Na. Jacob Kasiri - Mbeya
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) amesema kuwa Utalii ukishamiri sekta ya kilimo na mifugo italeta tija kwa taifa, hivyo uwepo wa TANAPA katika Maonesho ya Nanenane unaongeza thamani ya maonesho hayo.
Ameyasema hayo leo tarehe 03.08.2023 alipotembelea banda la TANAPA lilipo ndani ya Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii wanaoshiriki Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima (Nanenane) katika Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.
Akiwa katika banda la TANAPA, Majaliwa alisema "utalii ukishamiri sekta ya kilimo italeta tija, nyama zitapatikana na kuliwa na watalii, hivyo ushiriki wenu katika maonesho haya unaongeza thamani kubwa sana katika kukuza uchumi."
Aidha, Mhe. Majaliwa alisema kuwa jambo kubwa analolisisitiza kwa TANAPA ni kuvitangaza vivutio vya utalii kupitia vyombo vya habari. Hata hivi alivitaka vyombo
hivyo vya habari kueleza kwa wananchi shughuli zinazofanywa na TANAPA na kuvitangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana katika hifadhi za taifa.
Katika kuongeza idadi ya watalii nchini Mhe. Majaliwa alisema "juzi niliongea na Balozi wa Urusi kuwa wanataka kuleta ndege, hivyo wanamalizia makubaliano kati ya Tanzania na Urusi na yakishakamilika ndege za watalii kutoka Urusi zitaanza kuleta watalii, niwatake TANAPA kuongeza kasi ya miundombinu na kujitangaza zaidi ili wageni hawa wakianza kuja iwakute sehemu sahihi zaidi".
Hata hivyo, aliipongeza Menejimenti ya TANAPA kwa kazi nzuri ya ulinzi wa maliasili hizi, Mhe. Majaliwa alisema, "niwape hongera Menejimenti yenu, pia niendelee kuwatia moyo kwa kazi mnayofanya, tangazeni vivutio vinavyotangazwa na wengine kuwa vya kwao, si mnajua ee! tangazeni kuwa ni vya kwetu".
"Mabalozi wanahitaji hizi "copy" za vipeperushi, fungasheni na mpeleke maeneo kama vile Israel na maeneo mengine ya kitalii tunayopata watalii wengi" alisisitiza Mhe. Majaliwa.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi - TANAPA, Theodora Aloyce akimkaribisha Mhe. Waziri Mkuu alisema "shughuli za uhifadhi wa vyanzo vya maji vinavyopatikana katika hifadhi za taifa husaidia katika kilimo, ufugaji, uvuvi na uzalishaji wa umeme. Hivyo ni wajibu wa TANAPA kuvilinda kwa manufaa ya taifa".
TANAPA ni miongoni wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii wanaoshiriki Maonesho ya Kimataifa ya kilimo (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...