Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Saidi Mfaume, miaka 32, Mtaalam wa Technolojia ya Mawasiliano (IT), mkazi wa Arusha kwa kosa la kumjeruhi mpenzi wake kwa kumchoma na kisu sehemu mbalimbali za mwili wake kisha na yeye kujaribu kujiua kwa kujichoma na kisu tumboni baada ya kuamini amemuua mpenzi wake.

Tukio hilo lilitokea tarehe 06.08.2023 muda wa saa mbili asubuhi katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Citizen Lodge iliyopo eneo la Pasiansi Wilayani Ilemela ambapo Faudhia Juma, miaka 24, mfanyabiashara, mkazi wa Singida akiwa na mpenzi wake katika nyumba hiyo alichomwa na kisu sehemu mbalimbali za mwili wake na Saidi Mfaume baada ya kuzuka ugomvi uliotokana na Faudhia kukataa kuolewa naye.

Kwamba hapo awali Saidi Mfaume alikuwa na mawasiliano na mama mzazi wa Faudhia Juma aitwaye Mwanahamisi Juma, miaka 49, mkazi wa singida ambapo alishatoa posa kwa ajili ya kumuoa mwanae. Hata hivyo, Faudhia hakuwa ameridhia kuolewa na Saidi. Hivyo alitoweka hapo nyumbani na kwenda kutafuta kazi ili kujikimu kimaisha kitendo ambacho hakikumfurahisha kijana huyo hivyo aliamua kutumia taaluma yake ya IT na kuanza kumfuatilia huyo mchumba wake mahali alipokuwa.

Faudhia Juma amepatiwa matibabu katika hospitali ya Mkoa Sekou Toure na kuruhusiwa kurudi nyumbani na mtuhumiwa anaendelea na matibabu akiwa chini ya ulinzi katika hospitali hiyohiyo hali yake kiafya inaendelea vizuri na atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawakumbusha wananchi kuwa kujichukulia sheria mkononi haijawahi kuwa njia sahihi katika kuondoa na kumaliza changamoto za kimahusiano ya kimapenzi kati ya mwanamke na mwanaume bali kukaa pamoja na kukubaliana au kuelewana ndio njia sahihi. Mapenzi hayalazimishwi bali ni jambo la hiari hivyo inapotokea mtu mmoja amekataliwa anashauriwa kuwa mpole na kutafuta mwenza mwingine kwani watu wapo wengi tu. Pia, tunawaomba wananchi waendelee kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili ziweze kufanyiwa kazi.

Katika tukio lingile, Jeshi la polisi mkoa wa Mwanza limewakamata watuhumiwa 12 wakiwa na simu 309 na vifaa mbalimbali vya simu zidhaniwazo kuwa mali za wizi wakiwemo mafundi simu wawili ambao wamekutwa na vifaa mbalimbali vya ufundi pamoja na simu zidhaniwazo kuwa mali ya wizi.

Watuhumiwa pamoja na mali hizo wamekamatwa kufuatia oparesheni maalumu iliyofanyika tarehe 10.08.2023 majira ya saa 12:30 mchana hadi saa 15:15 alasiri mtaa wa Lumumba, wilaya ya Nyamagana baada ya Jeshi la Polisi kupata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa kuna baadhi ya mafundi simu wanashirikiana na wezi wa simu kubadilisha vifaa vya simu za mkononi zilizoibiwa na kuziuza kwa baadhi ya wafanyabiashara wa simu.

Aidha, watuhumiwa hao wamekamatwa wakiwa na vifaa pamoja na simu mbalimbali zilizotumika bila kuwa na nyaraka muhimu zinazoonesha uingizwaji wa simu hizo. Hata hivyo, Jeshi la polisi tumebaini watuhumiwa hao ni wapokeaji wa simu na vifaa vilivyotumika na baadhi ya leseni za biashara zao zinaonesha wanatakiwa kuuza vifaa vya simu na sio simu kama wao wanavyouza.

Mafundi simu wanaoshikiliwa ni Mussa Ayoub, miaka 29, mkazi wa Kitangili na Patrick Herman, miaka 24, mkazi wa Iseni ambao wamekamatwa na simu pamoja na vifaa mbalimbali wanavyobadirisha kutoka kwenye simu za wizi wanazopokea kutoka kwa wezi wa simu za mkononi na kuuza kwa wateja wao.

Watuhumiwa wengine waliokamatwa na simu ni;- 1. Meckrida Samwel, miaka29, mkazi wa Nyegezi, Mfanyabiashara, Amekamatwa na simu 28, 2. Eled Bwire, miaka 33, mkazi wa kangaye, Mfanyabiashara, Amekamatwa na simu 12, 3. Ally Abdullah, miaka 23, fundi simu, mkazi wa ksimru. Amekamatwa na simu 5, 4. Chacha maliba, miaka 40, makazi Buhongwa, Mfanyabiashara. Amekamatwa na simu 72. 5. Jonathan Benard, miaka 23, biashara na makazi buhongwa. Amekamatwa na simu 6, 6. Robert Rongino, Miaka 33, mkazi Mahina biashara. Amekamatwa na simu, 39, 7. Evadius

