Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt Grace Maghembe katikati wakati akichangia mada katika mkutano wa masuala ya lishe na afya,uliofanyika sambamba na mkutano wa Mifumo ya Chakula Afrika( AGRF), unaoendelea katika ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam.

ILI kuipunguzia serikali mzigo wa kutibia magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari na shinikizo la damu yanayosababishwa na mpangilio mbovu wa vyakula,jamii imeshauriwa kuzingatia suala la lishe bora katika familia zao.

Hayo yalibainishwa jana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt Grace Maghembe wakati akichangia mada katika mkutano wa masuala ya lishe na afya,uliofanyika sambamba na mkutano wa Mifumo ya Chakula Afrika( AGRF), unaoendelea katika ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere uliopo jijini Dar es salaam.

Dkt Magembe alisema kuwa,serikali inatumia gharama nyingi kutibu magonjwa yasiyoambukiza yanayosababishwa na mpangilio mbovu wa vyakula, hivyo kila mmoja anapaswa kuangalia suala zima la lishe.

"Serikali inatumia gharama kubwa kutibu magonjwa yasiyoambukiza,hivyo kila mmoja anapaswa kuliangalia hilo na wasisubiri serikali pekeyake,"alisema Dk Magembe.

Hata hivyo alisema ifike wakati nchi za Afrika kuwa na Mpango wa kusaidia kaya maskini kama ilivyo hapa nchini,ili kuepusha suala la utapia mlo katika maeneo mbalimbali.

Alisema kuna maeneo wanalima vyakula kwa wingi,lakini cha kushangaza mikoa hiyo inakuwa na tatizo la utapiamlo na hii ni kutokana na kutokujua namna ya kupangilia mlo kamili.

Kutokana na hilo alisisitiza elimu ya ulaji vyakula vyenye kuleta virutubisho izingatiwe na ikiwemo kupangilia huku akisisitiza jamii ipende kutumia vyakula vya asili na si chipsi na baga ambazo watoto wengi huzipenda.

Alisema jamii kubwa ina changamoto ya kutokuangalia suala la mlo kamili,isipokuwa wanajali kushiba tu na kuongeza wanapokula wanapaswa kuangalia suala la mboga za majani,maji,wanga,vitamini na proteini.

Dkt. Maghembe alisema lazima tuzijenge familia kula mlo kamili, ikiwemo kupanda mboga za majani badala ya kupanda maua pekeyake.

Alisema jamii haiwezi kuepukana na lishe mbaya kwa kuisubiria serikali ihamasishe kula mlo kamili,badala yake wanapaswa kuanzia kwenye familia kwa kuwafundisha watoto wao kuwa mboga ndio chakula cha maana.

Amewataka wataalamu wa lishe kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa matumizi ya vyakula vya asili na iachane na Chip's zege, tomato na soda ambavyo huongeza mafuta kwenye mwili,sukari na kusababisha magonjwa yasiyoambukiza.

Kuhusu suala la ugumu wa upatikanaji wa mlo kamili Dkt. Maghembe alisema kuwa serikali imeweka juhudi na kuanzisha Mfuko wa kunusuru Kaya masikini, (TASAF), hivyo na Afrika kwa ujumla ifike mahala kuwatengea bajeti kwa ajili ya kupewa kaya masikini ili waweze kula mlo kamili.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...