* Rais Samia atajwa kuwa kioo katika jitihada, umakini na ustahimilivu

Na Leandra Gabriel, Dar es Salaam

BINTI Rafat Simba (10,) aliyeandika kitabu cha kubuni (fiction,) 'The First Female President' kilichobeba maono ya Rais wa awamu ya sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amepongezwa kwa kuonesha uzalendo, utu, ubunifu na uongozi kwa watoto na vijana kupitia kitabu hicho.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho leo Agosti 26, 2023 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi rasmi wa kitabu hicho, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Rehema Omary amesema, maboresho yaliyofanywa na Rais Samia katika sekta ya elimu, ikiwemo ujenzi wa madarasa na kutoa ajira kwa walimu yamekuwa chachu kubwa kwa mabinti kama Rafat.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi wa
Serikali, walimu, watunzi, wanafunzi, wazazi na wadau wa sekta ya elimu amesema uchapakazi wake wa kizalendo na umefanya makubwa zaidi kwa kuonesha mwelekeo bora wa sekta ya elimu nchini.

"Rafat amebeba maono makubwa kupitia kitabu hiki ikiwemo utu, uzalendo na uongozi na katika kitabu hiki cha kubuni tumeona uwezo wa binti Sakina mwanamke aliyebeba shabaha kubwa ya kusaidia jamii na taifa, pia kinaonesha mazingira halisi ya sasa tunaona namna Rais Samia Suluhu Hassan alivyo jasiri, shupavu, mstahimilivu na kioo kwa jamii ambaye ameweza na kufanikisha mengi haya ni baadhi ya mambo yaliyomsukuma Rafat kuandika kitabu hiki ambacho kimebeba masuala mbalimbali yenye tija kwa jamii na Taifa kwa ujumla.....Ninaahidi kushirikiana katika kuendeleza mawazo haya na nitamkabidhi Rais wetu nakala ya kitabu cha 'The First Female President'." Amesema

Aidha amesema kuwa dhamira ya kitabu hicho ni kutoa hamasa kwa watoto na vijana kubadili changamoto kuwa fursa pamoja na kuondokana na mila potofu.

"Niwatake wazazi na walezi kuwaandaa mapema watoto wetu ili wawe tayari kuwajibika kwa kukuza uchumi binafsi na uchumi wa taifa....tuwape elimu, kutambua na kuendeleza vipaji vyao pamoja na kushirikishwa kazi na majukumu ya nyumbani " Amesema.

Komrade Rehema amewapongeza wazazi wa Rafat kwa kuwekeza muda, Fedha na ujuzi kwa binti yao na kuwahimiza wazazi kuwa wasimamizi bora kwa watoto pamoja na kubaini vipaji vyao na kuviendeleza hali itakayosaidia kupunguza changamoto ya ajira na kuwa na kizazi chenye maadili.


Rafat Simba, mwandishi wa kitabu hicho amesema alipenda kusoma na kuandika tangu alipokuwa na miaka mitatu na ameendelea kushiriki mashindano mbalimbali ya kusoma pamoja na kujiunga na klabu ya usomaji ya Mwangaza.

"Katika kuandika kitabu hiki Cha The First Female President nilihamasika na jitihada, ustahimilivu na umakini wa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akiwa Rais mwanamke wa kwanza aliyebeba maono ya taifa.

Rafat amesema, kitabu hicho cha kufikirika (fiction,) kitabadilisha mawazo ya wengi na kimebeba dhamira mbalimbali ikiwemo kujiamini, kujiongoza na kujenga tabia ya kujisomea katika kufikia malengo.

Kwa upande wa baba mzazi wa Rafat, Dr. Ally Simba ameeleza safari ya ubunifu wa Rafat tangu alipokuwa mdogo;

"Kama wazazi tumefurahi kwa hatua na dhamira aliyoonesha Rafat katika kufuata ndoto zake kwa kuandika kitabu chake cha kwanza, tunasherekea uzinduzi pamoja na kushiriki hisia zake kupitia andiko hili kama mwandishi mchanga anayepambana." Amesema.

Amesema, wamekuwa wakufuatilia katika uandishi wa kitabu hicho chenye taswira halisi ndani yake na wamekuwa wakimpa moyo katika safari yake ya uandishi.

Pia amewashauri wazazi kutenga muda kwaajili ya watoto wao na kuwapa moyo katika ndoto zao wanazozipigania kwa manufaa ya Taifa kwa kutengeneza vijana wabunifu, wapenda maendeleo na wenye kujiamini na nidhamu.

Pia mkufunzi wa masuala ya watoto na mwanzilishi wa Taasisi ya Mwanga Mpya Academy, Justine Kakoko amesema, kitabu hicho kimesheheni misingi ya lugha na matumizi sahihi ya lugha na kimechukuwa takribani mwaka mmoja hadi kukamilika kwake.

Kakoko amewapongeza wazazi wa Rafat kwa kuunga mkono jitihada za binti yao kwa kuweka kipaumbele kwa kuendeleza kipaji chake cha uandishi na wao kama taasisi wamekuwa bega kwa bega kimawazo,ujuzi ili kufanikisha ndoto za Rafat.

Aidha amewashauri wazazi kuzingatia kuwa kila 'Kila mtoto ana uwezo ndani yake unaosubiri kuendeleza.' kwa kukuza, kusimamia na kuendeleza uwezo wa watoto kwa misingi ya kuwapatia elimu rasmi na elimu binafsi, kutengeneza mazingira ya kuchochea kubaini kilichopo ndani ya mtoto na kukiendeleza pamoja na kujenga mahusiano ya kuwa karibu na watoto ili kuwakinga na ombwe la mabadiliko ya teknolojia.

Hafla ya uzinduzi huo ulikwenda sambamba na utolewaji wa mada mbalimbali za Afya ya akili kwa familia, namna ya kuibua na kuendeleza vipaji kwa watoto pamoja na matumizi salama ya mitandao kwa watoto.


Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM,) Komred Rehema Omary akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitabu cha 'The First Female President' na kupongeza jitihada za Rafat na wazazi wake kwa kuhakikisha ndoto za binti yao zinatimia na kuwataka wazazi kuwekeza muda kwa watoto pamoja na kuendeleza vipaji vyao. Leo jijini Dar es Salaam.
Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM,) Komred Rehema Omary akiwa ameambatana na mwandishi wa kitabu Rafat Simba na wazazi wake wakizindua rasmi kitabu cha 'The First Female President' Leo jijini Dar es Salaam.
Mwanzilishi wa Taasisi ya Mwanga Mpya Academy na mkufunzi wa masula ya watoto Justine Kakoko (kulia,) akiwa na mwandishi wa kitabu hicho Rafat Simba mara baada ya uzinduzi wa kitabu hicho, awali Kakoko alieleza kuwa imechukua mwaka mmoja hadi kukamilika kwake na ni mahususi kwa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan. Leo jijini Dar es Salaam.

Matukio mbalimbali wakati wa uzinduzi wa kitabu cha 'The First Female President' jijini Dar es Salaam.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...