Na Munir Shemweta, WANMM MAKETE

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewataka wamiliki wa ardhi nchini kuhakikisha wanamilikishwa maeneo yao kwa kupatiwa hatimiliki za ardhi ili kuwa na salama ya miliki zao.

Dkt Mabula alisema hayo tarehe 10 Agosti 2023 wilayani Makete mkoani Njombe wakati wa kukabidhi hatimiliki za ardhi kwa wananchi wa wilaya hiyo akiwa katika ziara yake ya siku tatu katika mkoa huo.

Alisema, wananchi wa Makete waliojitokeza kuchukua hati mara baada ya kukamilisha taratibu za umilikishwaji wamechukua uamuzi sahihi unaoenda kuwahakikishia usalama wa milki zao.

Alibainisha kuwa, mmiliki wa ardhi mwenye hati mbali na kuwa na salama ya miliki yake lakini hati hiyo inampa fursa nyingi ikiwemo kuhukua mikopo benki pamoja na kuitumia kama dhamana.

Hata hivyo, Dkt Mabula alishangazwa na idadi ndogo ya wananchi wanaojitokeza kuchukua hati ambapo alisema kati ya wamiliki 88 wa wilaya ya Makete waliothibitisha kwenda kuchukua hati katika tukio la kukabidhi hati ni wamiliki 25 tu waliojitokeza na kukabidhiwa hati zao.

‘’Hii mara nyingi inatokea wanaothibitisha kwenda kuchukua hati ni wengi lakini wanaokwenda kuchukua ni wachache sasa mimi naomba ninyi mkawe mabalozi pengine wasiokuja wameona wamekuwa wakidanganywa na leo wangedanganywa ‘’ alisema Dkt Mabula.

Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Serikali ya Awamu ya Sita imeamua kuwawezesha wananchi kupitia ardhi zao na uwezeshwaji huo ni kuwa na umiliki halali wa ardhi unaowapa salama ya maeneo yao sambamba na kuwawezesha kutumia hati katika kujiwezesha kiuchumi.

Alisema, wamiliki wa ardhi wanaojua alama za mipaka katika maeneo wanayomiliki ni tofauti na wale wanaomiliki maeneo wakiwa na hati zao na kueleza kuwa wanaopatiwa hati wana shughuli nyingi za kimaendeleo wanazoweza kuzifanya kupitia hati.

Kwa upande wao Wananchi wa Makete waliokabidhiwa hati milki za ardhi waliishukuru Wizara ya ardhi kupitia waziri mwenye dhamana kwa kuwapatia hati milki za ardhi amabpo walisema huko nyuma ilikuwa vigumu kuzipata.

Faidon Kyando mkazi wa Makete aliyekabidhiwa jumla ya hati sita na Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula alisema hakuamini alipopigiwa simu akitakiwa kwenda kuchukua hati za maeneo yake hasa akiwa na kumbukumbu za huko nyuma kusikia kwamba kuna mtu alichukua hati kwa kiasi cha milioni mbili.

‘’Baada ya kukuona mama umefika hapa na kutushika mkono kwa kutukabidhi hati ambapo kama mimi nilisikia mwaka 1998 kuna mtu alichukua hati mkoani mbeya kwa milioni 2 na ndiyo maana niliposikia tunakuja kukabidhiwa hati sikuamini’’ alisema Kyando.

Jumla ya wamiliki 25 kati ya 88 wa ardhi katika wilaya ya makete mkoani Njombe walikabidhiwa hati milki za ardhi na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula katika tukio lililohudhuriwa pia na Mkuu wa mkoa wa Njombe Athony Mtaka pamoja na mbunge wa jimbo la Makete Festo Sanga.Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi hati milki ya ardhi mmoja wa wananchi wa wilaya ya Makete wakati wa ziara yake ya siku tatu mkoani Njombe tarehe 10 Agosti 2023. Wa pili kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Njombe Athony Mtaka na wa kwanza kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Makete Festo Sanga.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimuonesha Faidon Kyando mkazi wa Makete namna anavyoweza kujua kiasi anachotakiwa kulipa kodi ya pango la ardhI wakati alipokabidhi hati kwa wananchi wa wilaya ya Makete mkoani Njombe tarehe 10 Agosti 2023.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na viongozi, watendaji wa sekta ya ardhi na wananchi wa Makete aliowakabidhi hati wakati wa ziara yake ya siku tatu mkoani Njombe tarehe 10 Agosti 2023. Wa pili kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Njombe Athony Mtaka na wa kwanza kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Makete Festo Sanga.
Mbunge wa jimbo la Makete Festo Sanga akizungumza katika zoezi la utoaji hati kwa wananchi wa wilaya ya Makete wakati wa ziara ya Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula wilayani humo mkoa wa Njombe Agosti 10, 2023. Kushoto ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Ardhi Sheushi Mbuli na wa pili kulia ni Mkuu wa mkoa wa Njombe Anthony Mtaka.

Mkuu wa mkoa wa Njombe Athony Mtaka akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula katika wilaya ya Makete mkoani Njombe Agosti 10, 2023. Kushoto ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Ardhi Sheushi Mbuli na wa pili kushoto ni Mbunge wa jimbo la Makete Festo Sanga.Sehemu ya wananchi waliokabidhiwa hati miliki za ardhi wakimskiliza Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula wakati wa ziara yake ya siku tatu mkoani Njombe tarehe 10 Agosti 2023.

(PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...