Na Pamela Mollel
MHIFADHI Mkuu anayesimamia Kitengo cha Utalii Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi Hapyness Kiemi amesema uwepo wa Mradi wa Mbwamwitu na Faru ndani ya hifadhi hiyo umefanya idadi ya wageni kuongezeka kwa asilimia 100 kwa mwaka 2022/2023.
Kiemi ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea hifadhi hiyo hivi karibu ambapo ametumia nafasi hiyo kuelezea ongezeko la watalii katika hifadhi hiyo kutokana na uwepo wa wanyama hao adimu.
Amesema bado wana matarajio ya kuongezeka kwa wageni hususan wageni wa ndani na ongezeko hilo pia limetokana na uwepo wa filamu ya Royal Tour iliyozinduliwa na Mh.Rais.
“Hifadhi yetu bado ina matarajio ya kuwa na ongezeko la wageni hususan wageni wa ndani ambao wanakuja kutazama Faru na Mbwamwitu na katika kipindi cha miaka miwili ijayo tunatarajia wageni kuongezeka zaidi, "amefafanua Kiemi.
Kwa upande wake Mhifadhi Mwandamizi anayesimamia miradi hiyo ya wanyama adimu Emanueli Sisya ameeleza kuwa hifadhi ya Mkomazi ilichanguliwa kama hifadhi ya uzalishaji Mbwa mwitu kutokana na eneo hilo kushabihiana na mazingira wanayoishi mbwa hao
Sisya amefafanua kuwa mradi huo ulianza ukiwa na mbwa mwitu 25 ila kwa sasa wameongezeka na kufikia zaidi ya 300 ambapo huwaachia mbwa hao katika mifumo ya kiiolojia na kwa sasa lengo lao ni kuzalisha na kuwarudisha katika maeneo yao ya asili
“Mbwamwitu ni wanyama wanaoishi kimakundi kwa maana ya kifamilia hivyo tunawaachia katika makundi tukiangalia mbwamwitu wenye umri unaolingana, amesema Sisya
Aidha amezitaja faida zinazotokana na mbwamwitu kuwa ni kivutio kikubwa cha utalii hususan kwa wageni ambao wengi wamekuwa wakitembelea hifadhi hiyo kutokana na uwepo wa kivutio hicho cha mbwa mwitu,na hivyo wana mpango wa kuendelea kutanua kwa kujenga boma lingine ili kuwezesha wageni kuendelea kuwaona na utalii kukua
Kwa upande wake Mratibu wa Wanyama hao Jackson Lyimo amezitaja changamoto kubwa wanazokabiliana nazo mbwamwitu kuwa ni pamoja na migongano baina ya wafugaji na wanyama hao kwa kuwa wanawaona kama wanyama waharibifu
Lyimo amefafanua tangu kuzalishwa kwa mbwamwitu katika hifadhi ya Mkomazi tayari wameachia makundi 15 yenye mbwa zaidi 209 ikiwa ni kurudisha ikolojia ya hifadhi ya Mkomazi kwa kuwarudisha katika hifadhi ambazo zilikuwa na mbwamwitu ila wakatoweka kutokana na sababu mbalimbali
“Mbwa hawa pia wanakutana na changamoto za magonjwa pindi wanapokutana na wanyama wakufugwa lakini pia binadamu ni adui mkubwa wa wanyama hao kwa kuwa wanamuona kama mharibifu”.Alifafanua Lyimo.
Mradi wa mbwa mwitu katika hifadhi ya Mkomazi ulianzishwa mwaka 1995 ukiwa na lengo la kuzalisha mbwa mwitu na kuwarudisha katika maeneo yao ya awali kutokana na kuendelea kutoweka kutokana na sababu mbalimbali
Jackson Lyimo,mratibu wa mradi wa Mbwa mwitu hifadhi ya Mkomazi akizungumza na vyombo vya habari hifadhi hapo
Emanuel Sisya,Mhifadhi mwandamizi,hifadhi ya Mkomazi anayesimamia mradi wa wanyama Adimu


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...