Na Munir Shemweta, ARUMERU
Serikali imesikiliza kilio cha waliokuwa wafanyakazi katika shamba la Tanzania Plantation lilipo wilaya za Arusha na Arumeru mkoa wa Arusha kwa kuwapatia maeneo kwa ajili ya kujenga makazi, kilimo pamoja na ufugaji.
"Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kusikia kilio cha muda mrefu cha waliokuwa wafanyakazi wa Tanzania plantation Ltd ameridhia wananchi 102 wawe kipaumbele cha kwanza katika kupewa ardhi" alisema Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula.
Akizungumza na wananchi wa kitongoji cha Lucy eneo la Bwawani wilayani Arumeru mkaoni Arusha tarehe 2 Agosti 2023 Dkt Mabula alisema, kutokana na uamunifu waliokuwa nao wananchi hao kwa muda mrefu katika eneo hilo kwa kuendelea kutunza mashamba hata pale wawekezaji walipotetereka serikali inakwenda kuwapatia maeneo ya kujenga nyumba zao za makazi na kumilikishwa kisheria.
Aidha, aliongeza kwa kusema kuwa, kama hiyo haitoshi Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutambua kuwa wananchi hao bado ni wakulima na wana nguvu za kufanya shughuli za kilimo, ameelekeza pamoja na kupatiwa eneo la ujenzi wa nyumba wapatiwe pia walau ekari mbili kwa ajili ya shughuli za kilimo.
Waziri Mabula alibainisha kuwa, katika eneo hilo la shamba la Tanzania Plantation Ltd wapo wananchi 486 waliovamia mashamba kwenye eneo hilo ambapo aliweka bayana kuwa, pamoja na ukiukwaji wa taratibu uliofanywa na wananchi hao Rais ameelekeza wazingatiwe katika kupatiwa maeneo kwa kufuata taratibu.
‘’Pia wapo wasamaria wema 27 waliojitolea maeneo yao kwa serikali ili kujengwa shule na zahanati ambapo nao imeelekezwa kuingizwa katika utaratibu wa kupatiwa maeneo’’. Alisema Dkt Mabula
Akifafanua zaidi, Dkt Mabula alisema kwa kuzingatia uwezo wa kiuchumi wa wananchi hao, serikali imeamua kuwapatia maeneo ya makazi kwa gharama ya shilingi 601 kwa mita moja ya mraba huku mashamba yakitolewa kwa shilingi milioni 2.5 kwa ekari moja.
Serikali ilikabidhiwa mashamba yaliyokuwa yakimilikiwa na Kampuni ya Tanzania Plantations Ltd baada ya kukamilisha taratibu za kutwaa mashamba hayo.
Makabidhiano ya mashamba hayo yaliyokuwa yakijulikana kama Karangai na Lucy Estate yalihitimisha mgogoro uliodumu kwa muda mrefu baina ya serikali na Kampuni ya Tanzania Plantations Ltd sambamba na ule wa wananchi na Kampuni hiyo kutokana na wananchi kuuziwa baadhi ya maeneo katika mashamba yaliyobatilishwa.
Mgogoro kati ya Tanzania Plantations Ltd na Serikali uliibuka mwaka 1999 baada ya kampuni hiyo kupinga ubatilisho wa mashamba yake uliofanywa na serikali kwa kushindwa kutimiza masharti ya umiliki jambo lililoifanya kampuni hiyo kufungua kesi Mahakama Kuu Arusha mwaka 2015.
Hata hivyo, katika kutafuta suluhu nje ya Mahakama Serikali kupitia Wakili Mkuu wa Serikali Mei 15, 2019 aliwasilisha ombi la majadiliano na mdai kwa lengo la kumaliza shauri nje ya mahakama ambapo Mahakama iliridhia pande mbili za shauri kumaliza suala hilo nje ya mahakama na ndipo Serikali ilikubali kulipa shilingi bilioni 5.7 kwa ajili ya fidia ya mashamba.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza katika mkutano wa wananchi wa kitongoji cha Lucy eneo la Bwawani wilayani Arumeru tarehe 2 Agosti 2023 mkoani Arusha.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiingia katika kiwanda cha kuchakata mkonge alipotembelea eneo la shamba la Tanzania Plantantion wilayani Arumeru mkoa wa Arusha tarehe 2 Agosti 2023. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiangalia mashine ya kuchakata mkonge alipotembelea eneo la shamba la Tanzania Plantantion wilayani Arumeru mkoa wa Arusha tarehe 2 Agosti 2023.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiangalia mazingira ya kiwanda cha kuchakata mkonge alipotembelea eneo la shamba la Tanzania Plantantion wilayani Arumeru mkoa wa Arusha tarehe 2 Agosti 2023.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiangalia mtambo wa kuchakata mkonge alipotembelea eneo la shamba la Tanzania Plantantion wilayani Arumeru mkoa wa Arusha tarehe 2 Agosti 2023.
Mbunge wa jimbo la Arumeru Magharibi Noah Lemburis Saputu akizungumza katika mkutano wa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula na wananchi wa Bwawani wilayani Arumeru mkoa wa Arusha tarehe 2 Agosti 2023.
Mkuu wa wilaya ya Arumeru mkoa wa Arusha Emmanuela Mtafikolo Kaganda akizungumza katika mkutano wa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula na wananchi wa Bwawani wilaya ya Arumeru mkoa wa Arusha tarehe 2 Agosti 2023.
Baadhi ya akina mama wa kitongoji cha Lucy wilayani Arumeru mkoa wa Arusha wakifuatilia maelezo ya Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (hayupo pichani) alipokwenda kutoa majibu ya kilio chao cha kupatiwa maeneo katika eneo la Shamba la Tanzania Plantantion ltd.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...