Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu Hemed Suleiman Abdulla amesema kukuwa kwa ufaulu Mkoa wa Kusini unguja kumetokana na juhudi zinazochukuliwa na Viongozi wa Mkoa huo kwa kuzingatia maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.

Mhe. Hemed ameyasema hayo wakati akiwasalimia wanachama wa Chama Cha Mapinduzi Jimbo la Paje na Jimbo la Makunduchi katika muendelezo wa ziara yake ya kukagua uhai wa Chama Mkoa wa Kusini Unguja.


Amesema kwa mwaka wa masomo 2022 Mkoa wa kusini Unguja umeongoza kwa ufaulu kutokana na juhudi za Makusudi zilizochukuliwa na Jumuiya ya Mwanamke Initiative Foundation (MIF) kwa kushirikiana na Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM).

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukua jitihada za kuanzia masomo ya Kidato cha Tano na kidato cha Sita Skuli ya Hasnuu Makame ili kupunguza masafa kwa wanafunzi kufuata elimu hiyo.


Aidha Mhe. Hemed amempongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuelekeza zaidi ya Bilioni 230 fedha za Mkopo wa Uviko 19 ambazo zimeelekezwa kwenye miradi mingi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Hospital za Wilaya na Mkoa, Skuli za Ghorofa pamoja na madarasa.


Aidha amewakumbusha wananchi na wanachama wa CCM kuendelea kudumisha Amani na Utulivu iliopo na kuwataka kuwa na umoja na mshikamano baina yao.


Nae Katibu wa Siasa na uhusiano wa Kimataifa Khadija Ali Salum amesema Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kusini Unguja wana kila sababu ya kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuelekeza miradi mingi ya Maendeleo Mkoani humo pamoja na kuwapongeza Wabunge, Wawakilishi na Madiwani kwa kuwatumikia wananchi wao.


Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Kusini Unguja Mhe. Rashid Hadid ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi imeelekeza miradi mingi ya maendeleo Mkoa wa Kusini Unguja na tayari Serikali imeahidi kujenga Tenki kubwa la maji mkoani humo ambalo litamaliza changamoto ya upatikanaji wa huduma ya Maji safi na Salama Mkoani humo.


Katika ziara hiyo Mhe. Hemed ameweka Jiwe la Msingi ujenzi wa Ofisi ya Jumuiya ya Maendeleo na urekebishaji wa maadili Bwejuu (JUMAMABWE) ambapo ameipongeza Jumuiya hiyo kwa juhudi zake za kusaidia kurekebisha tabia katika jamii hiyo.


Aidha ameeleza kuwa eneo hilo limezungukwa na mahoteli ya Kitalii na kuwataka wana Jumuiya hiyo kuhakikisha wanatoa elimu ya kuzingatia Maadili, silka na tamaduni kwa wenyeji na wageni wanaofika maeneo hayo.


Akisoma taarifa ya ujenzi huo Katibu wa Jumuiya ya Maendeleo na urekebishaji wa maadili Bwejuu Bwana Hassan Simai Issa ameeleza kuwa Jumuiya hiyo imeanzishwa mwaka 2018 na kupatiwa usajili mwaka 2019 ambapo ujenzi huo unaendeshwa kwa nguvu za wananchi na wadau mbali mbali wa Maendeleo waliozunguka kijiji hicho.


Amefafanua kuwa kuwepo kwa Jumuiya hiyo kutazalisha fursa mbali mbali kwa vijana, kuweka jamii katika Mila, Silka na Tamaduni, pamoja na kuinua uchumi wa Zanzibar.


Katika ziara hiyo Mhe. Hemed ameshiriki Ujenzi wa Ofisi ya CCM Jimbo la Paje, ameweka Mawe la Msingi Tawi la CCM Bwejuu Kusini, Ujenzi wa Ofisi ya Jumuiya ya maendeleo na urekebishaji wa maadili Bwejuu, Tawi la CCM Sheba, na nyumba ya maendeleo Shehia ya Kajengwa.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...