Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amewataka Watumishi wa Shamba la Miti Sao hill Wilayani Mufindi kufanya kazi kwa uadilifu huku akiwataka  kutanguliza mbele  uzalendo kwa kulinda rasilimali hizo

Ameyasema hayo jana Agosti 10,2023 alipokuwa akizungumza na Watumishi wa Shamba hilo  katika kikao kilichofanyika kwenye ofisi za Shamba Wilayani Mufindi Mkoani Iringa.

"Hatutamvumilia mtumishi yeyote anayefanya kazi kwa mazoea" Mhe. Masanja amesisitiza.

Aidha, ameelekeza wahifadhi wa shamba hilo kusimamia vyema maeneo ya misitu yanayovamiwa na wananchi na kuwaondoa wavamizi.

Kuhusu suala la wawekezaji wa viwanda vya uchakataji wa mazao ya misitu, Mhe. Masanja amesikitishwa na ununuzi wa miti isiyokomaa inayopelekea kutoa bidhaa zisizo la viwango na kuchafua sifa ya Tanzania.

"Tunakataza uvunaji wa miti ambayo haijakomaa.Tuendelee kuhamasisha uwekezaji wa mashamba ya miti ila uvunaji uwe unaokidhi vigezo" Mhe. Masanja amefafanua na kuongeza kuwa Serikali  inatamani kushirikiana na wawekezaji kukubaliana juu ya uvunaji wa miti iliyo bora.

Katika hatua nyingine, Mhe. Masanja ameitaka Menejimenti ya shamba hilo kushughulikia suala la changamoto ya ukaguzi wa mali zinazoenda bandarini.

"Afisa ukaguzi ahakikishe bidhaa inayoondoka hapa ifanane na inayofika bandarini.Ukaguzi ufanyike vizuri na mzigo ufungwe vizuri" amesema.

Awali, alipokuwa akizungumza na wawekezaji katika viwanda vya uchakataji wa mazao ya misitu kwa nyakati tofauti, Mhe. Masanja aliwaomba wawekezaji hao kuhakikisha wanatumia mazao ya misitu yaliyokomaa ili kuzalisha bidhaa bora.


Ziara ya Naibu Waziri Masanja Mkoani Iringa ni mwendelezo wa ziara zake za kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi na kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...