Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Switbert Mkama ameitaka jamii kupanda miti kuzunguka maeneo yenye miradi ili kuhifadhi mazingira na kuifanya kuwa endelevu.

Amesema hayo alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa Mradi ya Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mfumo Mfumo Ikolojia Vijijini (EBARR) katika Wilaya ya Kaskazini ‘A‘ Mkoa wa Kaskazini, Unguja - Zanzibar tarehe 19 Agosti, 2023.

Akikagua visima, ujenzi wa majengo ya vituo vya wajasiriamali wa ufugaji, ushonaji, utengenezaji wa sabuni pamoja na vitalu nyumba katika Shehia za Jugakuu, Mbuyutende na Kijini, Dkt. Mkama amesema ameridhishwa hatua iliyofikiwa.

Aidha, aliwahimiza viongozi wakiwemo masheha wa shehia hizo ambazo zimefaidika na miradi ya visima kuwasimamia wananchi kupanda miti na kuimwagilia.

“Binafsi nimeridhishwa na namna mnavyosimamia miradi hii na nawapongeza masheha kwa kuisimamia na wananchi kwa kuipokea na kushiriki kikamilkfu katika kuitekeleza, niwaombe mhakikishe inaendelea kuwa na ubora ule ule,“ amesisitiza.

Kwa vile ujenzi wa majengo ya wajasiriamali wa ushonaji na uzalishaji wa sabuni utahusisha mashine na vifaa, Dkt. Mkama alisema ni muhimu kuwepo na mpango mkakati ili mradi uwe endelevu hata pale utakapokwisha muda wake.

Alisema vyerehani vitakavyotolewa pamoja na vifaa vingine vikiwemo taa na mabomba ya maji vitahitaji matengenezo madogo madogo na kulipiwa umeme hivyo wanajamii waangalie namna ya kuuhudumia bila kusubiri serikali.

Sanjari na hilo, Naibu Katibu Mkuu amehimiza kuwa itolewe elimu ya ujasirimali kwa watakaonufaika na mradi, pia kuna umuhimu wa kuwaelimisha kuhusu utunzaji wa miundombinu.   

Mratibu wa EBARR Wilaya ya Kaskazini ‘A‘ Bw. Alawi Haji Hija amesema kupitia vitalu nyumba wananchi watafundishwa kilimo cha kustahimili ukame kwani watatumia maji ya visima kumwagilia mazao.

Pia, amesema visima hivyo vitawasaidia katika upatikanaji wa huduma ya maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani ambayo walikuwa wanashindwa kuipata kutokana na changamoto ya ukame.

Pamoja na hayo, Bw. Hija aliongeza kuwa maeneo ambayo mradi unatekelezwa yamepimwa na tayari yamewekwa katika mpango wa matumizi bora ya ardhi ili yalindwe.

Hivyo, alisema kuwa kutajengwa uzio kuzunguka eneo la mradi ili kuweka ulinzi na kuutunza huku huduma ya maji ikiendelea kuwepo kwa wananchi wa maeneo hayo.

Naye Sheha wa Shehia ya Jugakuu Bw. Ali Abdallah Pili aliishukuru na kuipongeza Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuwapelekea wananchi hao Mradi wa EBARR.

Alisema wananchi wa shehia hiyo wanafarijika kujengewa visima na hivyo ambavyo vinatumia sola, nishati ambayo ni ya gharama nafuu na wanayoweza kuimudu.

“Tunashukuru sana serikali kwa mradi huu na tumepata kikundi cha kutengeneza sabuni nzuri na umetupatia boti za kisasa za uvuvi ambazo wananchi wetu wanazitumia katika shughuli kuvua samaki na hivyo kujipatia kipato,” alisema.

Hata hivyo, sheha huyo aliwashauri wanakikundi kuienzi na kuitunza miradi hiyo na kushirikiana kikamilifu katika shughuli mbalimbali zinazohusu miradi hiyo.

Miradi iliyotembelewa na kukagualiwa na Naibu Katibu Mkuu Dkt. Mkama katika eneo la Matemwe Wilaya ya Kaskazini ‘A‘ imegharimu kiasi cha shilingi milioni 760.

Mradi wa EBARR unaofadhiliwa na Mfuko wa Nchi zinazoendelea kupitia Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF) unatekeleza pia katika wilaya za Mpwapwa (Dodoma) Simanjiro (Manyara), Mvomero (Morogoro) na Kishapu (Shinyanga).

Kupitia mradi huo wananchi wan maeneo yenye ukame wanawezeshwa kujipatia kipato kwa njia mbadala bila kujihusisha na vitendo vya uharibifu wa mazingira vikiwemo ukataji miti kwa ajili ya nishati na unyweshaji wa mifugo kwenye vyanzo vya kwa kuwa wanajengewa miundombinu kwa ajili hiyo.

Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Switbert Mkama akikagua mradi wa kisima cha maji katika Shehia ya Jugakuu, Matemwe wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa Mradi ya Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mfumo Mfumo Ikolojia Vijijini (EBARR) katika Wilaya ya Kaskazini ‘A‘ Mkoa wa Kaskazini, Unguja - Zanzibar tarehe 19 Agosti, 2023.

Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Switbert Mkama akikagua mradi wa ujenzi wa jengo la wajasiriamali wa utengenezaji wa sabuni katika Shehia ya Mbuyutende, Matemwe wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa Mradi ya Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mfumo Mfumo Ikolojia Vijijini (EBARR) katika Wilaya ya Kaskazini ‘A‘ Mkoa wa Kaskazini, Unguja - Zanzibar tarehe 19 Agosti, 2023.

Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Switbert Mkama akikagua mradi wa ujenzi wa jengo la kituo cha ushonaji katika Shehia ya Kijini, Matemwe wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa Mradi ya Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mfumo Mfumo Ikolojia Vijijini (EBARR) katika Wilaya ya Kaskazini ‘A‘ Mkoa wa Kaskazini, Unguja - Zanzibar tarehe 19 Agosti, 2023.

Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Switbert Mkama (wa pili kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Makamu wa Rais Zanzibar Bi. Farhat Mbarouk (kulia) wakati akitoa maelezo kuhusu mradi wa kisima katika Shehia ya Jugakuu, Matemwe, unaotekelezwa kupitia Mradi ya Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mfumo Mfumo Ikolojia Vijijini (EBARR) katika Wilaya ya Kaskazini ‘A‘ Mkoa wa Kaskazini, Unguja - Zanzibar tarehe 19 Agosti, 2023.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...