NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA

BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania(BAKWATA) Mkoa wa Mwanza, limesimika uongozi wa Msikiti wa Masjid Noor na kukemea baadhi ya taasisi zilizo chini ya baraza hilo zinazosababisha mgogoro na uvunjifu wa amani kwa kusajiliwa katika taasisi mbili tofauti.

Limesema haliko tayari hata kwa dakika moja kupoteza dhiraa (kipimo cha mkono kuanzia vidoleni hadi katika kiwiko)moja ya ardhi yake inayoisimamia na kuwataka Waumini wa Dini ya Kiislamu wakiwemo wa Msikiti wa Noor,wasilishwe matango pori na wasioitakiwa nchi amani na Uislamu.


Hayo yameelezwa leo na Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke, wakati akitoa ufafanuzi kuhusu kusimikwa kwa uongozi wa Msikiti Masjid Noor uliopo Mtaa wa Uhuru jijini Mwanza, kupandishwa hadhi kuwa wa Wilaya ya Nyamagana.

Sheikhe Kabeke amesema msikiti huo umepewa hadhi kuwa wa Wilaya na Baraza la Masheikhe la Wilaya Nyamagana na kumpendekeza Sheikhe Musa Bin Rajab wa Msikiti wa Mabatini,kuwa Imamu wa msikiti huo kutokana na Sheikhe wa Wilaya hiyo kutingwa na majukumu mengi.

Amesema BAKWATA ikishirikiana na vyombo vyake waliamua kwenda kuswali Msikiti wa Masjid Noor kwa nia ya kuwafahamisha waumini kuwa msikiti huo unaomilikiwa na BAKWATA kwa mujibu wa sheria,umepandishwa hadhi kuwa wa Wilaya ya Nyamagana.

Sheikhe Kabeke amesema BAKWATA hawana tatizo isipokuwa jambo lilipo wanatofautiana nani aongoze hapo na hawana sababu ya kutumia nguvu kubwa na kuhoji kwa nini watumie nguvu na kwa jambo gani ilhali wao ni wamiliki?

Kwa masikitiko makubwa amesema vyombo vinavyosajili taasisi za dini kuna hila na ujanja ujanja unafanyika na haelewi vinaitakia nini nchi hii,kama vinaitakia mema huo mchezo unaoonekana si Mwanza tu ni Tanzania kote,kelele zipo za dhuluma katika shule na msikiti,kinatokea kikundi kinajisajili,usajili wao unafanyika taasisi nyingine nje ya BAKWATA.

Sheikhe huyo wa Mkoa wa Mwanza amesema taasisi inayoonewa sana ni BAKWATA,hivyo wameamua uonevu huo uondoke na ukome,mtu kwenda katika msikiti wa BAKWATA akajisajili kisha anakwenda kwenye vyombo vingine vya usajili anakubaliwa,huo ni kuleta mgororo na kuvuruga amani.

“Baraza limeona msikiti huu ulivyo utabaki kuwa wa Wilaya ya Nyamagana na tunachopigania ni maslahi mapana ya Uislamu na Taifa letu,sote ni raia tuwe na busara na jicho la tatu, asije mtu akapitia katika hili kuzua mgogoro ambao haupo,Mwanza imetulia na vitu vya documentation (nyaraka) ni vizuri vikazingtiwa,”amesema.

“Mtatusaidia (wana habari) kuwaelimisha Watanzania na waislamu hasa wa Mbugani na Wilaya ya Nyamagana,ifahamike msikiti huo una historia ndefu tangu East African Muslimu Wallfare Society,ni mali ya BAKWATA wala haijakurupuka.The Register of Trustee Masjid Noor iliposajiliwa mwaka 2010 iliuchukua kuuendesha,”amesema.

Sheikhe Kabeke amevitahadharisha vyombo vya usajili wa taasisi za dini vichukue tahadhari vinginevyo vinaleta fujo na kusababisha migogoro vinaposajili taasisi iliyokwisha kusajiliwa katika taasisi nyingine.

“Chonde chonde tunawatahadharisha wanaosajili,amani ya Tanzania kwanza, pia kuna dalili za kuwahamasisha waumini na kuwalisha matango pori,wasilishwe sumu kuwa BAKWATA imevamia msikiti hapana,ni msikiti wao tangu 1970,”amesema na kuongeza;

“Kwa maslahi mapana ya amani,hata jeuri hii ya kudai mali yetu tunaifanya sababu nchi imetulia,nchi ina amani huwezi kusema tu nataka mali yangu damu inamwagika maana yake nini,kwanza unataka kuwaswalisha akina nani wakati damu imemwagika.

“Pia heshima ya dini yenyewe na kwa nafasi yangu Sheikhe wa Mkoa waislamu hawa wote ni wangu natakiwa kuwakumbatia kwa huruma,maslahi ya heshima ya amani na dini yetu, msikiti ni wetu wenzetu hao wataendelea kuutumia kwa ibada.”


Kiongozi huyo wa kiroho amesistiza kuwa hawako tayari kupoteza hata dhiraa moja ya ardhi wanayoimiliki na kuisimamia na Watanzania wafahamu ukweli utabaki hivyo kuwa, mali ikiwa BAKWATA ni ya waislamu wote,Bodi ya Wadhamini itawasemea na kusimamia mali hizo kwa niaba yao.

“Baadhi ya bodi sisemi kwa ubaya zipo zinazofanya vizuri,shida iliyopo bodi zilizosajiliwa kwa ujanja ujanja zingine utakuta za familia moja,mapato hayasomwi,vikao hawafanyi bodi zipo tu,kibaya zimesajiliwa katika kiwanja cha BAKWATA,wanapata wapi ridhaa ya kujisajili katika taasisi zingine? Amehoji.

Sheikhe Kabeke amesema wamefikia hatua hiyo si kwa ubabe kwani nchi mihimili mitatu (Serikali,Bunge na Mahakama), inaendeshwa kwa utawala wa sheria ambapo kazi ya mahakama ni kutafsiri sheria na kutoa haki. Pia viongozi waliopewa dhamana na BAKWATA wanajitambua na hawawezi kukimbilia polisi iwasaidie kudai haki yao,wanaoona wanaonewa ama wamedhulumiwa waende,kwa sababu hawana mgogoro wa ardhi bali ulikuwepo mgogoro wa uongozi wa msikiti na tayari umepatikana.

Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke (kuhoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo kuhusiana na kupandishwa hadhi Msikiti wa Masjid Noor kuwa wa Wilaya ya Nyamagana.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...