Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kupitia Mfuko wake wa Dhamana kwa Wakulima Wadogo (SCGS) imeingia mkataba wa Tshs. Bilioni 6 na SELF Microfinance Fund (SELF MF) kwaajili ya kutoa dhamana ya mikopo ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Mkataba ulioingiwa kati ya pande hizi mbili ni utawezesha TADB kuchagiza upatikanaji wa mitaji kwa wakulima kupitia SELF MF. SELF MF watatoa mikopo kwenye mnyororo wa thamani wa kilimo, mifugo na uvuvi na TADB itatoa dhamana ya hadi asilimia 50 kwa mikopo yote. Wachakataji wa mazao wadogo na wakati (SMEs), wakulima wadogo wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi watanufaika kupitia ushirikiano huu kupitia ofisi zote za SELF MF kote nchini.

Akiongea katika hafla fupi ya kutia sahihi, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB David Nghambi alisema kupitia mkataba huu, utaiwezesha SELF MF kuongeza wigo wa utoaji mikopo katika sekta ya kilimo hasa wanawake na vijana.

“Mfuko wa SCGS unaosimamiwa na TADB, unasaidia kuongeza wigo wa upatikanaji wa mikopo kwa wakulima wadogo. Kupitia ushirikiano wa TADB na taasisi nyingine za kifedha kama SELF MF. Dhamana tunayoitoa inasaidia taasisi hizi za kifedha kuvutiwa na utoaji wa mikopo katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi. Pia kupitia mitandao ya taasisi hizi za kifedha wakulima wengi hasa walioko vijijini wanafikiwa.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Self Microfinance Fund (SELF MF) Mudith Cheyo, alisema kwamba kupitia ushirikiano huu na TADB, SELF MF itaongeza wigo wa kutoa mikopo katika sekta ya kilimo na kuwezesha wakulima wadogo kufanya kilimo cha kibiashara na kupata tija. Pia alisema kuwa kupitia dhamana hii wataweza kutoa mikopo kwa riba nafuu zaidi hivyo kumnufaisha mkulima.

“Tunaishukuru TADB kwa kutuongezea nguvu kwa ajili ya kuwafikia wakulima, wafugaji na wavuvi wengi zaidi. Mikopo hii iitapatikana katika matawi yote ya SELF MF yaliyopo Tanzania. Tunatoa rai kwa wakulima wote wadogo kuja na kuchangamkia fursa hii,” alisisitiza Bw. Cheyo.

Ushirikiano na SELF MF unafanya jumla ya taasisi za kifedha zinazonufaika na mfuko wa dhamana kwa wakulima wadogo (SCGS) kutoka TADB kufika 16. Taasisi hizi ambazo ni Benki za Biashara, Benki za Kijamii na Taasisi ndogo za fedha (Microfinance Financial Institutions) zinauwezo wakuhudumia wakulima kupitia mtandao wao wa matawi zaidi ya 700 kote nchini.

Hadi kufikia mwezi Julai, 2023 jumla ya mikopo iliyodhaminiwa na TADB kupitia mfuko wa SCGS ilikuwa Tshs. 214.5 bilioni kwa wanufaikaji zaidi ya 16,200 kutoka mikoa 27 (87% ya Mikoa yote Tanzania Bara na Viziwani) na Wilaya 123 (83% ya Wilaya zote Tanzania Bara na Visiwani) ambapo zaidi ya asilimia 95 ya wanufaikaji wote ni wakulima, wafugaji na wavuvi wadogo.


Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) David Nghambi (wa pili kulia) na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa SELF MF Mudith Cheyo (wa tatu kushoto), wakitia saini mkataba wa dhamana kwa wakulima wadogo kat ya taasisi hizo mbili wenye thamani ya shilingi bilioni 6. Mwanasheria wa Benki ya TADB Emily Lukiko (wa kwanza kulia) na Mkuu wa Kitengo cha Sheria SELF MF Angela Lushagara na Frank Lawi, Mwakilishi Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu (Nyuma) wakishuhudia utiaji saini uliofanyika Jumatatu Agosti 28, 2023, katika ofisi za makao makuu ya TADB.


Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) David Nghambi (kulia) na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa SELF MF Mudith Cheyo (kushoto), wakikabidhiana mikataba ya dhamana kwa wakulima wadogo wenye thamani ya shilingi bilioni 6, itakayosaidia wakulima nchini kupata mikopo kwa riba nafuu. Mikataba hiyo imetiwa saini Jumatatu Agosti 28, 2023 katika ofisi za makao makuu ya TADB jijini Dar es Salaam.


Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) David Nghambi (kulia) na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa SELF MF Mudith Cheyo (kushoto), wakipeana mikono kama ishara ya makubaliano katika halfa ya utiaji saini mkataba wa dhamana kwa wakulima wadogo wenye thamani ya shilingi bilioni 6, ulioingiwa baina ya taasis hizo. Hafla hiyo imefanyika Jumatatu, Agost 28, 2023 katika ofisi za makao makuu ya TADB jijini Dar es Salaam.


Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) David Nghambi (kulia) akijibu swali kutoka kwa waandishi wa Habari, katika hafla ya utiaji saini mkataba wa dhamana kwa wakulima wadogo wenye thamani ya shilingi bilioni 6, baina ya TADB na mfuko wa SELF MF. Pembeni ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa SELF MF Mudith Cheyo. Hafla hiyo imefanyika Jumatatu Agost 28, 2023 katika ofisi za makao makuu ya TADB jijini Dar es Salaam.


Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) David Nghambi (kulia) na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa SELF MF Mudith Cheyo wakionyesha mikataba ya dhamana kwa wakulima wadogo wenye thamani ya shilingi bilioni 6 waliyotia saini, itakayosaidia wakulima kupata mikopo kwa urahisi. Hafla ya utiaji saini imefanyika katika ofisi za makao makuu ya TADB jijini Dar es Salaam, Agosti 28, 2023.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...