*GCLA Kuendelea kutoa elimu kwa waganga wa Tiba Asili na Tiba Mbadala kote nchini

WAGANGA Wa Tiba Asili na Tiba Mbadala Wametakiwa kujisajili ili waweze kutambulika pamoja na kupata fursa za mafunzo na miongozo ya kuweza kuuza dawa hizo nje ya Nchi.

Hayo yameeelezwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Tiba kutoka Wizara ya Afya Prof. Paschal Rugajo katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya Tiba Asili ya Mwafrika yaliyoanza Agosti 27 hadi Septemba 5 mwaka huu kwa kauli mbiu ya "Mchango wa Tiba Asili kwa Afya Kamilifu na Ustawi kwa Wote.'

Prof. Rugajo amesema, huduma zinazotolewa na waganga hao lazima zitambulike na sio kufanyika gizani na hiyo ni pamoja na kuchangia huduma katika sekta ya afya.

"Wizara ya afya kati ya vipaumbele 14 vinavyoenda kutekelezwa katika mwaka huu wa kibajeti uendelezaji wa tiba asili ni moja wapo ...Hivyo ni vyema usajili wa waganga na dawa ukazingatiwa ili kwenda sambamba katika kuboresha sekta ya afya." Amesema.

Prof. Rugajo amesema, Hospitali Saba za mikoa za Bombo-Tanga, Temeke, Mbeya, Dodoma, Morogoro, Mount Meru na Sekou- Toure zimejumuisha tiba asili kwa baadhi ya dawa ambazo zimefikia takribani dawa 19.

"Wagonjwa baada ya kuchunguzwa kitaalam watapewa chaguzi tiba asili au kizungu na niwahakikishie dawa hizi hazina madhara kwa kuwa zimefanyiwa uchunguzi wa kina na Mamlaka za kisayansi." Amesema

Pia amewaonya vishoka wanaojifanya waganga wa kienyeji kuacha kutumia mitandao ya kijamii kutangaza dawa ambazo hazijathibitishwa wala kusajiliwa na Mamlaka husika na badala yake utaratibu wa kusajili na kutangaza dawa hizo ufuatwe na hiyo ni pamoja na kutotengeneza mazingira ya kugombanisha watu kupitia ramli chonganishi.

Kwa upande wake Meneja wa maabara ya chakula na dawa kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA,) Dkt. Shimo Peter amesema Mamlaka hiyo imejipanga kuwafikia waganga asilia katika maeneo yote nchini na tayari wamefungua Ofisi katika Kanda Sita pamoja na madawati katika mikoa mbalimbali ambayo yanatoa huduma na kupunguza gharama kwa watoa huduma hao kwa kusafiri kufuata huduma.

Amesema, wamekuwa wakishiriki maonesho hayo kila mwaka sambamba na kutoa elimu pamoja na kufanya utafiti wa dawa asili ambazo Mamlaka hiyo imekuwa ikifanya utafiti kwa ukaribu kwa kushirikiana na Mamlaka nyingine za kisayansi.

Kwa upande wake Msajili wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala Dkt. Ruth Suza amesema, mwaka 2017 walianza kuhamasisha usajili wa dawa asili na kuwataka waganga hao kuendelea kusajii dawa zote za asili ili kuzitumia katika kutibu magonjwa na kupeleka nje ya nchi.

Amewataka kuzingatia sheria, kanuni na miongozo kutoka katika Baraza kwanza; kujivunia dawa za asili na kutozichanganya na dawa za kisasa kwa kuwa kufanya hivyo ni kuvunja miiiko na kanuni katika kutoa huduma.

Msajili huyo amewataka waganga hao kutochanganya Tiba Asili na ushirikina, kwa kuzingatia ushirikiana haupo katika sheria no. 23, 2022 na atakayebainika atachukuliwa hatua kali.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa magonjwa ya Binadamu (NIMR) Prof. Said Shehe Aboud amesema, taasisi hiyo ni mdau muhimu katika sekta ya Tiba Asili hususani katika kufanya na kusimamia tafiti za Tiba Asili kupitia kituo chao cha Mabibo ambacho huangalia usalama, ubora na ufanisi wa Tiba Asili.

Amesema katika maadhimisho hayo wamefanya kongamano la kisayansi lililohudhuriwa na washiriki 250 na mada 19 na mijadala ya kina kuhusiana na Tiba asilia vilijadiliwa.

Amewataka waganga wa Tiba Asili kuiamini NIMRI, kwa kuwa watawafikia ili wapate sampuli na kufanya tafiti kwa ufanisi bila kutumia hizo kwa namna nyingine.

Pia Katibu Mkuu wa Umoja wa Waganga wa Wakunga wa Tiba Asili Tanzania ( UWAWATA,) Lukas Mlipu amesema, jitihada kubwa zinazofanywa na Wizara ya afya ikiwemo kutoa elimu kwa waganga wa asili na waratibu wa huduma hizo umesaidia kwa kiasi kikubwa hususani katika uboreshaji wa utoaji huduma, utuanzaji na ufungaji wa dawa ambao unatoa imani zaidi kwa watumiaji

Pia kupitia umoja wao wameomba Serikali kupitia Wizara ya afya kuendelea kutoa elimu zaidi kwa waganga, kuwezesha upatikanaji wa vifungashio vya dawa ili viweze kuwafikia waganga asilia kuanzia ngazi ya chini kabisa pamoja na kupewa miongozo ya kuuza dawa hizo nje ya Nchi kama zinavyoingia nchini.

Kufuatia Wimbi la waganga matapeli umoja huo umeshauri kushirikishwa kwa waganga asilia wenye taaluma ili kuweza kuwatambua na hiyo ni pamoja na kukomesha rushwa katika ngazi ya vijiji.

Mkurugenzi wa Idara ya Tiba kutoka Wizara ya afya Prof. Paschal Rugajo akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya Tiba Asili ya Mwafrika yanayoendelea katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, Prof. Rugajo amewataka waganga kujisajili na kusajili dawa kama Baraza la usajili linavyoelekeza. Leo jijini Dar es Salaam.
Meneja wa maabara ya chakula na dawa kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA,) Dkt. Shimo Peter (kulia) akitoa elimu kwa mmoja ya mwananchi aliyetembelea banda la mamlaka hiyo ambayo imeendelea kufanya tafiti na kutoa elimu kwa waganga wa Tiba asili kote nchini. Leo jijini Dar es Salaam.
Msajili wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala Dkt. Ruth Suza akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho hayo na kuwataka waganga hao kutochanganya Tiba asili na ushirikina na kutekeleza majukumu yao bila kuvunja kanuni na taratibu.Leo jijini Dar es Salaam.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Rashid Mfaume akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho hayo na kuwahimiza waganga hao kutunza mazingira kwa kupanda miti katika maeneo yao. Leo jijini Dar es Salaam.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...