miaka 10, utaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza kusini mwa nchi za Jangwa la Sahara kutimiza lengo hilo la maendeleo endelevu (SDGs)
"Ni hatua kubwa kwa Tanesco kutafsiri kwenye mkakati wake lile lengo namba saba," amesema na kuongezalicha ya kampuni nyingi za madini tangu miaka ya 2000 hutumia umeme wanaouzalisha wenyewe.
"Sasa Serikali imekuwa na jitihada za makusudi kufungamanisha sekta ya nishati na sekta kubwa za uzalishaji kwa kuzalisha umeme unaotosheleza mahitaji ya wawekezaji wakubwa.
"Sisi kwa sekta ya madini tunaona hii kama ni baraka kubwa kwa sababu huwezi kuendesha migodi mikubwa kama ya kwetu (GGML) kwa kutumia jenereta," amesema.
Ametoa mfano kuwa GGML hutumia megawati 29 ambazo huzalisha kwa mafuta lakini sasa wanatamani kuona mradi wa kupeleka umeme wa Tanesco katika mgodi wa kampuni hiyo ukikamilika ili kupunguza gharama za uendeshaji.
"Tukijiunga tu na Tanesco kwenye gridi ya Taifa na kutoka kwenye umeme tunaouzalisha wenyewe, tutapunguza gharama za umeme kwa asilimia 50, tuta-save dola za Marekani milioni 19 kila mwaka. Pia tutapunguza hewa ya ukaa kilotons 81 kufikia 2030," amesema.
Ameongeza kwa kuwa nchi ipo katika mipango ya kuwekeza pakubwa katika sekta ya madini kwa kuanzisha migodi ya uzalishaji wa madini mengine sehemu mbalimbali nchini
Amesema ni Dhahiri kuwa Tanesco itafanikiwa kuongeza mapato makubwa kutokana na mchango wa migodi hiyo kwenye matumizi ya umeme.
Amesema Tanesco wanajenga laini ya kilovolt 220 kutoka Bulyanhulu hadi Geita kisha laini ya kilomita sita yenye kilovolt 33 kuelekea katika mgodi wa GGML ilihali kampuni hiyi ikijenga kituo cha kupoza umeme kwenda kilovolt 11 kwa gharama ya dola za Marekani milioni 24.4.
Awali akizindua mpango huo mkakati wa Tanesco, Waziri wa Nishati, Januari Makamba amewataka wananchi wawe na subira wakati Shirika hilo linafanya mageuzi ya utendaji kazi wake.
Amefafanua Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuipa mtaji TANESCO ili itekeleze mipango yake kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa wananchi na Afrika kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa TANESCO, Maharage Chande amesema shirika hilo linakusudia kuendelea na mipango yake ya kuboresha huduma kwa wateja wake, kupitia miradi mbalimbali ikiwemo wa kufua umeme katika Bwawa la Julius Nyerere, ambao unatarajia kuanza kuzalisha umeme Juni 2024.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...