Benard, Miaka 28, mkazi Kiloleli biashara. Amekamatwa na simu 16, 8. Edson Kaponko, miaka 45, mkazi Isamilo, mfanyabiashara. Amekamatwa na simu

37, 9.Mgodi Mtundu, miaka 35, mkazi wa Igoma, mfanyabiashara, Amekamatwa na simu 78 10. Mussa Omary, miaka 55, mkazi wa Ibungilo, amekutwa na simu 07 11. Liberty Coasta, miaka 50, mkazi wa Nyamanoro amekamatwa na simu aina mbalimbali 16 . Watuhumiwa wote wamehojiwa kwa kina na watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili ziweze kufanyiwa kazi kwa haraka. Aidha, linawakumbusha wananchi kufuata njia sahihi za ununuzi wa simu kwa kwenda kwenye maduka rasmi yanayouza simu pamoja na vifaa vyake na siyo vinginevyo.

Vilevile, Jeshi la Mkoa wa Mwanza linawashikilia watu 50 kwa kosa la kufanya fujo kwa kupanga mawe barabarani, kuharibu mali na kujeruhi abiria waliokuwa wakisafiri katika barabara ya Mwanza-Musoma baada ya kutokea kwa ajali iliyowagonga wanafunzi wawili na kusababisha kifo na majeruhi.

Ajali hiyo ilitokea tarehe 11.08.2023, majira ya saa 07:30 mchana huko katika mtaa wa Nyalikungu “A”, kata ya Magu mjini, wilaya ya Magu na mkoa wa Mwanza katika barabara ya kutoka Mwanza kwenda Musoma iliyo husisha gari yenye namba ya usajili T.121 DCU aina ya Toyota Hiace inayomilikiwa na Boniphace Joseph, mkazi wa Buhongwa, Mwanza iliyokuwa inatoka Magu kuelekea Mwanza.

Gari hilo lilipofika mtaa wa Nyalikungu ‘A’ iliwagonga watoto wawili watembea kwa miguu ambao ni Consolata Marwa, miaka 10, mwanafunzi wa darasa la tano, shule ya msingi Nyalikungu, mkazi wa Manyasini, wilaya ya Magu na Magreth Ntemi, miaka12, mwanafunzi wa darasa la tatu, shule ya msingi Nyalikungu, mkazi wa Magu ambao walikuwa wakivuka barabara eneo la kivuko cha waenda kwa miguu (zebra) na kupelekea majeraha sehemu mbalimbali za miili yao.

Majeruhi hao walifikishwa katika hospitali ya wilaya ya Magu kwa matibabu Zaidi, wakiwa wanaendelea kupata matibabu hospitalini hapo, majeruhi Consolata Marwa alifariki dunia. Majeruhi Magreth Ntemi anaendelea kupata matibabu hospitalini hapo na hali yake inaendelea vizuri.

Baada ya ajali hiyo kutokea askari polisi wa wilaya ya Magu walifika eneo la tukio kushughulikia ajali hiyo, wakati wanafanya taratibu za kuondoa majeruhi pamoja na gari eneo la tukio ili kupisha magari mengine kupita, ndipo wananchi walianza kushinikiza kuchoma moto gari lililosababisha ajali lakini askari hawakukubaliana na shinikizo hilo, walifanikiwa kuondoa majeruhi pamoja na gari eneo la tukio ndipo wananchi walianza kuwarushia askari mawe na magari yote yaliyokuwa yanayopita kwenye barabara hiyo, kuweka vizuizi barabarani na kuchoma matairi moto ambapo abiria pamoja askari walijeruhiwa, kufuatia vurugu hizo abiria wawili pamoja na askari polisi watatu walijeruhiwa, lakini pia magari sita yaliharibiwa.

Hata hivyo, baada ya kutokea kwa vurugu hizo askari polisi wengine walifika eneo la tukio kwa haraka kwa ajili ya kuongeza nguvu na kulazimika kutuliza ghasia hizo kwa kuwatawanya wahalifu hao. Pia, katika kuhakikisha hali ya usalama ya eneo hilo inaimalika, Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa 50 waliokuwa wakifanya fujo na uharibifu huo wa mali za wananchi ambapo hali ya amani ilirejea muda mfupi.

Chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi na dereva kutojali watumiaji wengine wa barabara. Hali inayoendelea mpaka sasa ni shwari lakini pia moja ya mahitaji ya wananchi katika eneo hilo ni kuwekewa matuta ili kupunguza mwendokasi wa magari, mpaka sasa Tanroads Mwanza wameshapewa taarifa hiyo na wameahidi kulifanyia kazi. Juhudi za kumkamata dereva aliyetoroka mara baada ya kusababisha ajali zinaendelea.

Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza linawataka wakazi wote wa mkoa wa Mwanza kuheshimu kanuni taratibu na sheria za nchi kwa kutojihusisha kwa namna yoyote na vitendo vya kujichukulia sheria mkononi kwa kuwaadhibu watu waliofanya makosa mbalimbali yakiwemo ya usalama barabarani. Pia, halitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa yeyote atakayeleta uvunjifu wa amani.Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...