Na Said Mwishehe, Michuzi TV -Mbarali

HATIMAYE Rais Dk. Samia Suluhu Hassam amesikia kilio cha wananchi wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya kuomba waendelee kuitumia kwa kilimo sehemu ya eneo la Bonde la Mto Usangu wakati hatua za kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa GN28 ukiendelea.

Wananchi hao wakiongozwa na mgombea ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bahati Ndingo, viongozi wa Chama wa wilaya na Mkoa wa Mbeya kwa ujumla  waliwasilisha ombi hilo kwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana alipotembelea baadhi ya maeneo yenye mgogoro.

Kinana amewaambia wananchi wa Mbarali mkoani Mbeya kuwa Rais Dk. Samia amekubali ombi la wana Mbarali na kuruhusu kuendelea na kilimo kwa muda katika eneo lililozuiwa kupitia tangazo la GN 28.

Awali Serikali kupitia Kamati ya Mawaziri wanane ilitoa katazo kwa wananchi waliopo katika sehemu ya eneo la bonde la Usangu kuacha kulima kwa kuwa wanaharibu vyanzo vya maji vya Mto Ruaha Mkuu ambao unapeleka maji katika Mto Ruaha.

Hivyo tangu kutolewa kwa katazo hilo wananchi wamekuwa wakililalamikia na kuomba Serikali kuliondoa katazo hilo.

Akizungumza wakati akihitimisha kampeni za CCM katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mbarali mkoani Mbeya Makamu Mwenyekiti Kinana alisema mgombea ubunge, madiwani, viongozi wa chama na wananchi walimueleza kwa nini asimuombe Rais waendelee kulima wakati suala hilo linazungumzwa.

“Nimemuomba Rais jana jioni nikamwambia wananchi wa Mbarali wanaomba waendelee kulima kwa sababu msimu unaanza mwezi ujao na Rais akasema sawa waendelee.

“Ila tu kwa yale maeneo ambayo yanavyanzo vya maji, kwa yale maeneo yote yaliyoruhusiwa mwaka jana Rais amekubali muendelee kulima,” amesema Kinana alipokuwa akielezea changamoto hiyo ambayo imeibua malalamiko mengi ya wananchi.

Kinana akielezea zaidi amesema amepata nafasi ya kupita katika baadhi ya vijiji ambavyo vina mgogoro na amekutana na wananchi ambao walimvaa na kumpa ujumbe kwani kila mtu anajua GN 28.

“Na mimi niwaahidi mambo yafuatayo la kwanza watu wote wanaioshi katika maeneo hayo waliambiwa waache kulima, wakamuomba Rais kwa sababu serikali haikua tayari waendelee kulima.

“Rais akasema anaruhusu kwa mwaka mmoja sasa jana Bahati na madiwani wawili wakanivaa wakaniambia matatizo hayajatatuliwa bado, mchakato wa tathimini bado unaendelea, fidia haijalipwa, mawe ya alama wananchi hawajashirikishwa,” amesema.

Hivyo kutokana na maelezo hayo Kinana amesema tayari amezungumza na Rais Samia na ameruhusu wananchi waendelee na shughuli za kilimo.

Akizungumzia ombi la mgombea ubunge kuhusu ujenzi wa barabara iliyokaa muda mrefu ya kutoka Lujewa, Madibila hadi Mafinga, Kinana amesema atawasiliana na wahusika (Waziri wa Ujenzi) barabara hiyo haiwezi kuishia katika makaratasi, bali ni lazima zichukuliwe hatua.

“Nimemzikiliza Mwenyekiti wa Wabunge wa CCM Mkoa wa Mbeya amesema hivi; shughuli za uchumi Mkoa wa Mbeya zinategemea sana shughuli za uchumi za Wilaya ya Mbarali. Ukizungumza uzalishaji Mbarali, ukizungumza matrekta Mbarali, ukizungumza viwanda Mbarali.

“Ukizungumza bodaboda Mbarali, ukizungumza vijana kujiajiri Mbarali. Lazima tuwasikilize wananchi wa Mbarali na mkoa mzima wa Mbeya,” amesema Kinana.

Kuhusu mgombea ubunge wa jimbo hilo katika uchaguzi mdogo unaofanyika leo, ameowamba wananchi kumchagua Bahati huku akieleza kuwa kura haipatikani kwa matumaini bali kwa kupiga kura.

Awali wakati akiomba kura Bahati ametumia nafasi hiyo kuelezea masuala mbalimbali yanayoendelea katika wilaya hiyo yakiwemo maendeleo makubwa ambayo yamefanywa na serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia.

Pia, amezungumzia changamoto ya migogoro ya ardhi ambayo inakwamisha shughuli za maendeleo na uchumi wa wananchi wa Mbarali.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...