Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi amezindua ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kizimkazi kilichopo Mkoa wa Kusini Unguja kinachojengwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ikiwa ni jitihada za wadau hao wawili katika kuimarisha huduma za afya kwa wananchi.

Hafla ya uzinduzi huo imefanyika mwishoni mwa wiki ikihusisha uwekaji wa jiwe la msingi eneo unapotekelezwa mradi huo ikiwa pia ni sehemu ya uzinduzi wa Tamasha la Kizimkazi 2023 hafla ambayo ilihudhuriwa na viongozi waandamizi kutoka serikalini akiwemo Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Hassan Hafidh, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Rashid Hadidi, viongozi waandamizi wa benki ya NBC wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Theobald Sabi pamoja na wakazi wa eneo hilo.

Akizungumzia mradi huo wenye thamani ya sh bilioni 4.4 ambapo benki ya NBC imechangia kiasi cha Sh milioni 400, Rais Mwinyi pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa hatua hiyo muhimu, alisema huo ni adhma ya serikali hiyo kuboresha huduma ya afya kwa kujenga vituo vya afya vyenye hadhi ya kipekee katika baadhi ya maeneo kulingana na uhitaji mkubwa wa huduma hiyo katika maeneo hayo huku akiyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na eneo la Tumbatu, Fuoni na Kizimkazi.

‘’Kimsingi kwasasa ujenzi wa miundombinu kwenye sekta ya afya ndio kipaumbele chetu, jitihada ambazo zitafuatiwa kwa ukaribu sana na upatikanaji wa wataalamu wa afya pamoja na vifaa tiba. Kituo hiki cha Kizimkazi ni moja ya vituo vitatu vya afya vinavyojengwa katika mpango wa ujenzi wa vituo vyenye hadhi maalum hapa Zanzibar.’’

‘’Kipekee sana niwashukuru wadau wa maendeleo ikiwemo benki ya NBC kwa kutuunga mkono kwenye hili na ni matumani yangu kwamba msimu ujao wa Kizimkazi Festival tutazindua kituo hiki kikiwa kimekamilika,’’ alisema.

Akizungumzia mradi huo, Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Hassan Hafidh alisema kukamilika kwa kituo hicho kutawezesha utoaji wa huduma kwa wagonjwa takribani elfu nane kwa wakati mmoja huku akibainisha kuwa kituo hicho kitahusisha huduma za kliniki, huduma za kujifungua, vipimo vya maabara, huduma za meno, uchunguzi wa X-ray na ultrasound.

‘’Pamoja na kuboresha afya ya jamii kwa ujumla, kituo hiki kitawasaidia sana hasa wakina mama hususani wakati wa kujifungua, wagonjwa wa nje na wagonjwa wanaohitaji huduma ya kulazwa.’’ Alitaja.

Awali akizungumza kwenye hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Theobald Sabi alisema mradi huo ni sehemu ya muendelezo wa mkakati wa benki ya NBC kushirikiana na serikali katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii ikiwemo changamoto ya afya.

‘’Tunaamini kwamba kuwa kituo hiki kitatoa huduma bora za afya kwa wanawake na watoto wa Kizimkazi na maeneo jirani. Aidha kupitia ushirikiano wetu na Taasisi ya AMREF tumefanikiwa kuimarisha afya ya uzazi kwa wakina mama.Tumesaidia kuongeza upatikanaji wa vifaa tiba katika hospitali mbalimbali visiwani Zanzibar hasa kwa ajili ya matibabu wakati wa kujifungua kwa wanawake.’’ Alibainisha

Kwa mujibu wa Sabi, pamoja na ujenzi wa kituo hicho cha afya, benki hiyo imekuwa ikishiriki katika miradi mbalimbali ya maendeleo katika eneo hilo ikiwemo ujenzi wa madarasa ya chekechea, ununuzi samani za ofisi kwenye Saccos ya wakazi wa eneo hilo na mwaka 2021 benki hiyo ilianzisha mradi wa Mobile Clinic (Kliniki Inayotembea) ambapo kupitia mradi huo imeweza kutoa huduma za afya kwa wanawake wajawazito zaidi ya 4,000.

Jitihada za benki hiyo kwenye sekta ya afya zinakuja siku chache tu baada ya kufanyika kwa mbio za NBC Dodoma Marathon, ambapo hadi sasa zimefanikiwa kukusanya zaidi ya TZS milioni 500 kwa ajili ya kutoa elimu na kupambana na saratani ya shingo ya kizazi inayoongoza kwa vifo kwa wanawake sambamba na kufadhiri masomo ya wakunga ili kuokoa maisha ya wakina mama na watoto wakati wa kujifungua.

Mbali na kuzindua kituo hicho, Rais Mwinyi pia alipata wasaa wa kutembelea banda la maonesho la benki hiyo lililopo kwenye viwanja vya Paje vilivyopo Wilaya ya Kusini Mkoa wa Kusini Unguja sehemu ambapo uzinduzi wa Tamasha la Kizimkazi ulipofanyika .
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akitazama jiwe la msingi mara baada kuzindua mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya cha Kizimkazi kilichopo Mkoa wa Kusini Unguja kinachojengwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa ujenzi wa kituo hicho uliofanywa na Rais Mwinyi mwishoni mwa wiki ikiwa pia ni sehemu ya uzinduzi wa Tamasha la Kizimkazi 2023. Wengine ni pamoja na Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Hassan Hafidh (wa kwanza kushoto), Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi (wa kwanza kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya NBC Theobald Sabi (wa pili kushoto).


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (wa tatu kulia) akimsikiliza Mhandisi wa mradi Mhandisi Fatma Kara (alieshika kipaza sauti) wakati akitoa ufafanuzi kuhusu mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya cha Kizimkazi kilichopo Mkoa wa Kusini Unguja kinachojengwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa ujenzi wa kituo hicho uliofanywa na Rais Mwinyi mwishoni mwa wiki ikiwa ikiwa pia ni sehemu ya uzinduzi wa Tamasha la Kizimkazi 2023. Wengine ni pamoja na Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Hassan Hafidh (wa nne kulia) Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi (wa pili kulia), Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Rashid Hadidi (wa kwanza kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya NBC Theobald Sabi (katikati)

Muonekano wa mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya cha Kizimkazi unaotekelezwa kwa ushirikiano wa serikali kwa kushirikiana na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC).

Sehemu ya wakazi wa Kizimkazi wakifuatilia uzinduzi huo.

Meneja wa Biashara wa NBC Obeid Ngavatula akimuelezea huduma zinazotolewa na Benki ya NBC, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi alipotembelea banda la benki ya NBC kwenye Uzinduzi wa Tamasha la Kizimkazi 2023 uliofanyika mwishoni mwa wiki Paje, Mkoa wa Kusini, Unguja.Karibu tukuhudumie

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (katikati walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau mbalimbali wa tamasha la Kizimkazi 2023 ikiwemo Benki ya Taifa ya Biashara NBC wakati wa uzinduzi wa tamasha la Kizimkazi 2023 uliofanyika mwishoni mwa wiki Paje, Mkoa wa Kusini, Unguja.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...