Na Mwandishi Wetu

BARAZA la Ushindani wa Biashara (FCT) limetoa uamuzi kuhusu uamuzi wa Tume ya Ushindani (FCC) wa kuruhusu kampuni ya Scancem International DA inayomiliki kampuni ya Saruji ya Twiga kununua hisa za Kampuni ya Saruji ya Tanga kupitia uamuzi wake ulioutoa Februari 28, mwaka huu.

Uamuzi huo umefanyika baada ya ule wa awali kukatazwa na FCT Septemba, 2022 baada ya kufunguliwa kwa shauri na baadhi ya wadau kuwa uuzaji wa hisa hizo ambao ungesababisha muunganoko kati ya Twiga Cement na Tanga Cement ungesababisha athari za kibiashara.

Miongoni mwa athari zilizowasilishwa mbele ya baraza hilo na wadau hao ni kuwapo kwa ukiritimba katika soko kutokana na mzalishaji mmoja kuwa na asilimia nyingi na kuwapo kwa uwezekano wa kupanga bei ya bidhaa, hivyo kuathiri watumiaji.

Pamoja na kuwapo kwa katazo la muunganiiko huo, FCC ilitangaza tena kuwa muunganiko huo baina ya kampuni hizo mbili unarejewa na kukaribisha wadau kutoa maoni, jambo ambalo lilisababisha baadhi ya wadau kutaka jambo hilo lizuiwe kisheria na kwamba linakiuka sheria na uamuzi uliotolewa na FCT ambacho ni chombo cha juu katika utatuzui wa migogoro ya kibiashara.

Kutokana na hali hiyo, kampuni ya Saruji ya Chalinze ilikata rufani FCT kupinga uamuzi wa FCC kuruhusu muunganoko huo na baraza hilo limetoa uamuzi unaozuia kuendelea kwa muunganiko huo huku likisisitiza kwamba umezuiwa kisheria.

Katika hoja zake za rufani, mrufani amedai kuwa FCC ilikosea kisheria kwa kuruhusu muunganiko ambao ulikatazwa na FCT katika uamuzi wake uliotolewa Septemba 23, 2022.

Pia FCC inadaiwa ilikosea kisheria kwa kuitisha upya mchakato wa muunganiko wakati shauri hilo lilishatolewa uamuzi.

Hoja nyigine katika rufani hiyo ni kwamba FCC ilikiuka sheria kwa kudai kuwa katazo la FCT halizuii moja kwa moja, hivyo si la kudumu kwa kuzuia muungano wa kampuni
hizo.

Hata hivyo, mjibu rufani namba moja, FCC na Wakili Mkuu wa Serikali ambaye ni mjibu rufani namba mbili, waliibua hoja kuwa mchakato wa Februari, 2023 ulifanyika baada ya kufanya upembuzi yakinifu wa kisoko kuwa hakuna madhara yanayoweza kujitokeza.

Pamoja na hoja hiyo, FCT katika uamuzi wake imesema FCC ilifanya uchunguzi na kutoa ripoti inayoonesha dhahiri kwamba muunganiko unaokusudiwa unaweza kuwa na
athari katika ushindani.

“Baada ya kujiridhisha kuwapo kwa athari za kiushindani na uchumi kama muunganiko huu utapata kibali, mjibu rufani namba moja aliendelea na mchakato ...

"Baada ya kufanya tathmini na kuangalia uzito wa hoja, Baraza (FCT) limeridhika kuwa kama muunganiko huu utapitishwa bila masharti yoyote, kuna uwezekano wa kuathiri watumiaji wa bidhaa, hivyo muunganoko huo umezuiwa,” imeeleza hukumu hiyo.

Jaji Maghimbi pia amesema pamoja na kukubaliana na hilo kuna uwezekano wa kubadilika kwa nguvu za soko, haridhiki na muda mfupi uliotolewa katika kurekewa kwa mchakato.

Hivyo amesema haridhiki na mabadiliko hayo ambayo yangelifanya Baraza kurejea uamuzi wake wa awali kuhusu muunganiko huo.

Aidha, Jaji Maghimbi katika uamuzi huo, alieleza kushangazwa na FCC ambayo
imepewa jukumu la kusimamia ushindani kwenye masuala ya kiuchumi kwa maslahi ya watumiaji wa bidhaa, kudharau nguvu za kisheria za Baraza kwa kuendelea na mchakato ambao ulizuiwa kisheria.

Jaji Maghimbi amesisitiza kitendo kilichofanywa na wajibu rufani hakikuakisi ujumbe chanya kwa umma na kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika nchi yetu kwa
kuitisha upya mchakato katika jambo lililokuwa limezuiwa.

"Jambo hilo limefanywa kinyume dhidi ya uwapo wa utawala wa sheria.Sababu kubwa inayowafanya wawekezaji kuona nchi yetu ni ‘paradiso’ katika uwekezaji ni uwapo wa utawala wa sheria, kuheshimu sheria, kutokuwapo upendeleo na usawa mbele ya sheria.

" Hili halina budi kuheshimiwa kwa namna yoyote pasipo kumpendelea mwekezaji mmoja kwa sababu inaweza kusababisha madhara hasi.Kutokana na sababu zilizotatwa awali, nabatilisha uamuzi wa mjibu rufani namba moja kuhusu muunganiko wa Februari 28, 2023,” amesisitiza.

Jaji Maghimbi ameionya FCC kwamba FCT ni chombo cha juu ni chombo cha juu katika kusimamisha sheria na kutatua migogoro inayojitokeza kibiashara, hivyo inapaswa kuheshimu uamuzi wa awali wa Septemba 2022 ambao ulikataza muunganiko huo.

Pia Jaji Maghimbi katika hukumu hiyo
alimuuliza Wakili Mkuu wa Serikali kama kuanzisha mchakato mpya wa Februari 2023 wakati kuna hukumu ya Septemba 2022 kama ilikuwa njia sahihi na alikiri kuwa haikuwa sahihi kufanya hivyo.

Aidha, katika uamuzi huo, Jaji ametoa amri FCC iombe marejeo ndani ya siku 30 tangu Julai 6, mwaka huu kama inataka kuanzisha mchakato mpya kitu ambacho mpaka sasa hakijagfanyika na muda umemalizika.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...