Na Muhidin Amri,
Tunduru


HOSPITALI ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma,imezindua kampeni mpya ya kutokomeza ugonjwa huo kwa 
kutembelea kwenye vilinge(makambi) ya waganga wa tiba asili na tiba mbadala ijulikanayo kwa jina la Kilinge kwa Kilinge.


Kampeni hiyo,inakusudia 
kuwapata watu wote waliokatisha matibabu ya  Hospitali na kuacha kumeza dawa  ambao wamekimbilia kwa waganga wa tiba asili na kuwaibua wagonjwa wapya walioambukizwa ugonjwa huo ili waweze kuanzishiwa matibabu.


Mratibu wa kifua kikuu na 
ukoma wa wilaya hiyo Dkt Mkasange Kihongole amesema hayo jana, kabla ya kuanza zoezi la uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu kwa wananchi waliokutwa wakipata matibabu kwa Mganga maarufu wa tiba asili na tiba mbadala Bi Naweza mkazi wa kijiji cha Semeni wilayani humo.


Alisema,kitengo cha kifua 
kikuu na ukoma imeamua kuzindua kampeni hiyo kwa kufika kwenye vilinge vya waganga  hao kutokana na uwepo wa idadi kubwa wa watu kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini wanaofika ili kupata matibabu.


Mkasange alisema,kwenye 
vilinge vya waganga wa tiba asili ni miongoni mwa maeneo hatarishi ambayo watu wanaweza kuambukizwa ugonjwa huo kwa urahisi kwa sababu ni maeneo yanayopokea watu  wenye magonjwa tofauti ikiwemo ugonjwa wa hatari wa TB.


Alieleza kuwa,kwa kawaida 
ugonjwa wa kifua kikuu  unaambukizwa kwa njia  ya hewa hivyo,mtu mwenye ugonjwa huo ambaye hajaanzishiwa matibabu ni rahisi kuambukiza wengine pale anapopiga chafya na kukohoa kama hakutakuwa na tahadhari yoyote.


Alisema kutokana na hali hiyo,
Hospitali ya wilaya ya Tunduru kitengo cha kifua kikuu na ukoma imeanza kampeni hiyo ya kutoa elimu kwa waganga wenyewe,wasaidizi wao na wananchi wote wanaokwenda kwenye vilinge kwa ajili  ya kupata matibabu.


Dkt Mkasange alisema,kampeni 
ya uchunguzi kwenye vilinge vya waganga wa tiba asili sambamba na zoezi la kutoa elimu ya ugonjwa huo ni endelevu ili kuwaepusha watu na waganga wenyewe kuambukizwa ugonjwa huo.


Msaidizi wa mganga wa Tiba 
asili na tiba mbadala Bi Naweza Salum Mtingala alisema,kwa siku wanapokea  zaidi ya watu 2,000 kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini wanaofika kwa ajili ya kupata matibabu.


Alitaja huduma zinazotolewa 
na Bi Naweza ni upasuaji wa mabusha,tezi dume bila kutoka damu na magonjwa mengine kwa kutumia dawa za asili ambazo zimekuwa msaada mkubwa kwa watu wanaofika kwa mganga huyo.


Aidha Mtingala,ameipongeza 
Hospitali ya wilaya Tunduru kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma kupeleka elimu ya kifua kikuu na uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa huo kwani imesaidia wananchi wengi kufahamu na kuchukua tahadhari ili kuepuka kuambukizwa.


Ameiomba serikali kuwaunga 
mkono katika shughuli zao,kwa kuboresha miundombinu ikiwemo barabara na  kupeleka huduma ya maji ili kuwawezesha wananchi kufika kwa urahisi katika eneo hilo lenye mkusanyiko mkubwa wa watu.


Juma Makumbusya,ameishukuru 
serikali  kupitia wizara ya afya kupeleka elimu ya kifua kikuu kwa waganga wa tiba asili kwa kuwa itasaidia kuokoa maisha ya watu wengi ambao  kwa muda mrefu wanaangaika kutafuta majawabu ya shida zao.

Hata hivyo,ameshauri serikali 
kuendelea kushirikiana na waganga wa tiba asili ambao jamii inawaamini na wamekuwa kimbilio kubwa kwa baadhi ya watu wanaosumbua na magonjwa mbalimbali.

Mratibu wa tiba asili na tiba mbadala ambaye pia ni mratibu wa ugonjwa wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Dkt Mkasange Kihongole,akitoa elimu ya ugonjwa huo kwa mamia ya wananchi waliofurika kwa mganga wa tiba asili na tiba mbadala Bi Naweza anayefanya shughuli za kutoa tiba kwa kutumia tiba asili katika kijiji cha Semeni wilayani humo.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Semeni ambaye hakufahamika jina lake akizungumza na umati wa wananchi waliofika kwa mganga wa tiba asili na tiba mbadala Bi Naweza kwa ajili ya kupata matibabu ya maradhi yanayowasumbua.
 

Msaidizi wa mganga wa tiba asili na tiba mbadala Bi Naweza,Salum Mtingala akionyesha vikombe vya maji vinavyotumika wakati wa kutoa huduma ya tiba  kwa wananchi wanaofika kupata huduma za matibabu kwa Bi Naweza.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...