NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, MBEYA

MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), CPA. Hosea Kashimba, amesema utaratibu wa pensheni lengo lake ni kumsaida mtumishi wa umma atakapostaafu.

CPA. Kashimba ameyasema hayo kwenye banda la Wizara ya Fedha wakati akiongoza timu ya watumishi wa Mfuko huo kutembelea Wanachama chini ya kampeni ya “Banda kwa Banda” yenye lengo la kuwafikia na kuwapa elimu ya Mfuko wanachama huko waliko katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo maarufu Nanenane kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya Agosti 7, 2023.

Maonesho hayo yenye kauli mbiu “Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula”, yaliyofunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muunganowa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango Agosti Mosi, 2023, kilele chake Agosti 8, 2023 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndiye mgeni rasmi.

Katika kampeni ya banda kwa banda, CPA. Kashimba alifuatana na Meneja wa PSSSF Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bw. Ramadhani Mgaya, Afisa Uhusiano Mkuu, Bw. Abdul Njaidi na Afisa Uhusiano Mwandamizi, Bi. Coleta Mnyamani, alisema, utaratibu wa pensheni ni mfumo ambao haukujengwa kutoa fedha wakati wowote bali umejengwa kutengeneza mfuko wa pamoja wa kumuwezesha mfanyakazi pale anapostaafu awe analipwa pensheni mpaka atakapofariki.

“Tukumbuke kwamba huyu mtu amefanya kazi akiwa analipwa mshahara na mwajiri wake siku akiondoka kazini anaishije? ndipo mifuko ya pensheni ikiwemo PSSSF inaingia hapo kujibu tatizo hilo,” alisema

Alisema sasa hivi umri wa kuishi umeongezeka, na kutolea mfano wa mmoja wa wanachama wa PSSSF ambaye sasa anakaribia kufikisha umri wa miaka 100 na anaednelea kufaidika na pensheni.

Akizungumzia umuhimu wa Hifadhi ya Jamii, CPA. Kashimba alisema, “Sio kila mstaafu ana uwezo wa kufanya biashara, hasa kwa mfumo tuliolelewa wa kuishi kwa kutegemea mshahara wa kila mwezi, hivyo pensheni ya kila mwezi inamfanya mstaafu asione tofauti ya kipato. Pensheni ya mwezi inamfanya aishi kama yuko ofisini na anaendelea kuihudumia familia yake.”

Akitoa maoni yake kuhusu huduma za PSSSF, Mkurugenzi wa Usimamizi Rasilimali Watu na Utawala Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Kened Nyoni alisema BoT imekuwa na ushirikiano mzuri na PSSSF.

“PSSSF inafanya kazi vizuri na kwa kweli tumekuwa tukishirikiana kwa karibu sana.” Alisema Bw. Nyoni.

Mabanda aliyotembelea ni pamoja na banda la Wizara ya Fedha ambalo linajumuisha taasisi zote zilizo chini yake, banda la Azania Bank, banda la Hospitali ya Benjamin Mkapa, banda la Benki Kuu ya Tanzania (BoT), banda la Chuo Kikuu ha Dar es Salaam, banda la Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), na banda la NSSF.

Akizungumzia sababu za kampeni hiyo, Afisa Uhusiano Mkuu Bw. Abdul Njaidi alisema, “Kama unavyojua wanachama wetu ni watumishi wote wa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na walio katika Mashirika ambayo Serikali ina umiliki wa zaidi ya asilimia 30% wote hawa wapo katika viwanja hivi kwa nia ya kuwahudumia wananchi, kwa wale ambao hawatakuwa na fursa ya kufika katika banda letu, tunao utaratibu wa kuwatembelea. na kuwasikiliza lakini pia kutoa elimu.”

Naye Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bw. Ramadhani Mgaya, alisema katika kipindi chote cha Maonesho, PSSSF imekuwa ikitoa huduma kama zile zinazotolewa kwenye ofisi za Mfuko zinazopatikana nchi nzima.

Alisema Mwanachama akifika anaweza kupata taarifa za michango yake, taarifa kuhusu fursa za uwekezaji, wastaafu wanaweza kuhakiki taarifa zao na taarifa kuhusu mafao yatolewayo na Mfuko.

“Sambamba na hilo tumekuwa tukiwaelimisha wanachama kuhusu namna Mfuko ulivyoboresha huduma zake ikiwemo matumizi ya TEHAMA, mwanachama anaweza kupata huduma zote kupitia PSSSF Kiganjani.” Alifafanua Bw.

Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba (aliyeketi katikati) na Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wa Mfuko huo, Bw. Ramadhani Mgaya (wakwanza kulia) wakisikiliza maoni ya Meneja wa Tawi la Benki ya Azania jijini Mbeya, Bw. Mahimbi (kushoto) kuhusu huduma za Mfuko wakati wa kampeni ya PSSSF kuwatembelea wanachama wake ya banda kwa banda 
 
Mwanachama wa PSSSF akisoma mungozo wa mwanachama kuhsuu Mfuko huo
CPA. Kashimba (katikati), Bw. Mgaya (kushoto) na Bw. Njaidi wakielekea kwenye mabanda yenye wanachama wa  PSSSF kwa nia ya kuwafikia ili kupata maoni yao na kuwaelimisha kuhusu huduma zitolewazo na Mfuko.
CPA. Kashimba (wapili kulia) akisindikizwa na Mkurugenzi wa Usimamizi Rasilimali Watu na Utawala, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Kened Nyoni (wapili kushoto), Mkurugenzi wa Bodi ya Bima ya Amana, Bw. Isack Kijwili (kulia) na Meneja Msaidizi Idara ya Mwasiliano, Bi. Noves Moses mara baada ya kutembelea banda la BoT.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), CPA. Hosea Kashimba (kushoto) akimuhudumia Bi. Rehema Kapange (kulia), mnufaika wa  Mfuko. Katikati anayeshuhudia ni Afisa Uhusiano Mkuu, Bw. Abdul Njaidi.
Bi. Irene Museti (kushoto) Afisa Mwandamizi PSSSF, akimuhudumia Mwanachama aliyefika kupata taarifa ya michango yake
CPA. Kashimba akimpatia zawadi ya pakiti ya tangawizi ambayo inazalishwa na kiwanda cha kuchakata Tangawizi cha Mamba Ginger Growers ambacho PSSSF imewekeza na hivyo kuwawezesha wakulima wa Tangawizi walioko wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro na maeneo jirani kupata sehemu ya kuuza zao hilo. 



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...